The House of Favourite Newspapers

Leo ni Karume Day

0

DAR ES SALAAM: Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo wanaadhimisha siku ya kumbukumbu ya mauaji ya Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Abeid Amani Karume  (pichani), yaliyofanyika Aprili 7, 1972 katika Ofisi Kuu za chama, Kisiwandui Mjini Unguja.

Mzee Karume ndiye kiongozi wa Zanzibar aliyeingia makubaliano na Tanganyika, chini ya Mwalimu Julius Nyerere kuunganisha nchi zao Aprili 26, 1964, miezi mitatu baada ya kufanywa kwa mapinduzi ya visiwa hivyo vilivyokuwa chini ya utawala wa kisultani Januari 12, 1964.

Maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila mwaka, huambatana na dua maalum, uwekwaji wa mashada ya maua katika kaburi la Karume lililopo katika viwanja vya ofisi ya CCM Kisiwandui na shughuli zingine za kijamii.
Kiongozi huyo wa kwanza wa Zanzibar huru, aliuawa kwa kupigwa risasi wakati akicheza bao ndani ya ofisi za chama chake cha ASP, baada ya watu wanne waliokuwa na silaha kuingia na kumpiga risasi zilizomuua yeye, pamoja na kuwajeruhi maofisa wengine wawili wa juu wa chama chake.

Katika muda mfupi alioiongoza Zanzibar, Karume aliiwezesha nchi hiyo kuwa ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kuwa na kituo chake cha televisheni kilichoonesha kwa rangi, sambamba na kusimamia ujenzi wa mradi mkubwa wa maghorofa ya Michenzani ili kuwapa wananchi wa kisiwa hicho makazi ya uhakika

Leave A Reply