The House of Favourite Newspapers

Licha ya Corona… Harmo Apasua Anga!

0

LICHA ya janga la maambukizi ya Virusi vya Corona kumtibulia mambo mengi staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul Kahali ‘Harmonize’ anazidi kupasua anga.

 

Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa, ndani ya miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka 2020, tayari ameshafanya makubwa.

 

Pia gazeti hili linafahamu kuwa, baada ya kuondoka kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) iliyo chini ya mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Harmonize au Harmo alitabiriwa mengi likiwemo suala la anguko la kimuziki. Tofauti na utabiri huo, Harmo anazidi kupaa kimuziki na kiuwezo wa kipesa (utajiri).

Harmo amefanya mambo makubwa likiwemo kuzindua albam yake ya Afro East kwa kishindo pale Mlimani City jijini Dar.

 

Albam hiyo ina jumla ya nyimbo 18 na uzinduzi wake ulikuwa ni wa gharama.

Hata hivyo, Harmo hakuishia hapo kwani hivi karibuni amefanikiwa kumiliki ofisi zake baab’kubwa zilizopo kwenye mjengo wa kifahari uliopo Mbezi-Beach jijini Dar.

 

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko kuhusu mjengo huo, mmoja wa mameneja wa Harmo aitwaye Mchopa alisema kuwa, ni kweli amefungua ofisi zake zilizopo kwenye mjengo huo Mbezi-Beach.

KUZINDUA STUDIO ZA KIBABE

“Ni kweli hizo ni ofisi mpya za Konde Gang, zipo maeneo ya Mbezi-Beach na kutakuwa na kila kitu ikiwemo studio na zitazinduliwa rasmi muda si mrefu.

 

“Watanzania wanaomsapoti Harmonize ndiyo wamemfanya kufikia hapo alipo hivi sasa, kwa hiyo tunatoa shukrani sana na waendelee kutusapoti kwa kila namna moja hadi nyingine kwa kuwa mchango wao ni mkubwa sana na tunauthamini sana.

 

“Kuhusu gharama ambazo zimetumika ni kiasi kikubwa sana ambacho si vizuri kukitaja kwa sababu ukitaja mwingine hataamini, ataona kama unadanganya. Kwa hiyo ibaki hivyohivyo kwamba tumepata ofisi mpya za Konde Gang na tunaomba hili janga la Corona lipite ili tuweze kuendelea na majukumu ya kutangaza Albam ya Afro East kila kona ya Tanzania na nje ya nchi.

 

MIPANGO KABLA YA CORONA

“Huo ndiyo ulikuwa mpango wetu kabla ya Corona, lakini janga hili likipita tutaendelea.

“Cha msingi ni kujilinda na kufuata yale ambayo tunaelekezwa na Wizara ya Afya ili tuweze kujilinda.

“Ni matumaini yangu makubwa kwamba mambo yatakwenda kuwa sawa,” alisema Mchopa.

 

HAJANUNUA MJENGO

Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kwamba, mjengo huo si mali ya Harmo na hajanunua kama taarifa za mitandaoni zilivyodai, bali amepangisha kama ilivyo kwa aliyekuwa bosi wake, Diamond au Mondi.

 

Mbali na hilo, pia wikiendi iliyopita, Harmo alimsaini msanii wake wa kwanza kwenye lebo yake aliyetajwa kuwa na kipaji kikubwa cha muziki aitwaye Ibra.

Hata hivyo, mafanikio ya mtu yanapimwa kwa vigezo mbalimbali ikiwemo mali anazozimiliki na jinsi anavyoishi.

 

Wasanii wengi Bongo wamekuwa na majina makubwa, lakini ukiangalia mali walizonazo ni za kawaida au hazifanani na ukubwa wa majina yao.

Lakini kwa Harmo mambo ni tofauti, kwani akiwa na miaka minne tu kwenye muziki, tayari ana mafanikio ya kiasi chake.

 

MBALI NA OFISI

Uchunguzi wa Gazeti la Risasi Mchanganyiko ulibaini kwamba, mbali na ofisi hizo ambazo ni levo ya zile za Wasafi, Harmo anamiliki magari mbalimbali.

 

Miongoni mwa magari anayomiliki ni Toyota Alphard ya mwaka 2018 lenye thamani ya Dola za Kimarekani 10,378 (zaidi ya shilingi milioni 23.8 za Kitanzania). Ukiachana na Toyota Alphard, Harmo pia anamiliki gari aina ya Audi TT RS Roadster (open-roof) lenye thamani ya Dola za Kimarekani 28,535 (zaidi ya shilingi milioni 65 za Kibongo).

Gari la tatu analomiliki Harmo ambalo huwa analitumia kwenye misafara yake mara nyingi kama ile ya shoo na akiwa amepata mwaliko sehemu kwa ajili ya sherehe au mikutano ni Land Cruiser V8, toleo la mwaka 2016 lenye thamani ya Dola za Kimarekani 41,082 (zaidi ya shilingi milioni 94 za Kitanzania).

 

KIASI CHA PESA

Kwa mujibu wa Mtandao wa Celebrities Worth unaodili na kujua kiasi cha pesa wanachomiliki mastaa wa Afrika Mashariki, ripoti ya mwaka 2020 inaonesha Harmo ana utajiri unaokadiriwa kufikia Dola za Kimarekani milioni moja (zaidi ya shilingi bilioni 2 na ushee za Kibongo).

STORI | Neema Adrian, Risasi

Leave A Reply