LICHA YA JPM KUSEMA WAACHWE…RAIA 4 WAPIGWA RISASI !

INAUMA sana! Watu wanne katika Kata ya Kapalamsenga, Wilaya ya Tanganyika, mkoani Katavi, wamepigwa risasi na askari wa wanyamapori, ambapo mmoja wao aitwaye Kashinje Yabona (38), amefariki dunia. 

 

Kisa cha wananchi hao kupigwa risasi, kinaelezwa kuwa ni kuishi katika eneo ambalo linadaiwa ni njia za wanyamori (shoroba), waliopo katika Hifadhi ya Katavi, jirani na eneo hilo. Tukio hilo limetokea ikiwa ni siku chache tangu Rais Dk. John Magufuli atoe tamko la kukataza wananchi wanaoishi jirani na hifadhi za taifa nchini, kufukuzwa holela na kuharibiwa mazao yao.

 

Katika maagizo yake kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangala, Rais Magufuli alisema siyo jambo la kibinadamu, kuharibu mazao ya wananchi hasa yale ya msimu na kuwafukuza katika maeneo yao bila utaratibu kwa maelezo kuwa, binadamu wana thamani kuliko wanyama, akashauri kuwe na njia ya kuhakikisha hayo hayafanyiki.

 

HABARI KAMILI

Akisimulia mkasa mzima mbele ya mwandishi wa Uwazi, Esta Masanja ambaye ni mjamzito wa miezi nane, mkazi wa eneo hilo, alisema tukio la Kashinje kuuawa na wakazi wengine kujeruhiwa lilitokea Januari 14, mwaka huu, majira ya saa 5 asubuhi.

 

“Siku moja kabla ya tukio hilo, askari hao walinikuta shambani, nikashangaa wakianza kunyunyizia sumu ya kukausha magugu kwenye mahindi kwa lengo la kuyaharibu,yalikuwa yamefikia hatua ya kuchanua. Mbali na mahindi walinyunyizia pia maharage, mtama na pamba, wakidai tumelima eneo ambalo haliruhusiwi.

 

“Hiyo ni dawa hatari ambayo hutumika kuua magugu na majani. Wakati wakiendelea na zoezi hilo, wakanilazimisha niwaonyesha makazi ya watu wanaoishi na kulima kwenye maeneo hayo. Bila kujali hali ya ujauzito niliyonayo walitembea nami kwenye maeneo mbalimbali na kila walipokuta nyumba waliichoma moto,” alisimulia Esta.

 

Alisema hawakuishia hapo, walikwenda hadi kwenye kisima kinachotumiwa na wanakijiji hao na kumwagia sumu hiyo ya kuuwa magugu, kitendo kilichosababisha mjamzito huyo ashtuke na kuwahoji sababu za kufanya hivyo. “Hawakunijibu cha maana. Lakini ghafla mvua ilianza kunyesha, wakasitisha zoezi hilo na kuondoka zao, kesho yake wakarejea saa 5 asubuhi, wakakuta wananchi tumekusanyika tukijadili tukio hilo,” anasema.

 

SIKU YA TUKIO

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Jalala Deus alisema siku ya tukio, wananchi walijikusanya kwenye maeneo ya mashamba yao baada ya kupata habari kuwa yameharibiwa kwa kuwekewa sumu. “Tukiwa tunajadiliana, ghafla askari wa wanyamapori walifika wakiwa na magari mawili aina ya Toyota Land Cruiser huku wakiwa na silaha.

 

Walipotuamuru tuondoke eneo hilo, tuligoma, tukawaambia sisi tupo kihalali maana tulipewa maeneo hayo na Serikali ya Kijiji tangu mwaka 2013,” alisema Jalala na kuongeza: “Baada ya mabishano ya muda mrefu na askari hao walituambia wanahesabu hadi tatu, tuwe tuomeondoka. Sisi hatukuondoka, wakafyatua risasi nne hewani, wananchi wote tukatimua mbio kwa hofu.

 

“Wakati tunakimbia ndipo wakampiga risasi Yabona sehemu ya mgongoni, risasi ikatokea sehemu ya mbele, kifuani. Watu wengine watatu wakajeruhiwa sehemu za miguuni.” Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Kilonja Palapala aliyepingwa risasi mguu wa kushoto, Majingwa Chiganza, aliyejeruhiwa paja la kushoto na Ngonyeko Makolo, mguu wa kushoto.

WAFAFANUA UHALALI WAO

Akizungumzia uhalali wa kuishi katika eneo hilo, Malandana Deus alisema yeye alifika eneo hilo mwaka 2013 na alipewa eneo hilo kwa ajili ya makazi kihalali kwa kulipia Serikali ya Kijiji cha Kapalamsenga, Tsh. 60,000 na kupewa risiti yenye namba 105020 iliyotolewa Agosti 3, 2013.

“Tumeharibiwa mazao yetu ambayo tulikuwa tunayategemea, imetuuma, maana tupo kihalali lakini tunaishi kwenye nchi yetu kama wakimbizi,” alisema Malandana.

 

DIWANI ACHARUKA

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kapalamsenga, Izack Lusambo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, akisema alitaarifiwa tukio hilo la wananchi kupigwa risasi na mazao yao kuharibiwa kwa kunyunyuziwa sumu akiwa katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda.

“Nimekasirishwa na nimesikitishwa na tukio hilo, naomba hatua kali za kisheria zichukuliwe kwani eneo hilo wananchi walipewa na baadaye wakaambiwa waondoke kwani ni mapito ya wanyama wanaotoka Hifadhi ya Wanyama ya Katavi kwenda Hifadhi ya Wanyama ya Gombe iliyopo mkoani Kigoma, lakini hawakufidiwa,” alisema Lusambo.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, ACP Damas Nyanda amekiri kutokea kwa tukio hilo, akasema ameshamwagiza OCD kwenda eneo la tukio ili kufuatilia chanzo cha tuko hilo.

“Askari waliofanya tukio hilo ni wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi, baada ya kukuta wananchi hao wakiwa wamekusanyika huku wakiwa na silaha za jadi, ndipo walipoanza kuwashambulia askari hao. Nao katika kujihami walifyatua risasi, ndipo mtu mmoja alipigwa risasi na kufariki dunia hapohapo na wengine watatu kujeruhiwa,” alisema ACP Nyanda.

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Loading...

Toa comment