Ligi Yaanza na Rekodi

SAFARI ya kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/20 ilianza rasmi Agosti 24,mwaka huu katika viwanja tofauti. Na utamu zaidi katika safari umenogeshwa baada ya kupata mdhamini aliyewekeza bilioni 9 kwa miaka mitatu na kwa sasa ligi hiyo ina timu 20 tu.

 

Lakini kwenye safari hiyo ya kusaka ubingwa katika raundi ya kwanza tu kuna rekodi na matukio ambayo yametokea kwenye mechi kumi za raundi ya kwanza. Makala hii inafafanua matukio na rekodi ambazo zimesajili katika raundi ya kwanza ya ligi msimu huu.

1. YANGA KUFUNGWA NA RUVU

Katika rekodi za Yanga msimu wa 2019/20 kwa mara ya kwanza walipoteza mbele ya Ruvu Shooting baada ya kufungwa bao 1-0.

Yanga na Ruvu kwenye ligi wamekutana mara 19 na Yanga ilishinda mara 15 na kutoa sare mara tatu lakini safari hii walipata doa hilo timu ikiwa chini ya kocha wao, Mwinyi Zahera.

 

2.KAGERE AENDELEZA REKODI

Msimu uliopita ukiwa ni msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu Bara mechi ya kwanza dhidi ya Prisons alifunga bao la kwanza na lilikuwa bao pekee.

Lakini msimu huu ameendeleza rekodi yake kwa kufunga bao lake la kwanza msimu kwenye mechi ya kwanza na safari hii akifunga mabao mawili dhidi ya JKT Tanzania kwenye ushindi 3-1. Msimu uliopita alifunga bao la kwanza la msimu akiwa na Simba.

3.POLISI, NAMUNGO WAANZA KWA KASI

Polisi Tanzania na Namungo FC walicheza kwa mara ya kwanza kwenye Ligi Kuu Bara na kuweka rekodi kwa kupata matokeo kwenye michezo ya kwanza. Rekodi nyingine ni kitendo cha timu hizo kila mmoja kucheza kwenye uwanja wake wa nyumbani na kuondoka na ushindi.

4.NADO AANZA NA REKODI AZAM FC

Huu ni msimu wake wa kwanza ndani ya Azam FC akitokea klabu ya Mbeya City. Idd Seleman ‘Nado’ alifanikiwa kuifungia Azam FC dhidi ya KMC ambao walishinda bao 1-0 lakini msimu uliopita Azam walipokutana na KMC kwenye Uwanja wa Uhuru walitoa sare ya 2-2.

5.BAO LA MAPEMA NA USIKU

Kwenye raundi hii ya kwanza Meddie Kagere wa Simba ndiye mchezaji ambaye alifunga bao la mapema zaidi dakika ya kwanza pale timu yake ilipocheza dhidi ya JKT Tanzania na kuibuka na ushindi wa 3-0.

Bao ambalo lilifungwa dakika za mwisho zaidi ni lile la kiungo Awesu Awesu wa Kagera Sugar pale ilipoivaa Biashara United pale kwenye Uwanja wa Karume, Mara akifunga dk 90.

 

6. KOCHA ALLIANCE MECHI MOJA ATIMULIWA

Alliance wao walikuwa wanaota ushindi tu kwenye mchezo wao kwanza ambao walicheza dhidi ya Mbao walipotoa sare tu ikawa ni shida. Lakini Mbao ikiwa nyumbani iliifunga bao 1-0, hii ilikuwa msimu uliopita.

Katika raundi ya kwanza msimu uliopita timu hizo zilikutana katika mchezo wa raundi ya kwanza kwenye Uwanja wa Kirumba. Msimu huu timu hizo zimekutana tena kwenye raundi ya kwanza na kutoka sare ya bao 1-1 matokeo ambayo yamemng’oa kocha Athuman Bilali ‘Bilo’ aliyekuwa Alliance baada ya kuonekana hafai.

 

7.MABAO 19

Kwenye raundi ya kwanza jumla ya mabao 19 yamefungwa kwenye mechi kumi za kwanza huku Simba na Lipuli zikiongoza kwa mabao, kila moja imefunga matatu. Msimu uliopita raundi ya kwanza yalifungwa mabao 15 na matokeo ya ushindi mkubwa yalitoka kwa Yanga vs Mtibwa (2-1) Azam vs Mbeya (2-0) na Kagera vs Mwadui (2-1).

 

8. REKODI MCHEZAJI WA KIGENI

Pamoja na ushindi kwa baadhi ya timu na nyingine kupoteza kwenye raundi ya kwanza mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere pekee ndiye mchezaji wa kigeni ambaye alifunga mabao tena mawili hakuna mchezaji wa kigeni mwingine aliyefunga. Msimu uliopita mechi za kwanza alifunga Kagere na Heriter Makambo wa Yanga.


Loading...

Toa comment