The House of Favourite Newspapers

Mrithi wa Lissu Kuapishwa Kesho Bungeni

MKUTANO wa 16 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utaanza kesho Jumanne Septemba 3, 2019, jijini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine itashuhudia Miraji Mtaturu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiapishwa kuwa mbunge wa Singida Mashariki.

 

Mtaturu anaapishwa kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Tundu Lissu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye Juni 28, 2019, Spika wa Bunge hilo, Job Ndugai alilitangazia Bunge kwamba amepoteza sifa za kuwa mwakilishi wa Singida Mashariki.

 

Ndugai alitoa sababu mbili zilizomfanya Lissu kupoteza ubunge, ambazo ni kutojaza fomu za mali na madeni za viongozi wa umma  na kutotoa taarifa kwake (spika) ya wapi alipo.

 

Wakati Ndugai akitoa taarifa hiyo, Lissu alikuwa nchini Ubelgiji akiendelea na matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 mchana wa Septemba 7, 2019, akitoka bungeni.

 

Ratiba iliyotolewa na Bunge la Tanzania mbali na kuelezea shughuli zitakazofanywa na mkutano huo wa 16 ni pamoja na kiapo cha uaminifu kwa Mtaturu ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

 

Katika harakati za kumrithi Lissu, Mtaturu alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa ubunge Julai 2019,  baada ya washindani wake kutorejesha fomu za kuomba kuteuliwa.

Comments are closed.