The House of Favourite Newspapers

ACT Wazalendo Wataja Uelekeo Wa Chama Chao Kwa Mwaka 2018

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano ya Umma ya chama hicho, Ado Shaibu.

Chama cha ACT-Wazalendo kimetangaza mikakati minne ya kipaumbele itakayoitumia kufanya siasa mwaka huu, ikiwemo kuimarisha ushirikiano na vyama vya wafanyakazi.

 

Akizungumza leo Jumapili, Januari 7, 2018, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano ya Umma ya chama hicho, Ado Shaibu amesema wanatambua kwamba wafanyakazi wanakabiliana na changamoto mbalimbali.

 

Amesema chama hicho kitawasemea wafanyakazi wanaolipwa mishahara duni, mazingira duni ya kufanyia kazi na uonevu unaofanywa na waajiri.

Shaibu amesema jambo jingine litakalofanywa mwaka huu ni kuimarisha ushirikiano na vyama vya siasa hasa katika kudai demokrasia na Katiba Mpya.

 

“Tutaongeza ushirikiano na vyama vingine vya upinzani katika kudai Katiba Mpya, tunahitaji kushirikiano ili kufanikisha hili,” amesema.

 

Amesema mwaka huu chama hicho kitafanya uchaguzi wa ndani ya chama kuanzia ngazi ya shina hadi taifa.

“Demokrasia inatakiwa ianzie ndani ya chama, tunawaomba wanachama wetu wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali za uongozi,” amesema.

 

Shaibu amesema chama hicho kitaongeza juhudi katika kupambana na haki za kijamii hasa katika kuwapigania wastaafu na bima ya afya kwa watu walio nje ya mfumo rasmi wa ajira.

 

“Mwaka 2018 utakuwa wa kuimarisha ushirikiano wetu na wanyonge katika kupigania haki za kijamii na kurejesha misingi ya utu na heshima,”amesema.

Comments are closed.