The House of Favourite Newspapers

Lugola, Ndugai Wasema CAG Muongo, Amemdanganya Rais – Video


SAKATA  la Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) liliibuka tena jana bungeni, ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola na Spika wa Bunge, Job Ndugai walisema ripoti hiyo  imesheheni uongo. 

 

Lugola alimkosoa CAG ambapo alisema  hajawahi kumuona mtu muongo nchini Tanzania kama CAG, kwani  amewasilisha kwa rais ripoti yenye uongo kuwa jeshi la polisi limelipa fedha kununua sare ambazo ni hewa.

 

Katika ripoti yake, Prof. Mussa Assad (CAG) alisema kuwa Jeshi la Polisi lililipa Sh. bilioni 16 kwa ajili ya ununuzi wa sare za polisi bila kuwapo kwa ushahidi wa ununuzi. Lakini waziri  huyo mwenye dhamana, Lugola,  jana alikanusha madai hayo na kusema kuwa hakuna sare hewa, na kwamba yupo tayari kuandamana na CAG, au maofisa wake kwenda kwenye maghala ya polisi ili akaone sare hizo.

 

“Sijawahi kuona mtu muongo kama CAG kwenye nchi ya Tanzania. Haiwezekani sare zinazodaiwa kuwa hewa, mimi nimekwenda kwenye makontena na magodown ya Polisi nimekuta sare nyingi ambazo zimeletwa, halafu CAG anapelekea taarifa kwa mheshimiwa rais, ya uongo, kwamba hakuna sare za jeshi la polisi,” alisema Lugola.

 

Aliendelea kusema kwamba yupo tayari kuweka uwaziri wake rehani, ikiwa itabainika kuwa taarifa zake za ukaguzi kuhusu sare hewa za jeshi la polisi zilizogharimu Sh16 bilioni ni ya kweli. Alisema kama anasema uongo, atajivua nguo aambatane na maofisa wa CAG kwenye stoo kuu wakaangalie makontena zaidi ya 15 yenye futi 40 na maghala matano ambayo yamesheheni sare za jeshi hilo.

 

Licha ya kuwa CAG alieleza udhaifu mwingine katika ripoti yake kuhusu Jeshi la Polisi, waziri huyo hakuzungumzia masuala mengine, ikiwa ni pamoja na vifaa vya utambuzi wa alama za vidole vyenye thamani ya Sh1.73 bilioni havikufungwa kwenye magereza 35 kama ilivyoainishwa,  badala yake vilihifadhiwa katika ofisi ya upelelezi makao makuu ya jeshi lo polisi.

 

Mambo mengine yaliyoibuliwa na CAG ni malipo ya Sh604.39 milioni kwa ajili ya mafunzo kwa wataalamu 30 ambayo hayakufanyika. GAC alisema jeshi la Polisi lilishindwa kuionyesha timu yake ya ukaguzi zilipo monita 58 za kompyuta aina ya Dell zenye thamani ya Sh159.16 milioni zilizopelekwa kwenye kitengo cha cha uchunguzi wa kisayansi cha makao makuu ya polisi (Forensic).

 

Pia, alisema monita 213 za kompyuta aina Dell zilizolipiwa Sh195.22 milioni kwa mzabuni Lugumi Enterprises Limited hakuzikabidhiwa.

Naye Spika wa Bunge, Job Ndugai,  alisema wapo watu wanaowaaminisha Watanzania kuwa kila kinachoandikwa kwenye ripoti ya CAG, ni ukweli asilimia mia, jambo ambalo si sahihi.

 

Spika Ndugai alikuwa anamkosoa Mbunge Zitto Kabwe ambaye alisema kuwa amekuwa mwepesi wa kuupotosha  umma kwa kutumia ripoti zinazotolewa na ofisi ya CAG. Kiongozi huyo wa Bunge alisema kwamba kinachotolewa na CAG ni hoja, ndiyo sababu kamati zenye dhamana, Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Bunge Hesabu za serikali za Mitaa (LAAC) hukaa na kuichambua ripoti hiyo.

 

“Watu wanawaaminisha Watanzania kuwa kila kilichoandikwa na CAG au ofisi yake ni ukweli asilimia 100. Sio hivyo, yapo mambo mle si kweli hata kidogo. Zile ni hoja, ndiyo maana kamati za PAC na LAAC zinachambua kila kitu,” alisema Ndugai.

Comments are closed.