The House of Favourite Newspapers

Mimi, Wewe na Serengeti Boys Tutakuwa ‘Wapenzi Watazamaji’ Fainali ya AfconU17

WACHEZAJI wote wa Serengeti Boys pamoja na mimi na wewe tutakuwa ‘Wapenzi watazamaji’ Jumapili kwenye fainali ya Afcon ya U-17 kwenye Uwanja wa Taifa. Hata ukinuna, ufurahi ndiyo ukweli. Maisha lazima yaendelee na tukubali tulichemsha kama Taifa.

 

Tanzania ambayo iliwakilishwa na Serengeti walitolewa kwenye hatua za awali kabisa baada ya kupigwa mechi zote tatu za hatua ya makundi. Siyo kipigo tu, Serengeti walikosa ubingwa kwenye ardhi ya nyumbani wakiwa kama waandaaji na vilevile kukosa tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia kwa Vijana nchini Brazili.

 

Ilihitaji kushinda mechi mbili tu ili kufuzu Kombe la Dunia lakini maji yakazidi unga. Katika mechi za jana za nusu fainali, Nigeria ilipoteza kwa penati 9-10 dhidi ya Guinea huku Cameroon ikiishinda Angola penalti 4-3. Hivyo fainali ni Guinea na Cameroon Jumapili.

 

Timu hizo zote zilimaliza dakika 90 pamoja na mbeleko za marefa bila kufungana na ndipo majanga yalipomkuta wakumkuta kwenye penalti ambazo Serengeti Boys waliziangalizia kwenye vibandaumiza uswahilini. Mshindi wa tatu atapatikana Jumamosi jioni baina ya Angola na Nigeria. Mechi zote zitapigwa majira ya saa 10 jioni.

Comments are closed.