The House of Favourite Newspapers

Maajabu Ndani ya Basi la Dar-Arusha-5

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

“Meseji nilituma mimi au ulitumiwa na nani? Sijakuelewa mume wangu, maajabu gani kwani umekutana nayo au nikupigie uniambie vizuri?” aliniuliza mke wangu.

ENDELEA NAYO MWENYEWE SASA…

Nilishtuka tena, nikawaza moyoni kwamba, ina maana meseji ya kwanza sikuchati na mke wangu? Niliifuata ile meseji kwenye simu, sikuiona. Nikahisi kama naota. Namba ya mke wangu ilionekana kutuma meseji hiyo moja tu ya kuniuliza ni maajabu gani niliyoyapata.

“Usipige, nitakusimulia baadaye lakini unatakiwa kuniombea sana kwani hali si nzuri humu kwenye basi,” nilimjibu mke wangu.

Naye akanijibu: “Kama kuna mazingira ya hatari kwa nini usishuke ukapanda usafiri mwingine?”

“Nitafika na usafiri huuhuu, Mungu wangu atanisaidia.”

Safari iliendelea, sasa ilifika mahali nikahisi baridi mwilini. Lakini nilimwomba Mungu aninusuru na ubaya wowote ule.

Tulifika mji mmoja unaitwa Mombo ambao ni sehemu ya Wilaya ya Korogwe. Pale tulitangaziwa kwambba ndipo tutakapokula chakula na baada ya dakika kumi na tano tutaanza safari.

Mimi ndiye niliyekuwa wa pili kushuka. Sikutamani kukaa ndani kabisa. Na niliposhuka sikwenda kuagiza chakula ndani ya hoteli, niliagiza nje nyama choma.

Nilichukua mfuko wenye nyama na kwenda kusimama katika mti na kuanza kula huku macho yangu yakikazia kwenye basi ambapo abiria wenzangu wote walishashuka.

Mmoja wa abiria alikuja mpaka niliposimama mimi na kuniambia maneno ambayo yaliusumbua moyo wangu.

“Kaka. Kama nimekuona kwenye basi unahangaika sana. Una matatizo gani kwani?”

Nilimjibu sina matatizo ila ndani ya gari ndimo mna matatizo makubwa.

“Kama yapi?” aliniuliza.

Nilimuuliza kama yeye anaona hali ya kawaida. Akasema hali ni ya kawaida sana bali mimi naonekana kama si abiria mwema. Nikamjibu:

“Mimi ni abiria mwema sana ila labda wewe unaniangalia kwa jicho lingine. Yule mzee niliyekaa naye si mtu wa kawaida. Dar stendi ya Ubungo nilikaa naye, kufika Mbezi akaonekana ni msichana, mbele tena akatokea yule mzee, we unaona ni kawaida?”

“Unaona sasa! Ndiyo maana nikakwambia wewe si mtu wa kawaida. Pale kwenye siti yako umekaa na msichana tangu Ubungo, Dar es Salaam. Huyo mzee unayemsema wewe ni yupi?”

Nilimshangaa sana yule abiria. Nikahisi ndiye yule mzee kwani ina maana hakumwona mzee kwenye siti niliyokaa mimi?

“Bahati nzuri watu wanapanda kwenye basi, twende sasa hivi kama hutamwona mzee,” nilimwambia.

Ni kweli watu walikuwa wakiingia ndani ya basi. Tukaenda na yule abiria huku nikimkazia macho ili asije akanipotea katika mazingira yenye utata.

Tulipoingia  nikashangaa kumwona Rehema kwenye siti yangu. Tulipokutana macho aliachia tabasamu pana huku akiwa anasema maneno mwenyewe bila kutoa sauti.

Niliyasoma yale maneno kupitia namna alivyokuwa akipanua kinywa na kufumba. Alionekana kusema; ‘Mungu wangu… Mungu wangu.’

Nilipofika, nilijipenyeza na kukaa kwenye siti yangu upande wa dirishani. Kisha nikamgeukia na kumwambia mambo? Akatabasamu tena na kunijibu poa tu, vipi wewe?

Nilimwambia mimi siko poa kwani nashindwa kumwelewa. Akaniuliza kivipi? Nikamwambia haiwezekani aonekane ni mzee mara msichana.

“Mimi anko?” aliniuliza kwa mshangao mkubwa huku akijishika kwenye kifua chake.

“Wewe ndiyo?”

Niliposema wewe ndiyo nilisimama kidogo na kumwangalia yule abiria ambaye alinifuata kule nje. Yeye alikaa siti ya pembeni yangu kushoto baada ya korido, akaachia tabasamu tu bila kusema neno.

Nilirudi kukaa, nikamwangalia Rehema na kumwambia:

“Mungu wangu atanisadia, nitamaliza safari salama.”

“Atakusaidia, atatusaidia?! Sisi abiria wote tunaamini Mungu atatusaidia.”

“Si kwa maana hiyo mimi nazungumzia maruweruwe unayonifanyia,” nilimwambia, akaonekana kushangaa kwa kupanua kinywa, akasema:

“Ina maana mimi nakufanyia wewe maruweruwe?”

“Ndiyo,” nilimjibu pasipo na shaka.

Akasema: “My God! Hivi kweli mimi msichana naweza kukufanyia maruweruwe wewe mwanaume mwenye nguvu zako na akili timamu? Kwa hiyo una maana mimi ni jini siyo?”

Nilinyamaza kimya bila kumjibu, nikalala usingizi wa moja kwa moja, nilipokuja kushtuka tulikuwa tunaingia Moshi mjini.

Nikamwangalia Rehema, hakuwepo, alikuwa yule mzee. Tulipokutana macho akaachia tabasamu la kizee. Palepale nilimsukuma mpaka akaangukia kwenye korido ya basi huku nikimwambia kwa sauti ya ukali:

“Mimi siyo mtu wa kunifanyia hivi we mzee. Shika adabu yako la sivyo nitakuua mbele ya abiria wengine.”

Je, nini kiliendelea? Usikose kusoma wiki ijayo mkasa huu unaoitwa Maajabu Ndani ya Basi la Dar-Arusha.

Leave A Reply