The House of Favourite Newspapers

Maajabu Ndani ya Basi la Dar-Arusha-6

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Nilinyamaza kimya bila kumjibu, nikalala usingizi wa moja kwa moja, nilipokuja kushtuka tulikuwa tunaingia Moshi mjini.

Nikamwangalia Rehema, hakuwepo, alikuwa yule mzee. Nilimsukuma mpaka akaangukia kwenye korido ya basi huku nikimwambia kwa sauti ya ukali:

“Mimi siyo mtu wa kunifanyia hivi we mzee. Shika adabu yako la sivyo nitakuua mbele ya abiria wengine.”

SASA ENDELEA…

Abiria wengine walikuja kunitoa ili nisimng’ang’nie yule mzee lakini na mimi sikukubali, nilimkaba kabali ya nguvu huku nikimwambia uhai wake mwisho siku hiyo.

“Kwani tatizo ni nini?” aliniuliza abiria mmoja.

“Huyu mzee tangu Dar ananichezea. Mara mwanamke, mara mwanaume. Mara msichana, mara nini sijui!” nilisema.

Abiria wakaniangalia, wakapanua vinywa kuashiria mshangao mkubwa, wakauliza kwa pamoja:

“Mzee yupi sasa?”

“Si huyu.”

Wakati nasema si huyu nikamwangalia yule mzee, khaa! Kumbe ni Rehema. Nikasema:

“Si mnaona, sasa amekuwa mwanamke.”

“Mimi tangu lini nilikuwa mwanaume wewe kaka. Tangu Dar mimi na wewe tunazungumza uliniona ni mzee? Mbona tumeongea mambo mengi sana na sijakufanyia baya lolote,” alisema Rehema.

Nilimwachia, nikakaa kwenye siti sehemu yangu. Lakini nikamwangalia yule abiria aliyenifuata pale hotelini Mombo, alikuwa akiniangalia kwa macho yaliyojaa tabasamu pana.

Nilitaka kumwambia jambo lakini nikasita, nikaangalia mbele. Ghafla alikuja kondakta wa basi lile mpaka pale nilipokaa mimi na Rehema, akauliza:

“Eti tatizo ni nini?”

Mimi nilimsimulia kila kitu kuhusu Rehema, kondakta akasema:

“Mimi nadhani anko ujiangalie vizuri ulikotoka. Huyu dada alipandia Mbezi. Mpaka tunafika Chalinze mimi namwona, tunafika Korogwe mimi namwona, tunafika Mombo mimi namwona. Sasa kugeuka kuwa mwanaume mzee kumeanzia wapi?”

Abiria wengine waliangua kicheko cha kunikejeli. Nikajisikia vibaya sana. kondakta akaendelea:

“Sasa wewe twende ukakae kule, nitamtoa mtu mmoja aje akae hapa.”

Nilisimama haraka sana, nikachomoa beki langu la mgongoni lililokuwa kwenye keria ya juu na kuhama siti. Rehema alinipisha wakati napita lakini kabla sijaendelea kwenda niligeuka kumwangalia kwa hasira.

Nilifikicha macho ili nione sawasawa kwani nilimwona ni yule mzee akiachia tabasamu lakini hapohapo nikamwona ni Rehema akisema:

“Nakutakia kila la heri.”

Nilifikicha macho tena, nikahisi kama naota vile. Alikuwa ni Rehema lakini kabisa aligeuka muda f’lani kuwa yule mzee na kuniachia tabasamu.

Nilikwenda kukaa. Abiria niliyekaa naye akaniuliza:

“Kwani kule kuna nini anko?”

Nilimsimulia mwanzo mwisho, akaniambia:

“He! Unajua haya mabasi yaone hivihivi. Yana vituko sana, hasa kama mtu ni mwepesi ndiyo kabisa.”

“Mwepesi kwa maana gani?”

“Unajua kuna watu wana kinga mwilini, wengine hawana. Sasa ukiwa na kinga mara nyingi unasalimika kwenye matukio ya ajabu kama haya.”

“Ni kweli labda.”

Safari iliendelea. Nilitamani sana kumwona Rehema pale alipokaa. Lakini pia nilijua kwamba, yule abiria mwenzangu atakutana na makubwa zaidi. Na niliamini tusingefika mbali, angepiga kelele kwa maajabu.

Nilipitiwa na usingizi wa fofofo. Sikuweza kuamka mpaka nilipokuja kushtuka basi likiwa limesimama. Ndani ya basi hakukuwa na mtu mwingine zaidi ya dereva tu. Aliponiona nimeamka akasema:

“Usingizi gani ndugu yangu? Umeamshwa sana lakini wapi!”

“Hapa wapi kwani?” nilimuuliza dereva.

“We ulikuwa unakwenda wapi?”

“Arusha.”

“Unapafahamu?”

“Ndiyo.”

“Sasa mbona unauliza?”

Nilichungulia nje, kweli tulikuwa Arusha lakini siyo stendi. Dereva akasema basi lilishusha abiria stendi na kuondoka. Pale tulikuwa eneo linaloitwa Mbauda. Lakini hakusema alifuata nini hapo Mbauda.

Nilisimama, nikavuta begi langu dogo na kushuka huku macho ya yule dereva akiyakaza kwangu moja kwa moja ninavyoshuka.

Kufika chini, nikaangalia pande zote za dunia kisha nikaliangalia basi. Nilishangaa sikuona maandishi ya ubavuni yanayosema jina la basi.

Nikaanza kuondoka kwa kasi huku mapigo ya moyo yakinienda mbio. Niliogopa. Ilibidi nitafute teksi ili inipeleke mjini, ghafla lile basi likanipita, abiria walitoa vichwa na kuniangalia, akiwemo yule mzee.

Je, nini kiliendelea? Usikose kusoma wiki ijayo mkasa huu unaoitwa Maajabu Ndani ya Basi la Dar-Arusha.

 

Leave A Reply