The House of Favourite Newspapers

Maalim Seif: Hii Ndiyo Siri Yangu na Karume -3

0

 

WIKI hii tunamalizia mahojiano yetu na Katibu Mkuu wa  Chama Cha wananchi  CUF ambaye pia aliwahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Kitaifa ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamadi.

Anaendelea kueleza kuhusu msuguano uliokuwepo kati ya wana CCM enzi hizo akiwa katika chama hicho kwa upande wa Zanzibar kati ya Liberators na Frontliners; endelea:

Liberators hao walishaweka shinikizo kwa mzee Aboud Jumbe kuwa vijana aliowaingiza watakuja

mgeukia na kuwaondoa wao, Liberators, na yeye mwenyewe katika uongozi. Inaelekea mzee Aboud Jumbe alishawishika na shinikizo hilo, na hivyo naye, kwa njia zake, alitaka kuona kuwa Frontliners hawaingii katika NEC na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi ambako pengine wangekuwa na ushawishi katika maamuzi ya sera za chama.

Frontliners walipoingia, ikawalazimu Liberators na mzee Aboud Jumbe kutafuta njia nyingine ya kuweza kuwazingira ili, ikiwezekana, waweze kuondolewa katika ramani ya uongozi wa chama na serikali.

 

Maalim Seif Sharif Hamadi akizungumza na Mhariri wa Uwazi, Elvan Stambuli.

 

Hivyo basi, mara baada ya kikao cha Mkutano Mkuu wa Taifa kumalizika Novemba, 1982, mzee Aboud Jumbe aliwataka wajumbe wote wa NEC kutoka Unguja akutane nao Unguja, na wajumbe wote wa NEC kutoka Pemba akutane nao Pemba. Katika mikutano hiyo, hotuba ya mwalimu wangu, mzee Aboud Jumbe, ilitushtua wengi.

 

Swali: Kwa nini iliwashitua?

Alisema nini?

 

Jibu: Mzee Aboud Jumbe alishtumu kuwa kuna watu wanaoleta uchochezi kutaka kuvigawa visiwa vya Unguja na Pemba; kutaka kuigawa mikoa, yaani mkoa mmoja dhidi ya mwingine katika kila kisiwa; kutaka kuzigawa wilaya, yaani wilaya moja dhidi ya nyingine katika kila mkoa; na kutaka kuvigawa vijiji, yaani kijiji kimoja dhidi ya kingine katika kila wilaya. Akamalizia kwa kusema kuwa watu hao watahukumiwa na kuonja kile alichokiita “Revolutionary Justice”. Hili lilitushtua wengi, hasa sisi vijana wa wakati huo.

 

Tukakumbuka historia ya Zanzibar tangu Mapinduzi ambapo watu walioshukiwa kuwa wapinzani wa serikali, na hasa wasomi, walivyoshughulikiwa kwa kuhakikisha kuwa wanatoweka kabisa. Hofu yetu ikawa je, hawa wazee si wamekusudia kuturudisha huko huko tulikotoka?

 

Tukasema kama hatukuchukua  hatua za kichama kulizuia hili,  basi kuna uwezekano wa historia  kujirudia na watu wasiokuwa  na hatia kupotea kwa kile  kinachodaiwa kusimamisha  “Revolutionary Justice”

 

Swali: Je, mliishia kushituka tu?

Jibu: Hapana, baadhi yetu  tuliokuwa Wajumbe wa Sekretarieti  ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya  Chama, hasa sisi kutoka Zanzibar,  tukamfuata mzee Rashid Kawawa  aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM  na Mwenyekiti wa Sekretarieti na  kumueleza hofu yetu hiyo.

 

Swali: Mzee Kawawa  aliwaelewa? Alifanya nini?

 

Jibu: Mzee Kawawa alituelewa na akaamua iletwe agenda juu ya suala hilo katika kikao kilichofuata katika sekretarieti. Agenda ikaletwa. Ikajadiliwa kwa mapana yake, kisha ikawasilishwa katika kikao cha Kamati Kuu.

 

Kamati Kuu ikaamua kuunda timu mbili kwenda kuchunguza madai yaliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mzee Aboud Jumbe.

 

Timu moja ikaagizwa kufanya uchunguzi katika Kisiwa cha Unguja, na timu ya pili Kisiwa cha Pemba. Timu moja iliongozwa na marehemu Moses Nnauye na ya pili iliongozwa na Alfred Tandau.

 

Swali: Baada ya kuundwa timu hizo za uchunguzi, nini kilitokea?

 

Jibu: Baada ya uchunguzi,  timu zote mbili zikawasilisha taarifa zao katika kikao cha Kamati Kuu. Timu zote mbili ziliona kuwa madai ya Mzee Aboud Jumbe hayakuwa na msingi. Hivyo Kamati Kuu ikamsihi Makamu wa Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mzee Jumbe, kuzuia kuchukua hatua zozote zile ambazo zingeweza kusababisha ukiukwaji na uvunjaji wa haki za binadamu dhidi ya raia. Inavyoonekana, hili halikumpendeza mwalimu wangu, mzee Jumbe.

 

Alihisi kuwa chama na Muungano unamuingilia katika kutekeleza azma yake na ile ya Liberators ya kuisafi sha safu ya uongozi wa chama Zanzibar kwa kuwaondoa kwa njia yoyote ile Frontliners na vijana wenye mawazo mapya. Kipindi hicho kulikuwa na mjadala ulioanzishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM juu ya mapendekezo ya marekebisho ya Katiba.

 

Mzee Aboud Jumbe na timu yake wakaona kuwa waitumie nafasi hiyo kufanya kampeni kabambe kutaka muundo waMuungano ubadilishwe. Sisi wa Frontliners tulitafsiri kuwa kampeni hiyo madhumuni yake ni kutaka kubadili muundo wa Muungano ili kundi la Liberators lipate uhuru zaidi, nguvu zaidi, na madaraka zaidi ambayo kwa mawazo yetu, yangetumika dhidi ya watu wenye mawazo mapya na ambao walionekana kama ni tishio kwa Liberators.

 

Tulitafsiri kampeni hiyo kuwa na agenda iliyojifi cha ya kutaka kujiimarisha na kujichimbia katika madaraka kundi la Liberators ili kulinda status quo (hali ilivyo).

 

Swali: Baada ya kugundua kuwa kuna ajenda iliyojifi cha mlifanya nini?

 

Jibu: Ni kwa msingi huo ndipo mimi na wenzangu wa Frontliners tulimpinga mzee Aboud Jumbe.

Ifahamike kuwa hatukupinga dhana ya serikali tatu!

 

Tulipinga nia iliyojifi cha ya mzee Jumbe na wenzake ya kuibua agenda hiyo. Tulipinga njia zilizotumika katika kuisimamia na kuiendesha agenda hiyo. Ndiyo maana mara baada ya Chama cha Wananchi, CUF, kuundwa, tukabuni sera ya muundo wa Muungano wa serikali tatu. Ikumbukwe kuwa wengi wa waasisi wa CUF walitokana na kundi la Frontliners.

 

Ingalikuwa kulikuwa na nia njema, mzee Aboud Jumbe angetuita, walau baadhi yetu na kutaka mawazo yetu. Nina hakika wengi tungekubaliana naye na tungezungumzia mkakati wa kulikabili suala hilo.

 

Swali: Una hakika Wazanzibar mngeenda kwenye kikao mkiwa kitu kimoja kwa hoja, ingeshinda hoja yenu?

 

Jibu: Mimi nina hakika tungekwenda Kamati Kuu na baadaye Halmashauri Kuu kama uongozi wa Zanzibar ulioungana, wenzetu wa Bara wasingeweza kutupuuza. Na hapa niseme, tena kwa masikitiko makubwa, kwamba hili ndiyo limekuwa tatizo letu Wazanzibari.

 

Wazanzibari tuna madai ya msingi katika Muungano. Lakini tunashindwa kuyasimamia madai yetu hayo hadi kupatikana mafanikio kwa kuwa tumekubali kugawiwa na tumegawika. Kugawika huko hakuyanufaishi masilahi ya Zanzibari.

 

Swali: Kwa maana hiyo, nini wito wako kwa Wazanzibar?

 

Jibu: Nitoe wito, kupitia gazeti lenu, kwamba wakati umefi ka kwa Wazanzibari bila kujali tofauti zetu za kiitikadi, kuungana ili kusimamia, kutetea na kuendeleza masilahi ya Zanzibar na watu wake katika Muungano. Kwa kumalizia basi, kwa maoni yangu, Zanzibar ni nchi. Zanzibar ni taifa. Zanzibar ni dola.

 

Zanzibar ni nchi kwa sababu ni eneo lenye mipaka inayotambulikana na Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Swali:Lakini Zanzibar haina jeshi na polisi wake, je, ni kweli? Vipi kuhusu masuala ya kimataifa Zanzibar kama nchi?

 

Jibu: Ni kweli kuwa Zanzibar haina jeshi lake wala polisi wake. Lakini ni kweli pia kuwa Zanzibar ina vyombo vyake vingine vya maguvu vilivyoanzishwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Katiba inayotambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano na sheria za Zanzibar (Kama Kikosi cha Kupambana na Magendo- KMKM).

 

Mwandishi:Tunakushukuru sana kwa kukubali kwako kuzungumza na sisi na ufafanuzi wako wa mambo mengi.

Jibu: Ahsanteni na nyinyi karibuni tena.Ili kusikia na kuona sehemu ya mahojiano haya tembelea Global Tv online.

 

Leave A Reply