The House of Favourite Newspapers

Mabilionea wasio na huruma – 71

0

Viola na nduguye Vanessa wamedungwa sindano ya sumu, wakafa na kuzikwa, wakiwa wameacha wosia kwa mwanasheria wao Denis Crapton kwamba utajiri wote walioukusanya ungerithiwa na watawa wawili waliotajwa kwa majina ya Padri Silvanio Angelo na Sista Mariastela Geogio.

Hakuna mtu anayewafahamu watawa hawa zaidi ya kutajwa kwamba waliishi kwenye mji uitwao Santa Marta Kaskazini mwa Columbia, jambo hili limemfanya mwanasheria Crapton aingiwe na tamaa na kusema watawa hao hawakustahili kurithi utajiri wa dola bilioni mbili.

Uamuzi alioufikia ni kuwaondoa duniani kabla hawajapata taarifa za utajiri walioachiwa, baada ya hapo angebadilisha nyaraka na kujitaja kwamba yeye ndiye alikuwa mrithi halali wa utajiri huo! Amemtafuta rafiki yake James Kimberly, waliyesoma naye miaka mingi kabla ambaye kwa hivi sasa anaishi Bogota, Columbia akijihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Huyu ndiye amemuunganisha na mtu aitwaye Escobar, anayemiliki kundi la uhalifu, kwa malipo ya dola laki moja mtu huyo hatari ameamua kuwatumia vijana wake kwenda Santa Marta kuwaua Padri Silvanio na Sista Mariastela.

Je, watafanikiwa? SONGA NAYO…

ILIWACHUKUA muda wa saa ishirini na sita kuendesha gari kutoka Bogota hadi kuingia Santa Marta, mji mdogo wa milimani uliokaliwa na idadi ya watu wasiozidi mia nne, wengi wakiwa ni wakulima wa mmea uitwao Coca uliotumiwa kutengeneza dawa za kulevya aina ya Cocaine, ambayo ndiyo ilikuwa biashara kubwa ya watu wa Kaskazini mwa Columbia.

Vijana hawa watatu walikuwa na kazi moja tu ya kufanya kwenye mji huo wa Santa Marta; kuwaua Padri Silvanio na sista Mariastela, hawakujua ni kwa nini walitakiwa kuwaua, walichofanya wao ni kutekeleza maelekezo ya bosi wao Escobar!

Ilikuwa ni siku ya Jumapili asubuhi walipowasili wakiwa wamechoka tabaan, kwenye gari lao walibeba bunduki mbili aina ya SMG na risasi za kutosha, lakini pia walibeba galoni tano za petrol ili kama ingeshindikana kuwadungua kwa risasi kutokea mbali, walipue nyumba zao kwa petrol na kuwaua, lengo lilikuwa kuua, hawakuwa tayari hata kidogo kurejea Bogota wakiwaacha Padri Silvanio na sista Mariestala wakiwa hai, kama hilo lingetokea basi wao ndio wangekufa kwa niaba yao.

“Lazima wafe, ikiwezekana usiku wa leo ili turejee Bogota mara moja!”

“Hakuna sababu ya kuendelea kubaki huku, sidhani kama wana ulinzi wowote kwa jinsi ninavyouona mji huu ulivyokaa.”

“Hawa haitakuwa kazi kubwa kuwaua.”

“Kabisa.”

Mji wa Santa Marta ulikuwa ni miongoni mwa miji yenye ukimya kabisa duniani, watu wake wengi wakiwa ni watumiaji wa dawa za kulevya, miaka michache kabla hapakuwa na shule wala kanisa, kilichotawala kilikuwa ni uhalifu kama mauaji na ubakaji.

Kanisa Katoliki Columbia baada ya taarifa kusambaa kwenye vyombo vya habari juu ya ukatili na unyama uliokuwa ukiendelea kwenye mji huo, liliamua kutuma watawa kwenda kuhubiri Injili, Padri Silvanio na sista Mariastela walikuwa miongoni mwa watawa wa mwanzo kumi kupelekwa kwenye mji huo kufanya kazi ya Mungu.

Walipofika waliwaonea huruma wakazi wa mji huo, waliokuwa na maisha duni kupindukia, wakaanza kuwahubiri Ukristo, maana wengi hawakuwa na dini wala imani yoyote na kufanikiwa kuvutia wengi ndipo wakaanza kufungua makanisa na kuleta vyombo vya muziki wakiwafundisha kuimba na kupiga vyombo.

Watu waliwapenda na kuwafurahia hasa pale walipoanza kujenga shule na kuwaandikisha watoto wao, wao wenyewe Watawa wakiwa walimu wa mwanzo. Miaka michache baadaye tayari maendeleo na ustaarabu ulishaanza kuonekana katika Mji wa Santa Marta, tatizo kubwa lililojitokeza ilikuwa ni vifo vya watawa vilivyosababishwa na ugonjwa wa malale ulioua watu wengi katika maeneo hayo.

Wakabaki watawa wawili tu, Padri Silvanio na sista Mariastela, wenzao wote walikufa na kuzikwa kwenye kambi ya watawa hapohapo Santa Marta! Ilikuwa ni tukio la kusikitisha, lakini Padri Silvanio na sista Mariastela hawakuwahofia wala kuamua kuondoka, wakabaki na watu wa mji huo mpaka baadaye walipofungua hospitali kubwa kwa msaada wa Vatikani na kundi kubwa la madaktari na wauguzi wakaja ndipo ugonjwa wa malale ukatokomezwa.

***

Jumapili hiyo watu wengi walijaa ndani ya kanisa, wote walifahamiana kwa sababu ni watu walewale waliabudu kila Jumapili na ilipotokea mtu hakuhudhuria misa, ilijulikana kabisa kwamba mtu fulani hajafika na sista Mariastela alikuwa na wajibu wa kufuatilia kuona kulikuwa na tatizo gani, yeye ndiye alikuwa mkuu wa huduma za jamii kwenye parokia ya Santa Marta.

Padri Silvanio alikuwa mbele madhabahuni akiendesha misa ya Ekaristi Takatifu, waumini walikuwa wakitembea mmoja baada ya mwingine kwenye mstari kwenda kupokea mwili na damu ya Kristo, kula na kunywa huku wimbo wa “Damu ya Yesu msalabani” ukiimbwa kwa lugha ya Kihispaniola.

Ghafla padri alipotupa macho yake mbele mlangoni alishuhudia watu watatu waliovalia makoti marefu ya rangi nyeusi wakiingia, walikuwa wageni kabisa machoni mwake, hakuwa na hofu yoyote moyoni kwa sababu alikuwa ndani ya kanisa, mahali kwenye kila aina ya amani.

Watu hao walikuja na kuketi viti vya nyuma kabisa na ibada kuendelea, walivyoonekana kwa uchunguzi ambao Padri alifanya, hawakuwa Wakatoliki maana taratibu za ibada ziliwachanganya! Akaamua kuhamisha mawazo kwao na kuendelea na ibada hadi mwisho ndipo alipowafuata na kuwasalimia.

“Hamjambo jamani?” aliwasabahi.

“Hatujambo, habari za Jumapili?”

“Nzuri, tumsifu Yesu Kristo!”

“Ndiyo!” waliitikia vijana hao kwa pamoja, hapo ndipo Padri Silvanio akathibitisha kabisa kwamba watu waliokuwa mbele yake hawakuwa Wakatoliki kwani walitakiwa kuitikia salamu hiyo kwa kusema “Milele amina.”

Akajaribu kuongea nao akiwadadisi kama walikuwa wenyeji wa mji huo, wakamkatalia na kumweleza ukweli kwamba wao walitokea Bogota na walikuwa hapo kwa ajili ya kutalii na kuangalia namna ambavyo Kanisa Katoliki lilifanikiwa kuubadilisha Mji wa Santa Marta, Padri Silvanio alifurahi mno baada ya kusikia maneno hayo na kuwaona watu hao walikuwa ni wema kwake bila kuelewa kwamba walikuwepo kwenye mji huo kwa kazi ya kumuua yeye na sista Mariastela.

“Karibuni sana!”

“Ahsante.”

“Mmefikia wapi?”

“Ndiyo kwanza tumefika!”

“Tunaweza kuwahifadhi kwenye nyumba yetu ya wageni parokiani iwapo hamjapata mahali pa kufikia, maana kwenye mji huu hakuna nyumba ya kulala wageni, ni mji wa kizamani!”

“Tunashukuru sana, tunaomba tuupokee msaada huo kwa mikono miwili!”

“Basi washeni gari lenu mnifuate kwa nyuma, ni hapo jirani tu!”

Vijana hao wakarudi mpaka kwenye gari na kuwasha kisha kuanza kumfuata Padri kwa mwendo wa taratibu, mita kama mia moja hivi walifika kwenye jumba la watawa, kando yake ndiko kulikuwa na nyumba ya wageni, sista Mariastela alifika na kuwasalimia huku akiwakaribisha pia kwa ukarimu wa hali ya juu bila kuelewa alikuwa akikikaribisha kifo chake mwenyewe.

“Mimi naitwa sista Mariastela, nyie?” alisema sista Mariastela baada ya kuwazungusha kwenye nyumba ya wageni.

“Mimi ni John na hawa wenzangu ni Clement na Paul!”

“Karibuni kwa mara nyingine, mkiwa na shida yoyote mnaweza mkabonyeza kengele, hapa kwetu hakuna simu, nitafika mara moja kuwasaidieni!”

“Ahsante sista.”

Baada ya mazungumzo hayo Padri Silvanio na Sista Mariastela waliondoka wakiwaacha vijana hao watatu wameketi chumbani pamoja, wakaanza kujadiliana namna ambavyo kazi ilionekana kuwa rahisi kuliko walivyotarajia.

“Hapa tusitumie bunduki, petrol tu inatosha, tutawachomea ndani ya nyumba usiku!”

“Wazo zuri.”

Wakakubaliana na kusubiri usiku uingie.

JE, nini kitaendelea? Vijana hao watafanikiwa kutekeleza zoezi lao? Fuatilia wiki ijayo siku ya Jumatatu katika Gazeti la Championi.

 

 

Leave A Reply