The House of Favourite Newspapers

Mabilionea wasio na huruma 75

0

PADRI Silvanio na Sista Mariastela wametangazwa na mahakama kuwa warithi halali wa utajiri wa Dk. Viola na Vanessa ambao ni marehemu, mwanasheria Dennis Crapton ameangushwa katika kesi aliyotaka kudhulumu utajiri huo, jambo ambalo limemuumiza kupita kiasi.
Je, nini kitaendelea?

SONGA NAYO…

KUTOKA mahakamani msafara wa magari yasiyopungua kumi yaliyojaza wafanyakazi wa Kisiwa cha Bongoyo pamoja na Padri Silvanio na Sista Mariastela yalinyoosha moja kwa moja kuelekea Kivukoni, huko yalipandishwa kwenye pantoni ambalo liliyavusha mpaka upande wa pili wa kisiwani, wafanyakazi wote walikuwa na furaha kupata mabosi wapya.
“Welcome to Bongoyo Island, my name is Christine, the manager here!” (Karibuni Kisiwa cha Bongoyo, naitwa Christine, ndiye meneja hapa!)
“Good to meet you Christine, I am Father Silvanio and this is Sister Mariastela, the new owners!” (Tunafurahi kukutana na wewe Christine, naitwa Padri Silvania na huyu ni Sista Mariastela, wamiliki wapya wa kisiwa!”
“Congratulations, you are so lucky!” (Hongereni sana, mna bahati mno!)
“We thank God!” (Tunamshukuru Mungu!)
Yalikuwa ni maongezi kati ya Padri Silvania na meneja baada ya kushuka tu kwenye pantoni na kupokewa na kundi kubwa la wafanyakazi waliofika Kivukoni kuwapokea, taarifa zilishatangulia kwamba warithi halali wa utajiri wote wa Dk. Viola na Vanessa walikuwa njiani kuelekea visiwani, hapakuhitajika gari tena kutoka Kivukoni, bali walitembea kwa miguu mpaka kwenye jengo la ofisi na kuingia ndani ambako walipandisha kwa kutumia lifti mpaka ofisini ambako walipokelewa na katibu muhtasi.
Kilichowashangaza watu wote ni jinsi Padri Silvanio na Sista Mariastela walivyoutambua mlango wa kuingia ofisini namna ulivyofunguliwa, walifanya kila kitu kama vile waliwahi kuwa pale kabla. Kitasa cha mlango kilikuwa na shida na ilikuwa ni lazima mtu aliyefungua mlango atumie nguvu nyingi sana, vinginevyo asingeweza kuufungua, kwa Padri Silvanio pamoja na umri wake mkubwa haikuwa kazi ngumu ila aliacha maswali mengi miongoni mwa watu waliomsindikiza.
Kutoka ofisini waliingia chumba cha mikutano ambako wafanyakazi wa ngazi za juu wote walikusanyika na Padri Silvanio na Sista Mariastela waliwahutubia na kuwahakikishia kwamba wangefanya kazi kwa ushirikiano bila kuweka tofauti yoyote kati ya mwajiri na mwajiriwa, ili kuiwezesha kampuni kusonga mbele kama ambavyo wamiliki wa mwanzo walikuwa wamejiwekea malengo.
“Sisi ni wageni hapa, tutawategemeeni sana ninyi kufanya mambo yote, hivyo tunahitaji sana kupata ushirikiano wenu!”
“Hakuna tatizo bosi, tutashirikiana, hivyo ndivyo tulivyoishi na marehemu Dk. Viola na nduguye Vanessa, walikuwa watu wazuri sana, mnaelekea kufanana tabia na mienendo.”
“Basi itakuwa vizuri.”
Jioni ya siku hiyo ilifanyika sherehe kubwa ya kuwakaribisha wamiliki wapya, watu wote walihudhuria, chakula kizuri na vinywaji vilikuwepo na baadaye muziki uliporomoshwa. Kilichowashangaza wafanyakazi ni jinsi ambavyo Padri Silvanio na Sista Mariastela walivyoweza kuelewa vizuri kona za jengo hilo, ikiwa ni pamoja na mahali vyoo kwenye ukumbi vilipokuwa, hakuna mtu aliyewaonyesha walipotaka kuvitumia, walinyoosha wenyewe kama wenyeji wa jengo.
Sherehe ilimalizika saa tisa na nusu usiku, Padri Sivanio na Sista Mariastela wakapelekwa kwenye nyumba ambako Dk. Viola na Vanessa waliishi, kila kitu kilikuwa kimeandaliwa kwa ajili ya wao kulala vizuri. Wafanyakazi waliwapokea vyema na kuwaonyesha vyumba vyao, baada tu ya kuingia ndani, Padri Silvanio alitokeza nje na kuanza kuita.
“Vicky! Vicky!”
“Yes boss!” (Ndiyo bosi)
“Can I have a bottle of water?” (Naweza kupewa chupa ya maji?)
“Yes boss, warm or cold?” (Ndiyo bosi, ya moto au baridi?)
“Warm!” (Ya moto)
“Two minutes!” (Dakika mbili nitakuwa nimeyaleta)
Vicky, msichana wa Kichaga, kutokea Marangu-Mamba mkoani Kilimanjaro aliyefanya kazi na Dk. Viola tangu aanze kuishi kisiwani Bongoyo ambaye kifo chake kilimuumiza mno kwani alimsaidia mambo mengi katika maisha katika muda aliofanya kazi kwake, alikimbia haraka hadi jikoni na kuchukua chupa kubwa ya maji ya Kilimanjaro na kumletea Padri Silvanio.
“Thank you Vicky!” (Asante Vicky!)
“You are welcome, how did you know my name?” (Karibu, umenijuaje jina langu?)
“I heard someone calling you!” (Nimemsikia mtu akikuita!)
“Ohw!” alijibu kwa mshangao akionekana kama hajaridhishwa na jibu alilokuwa amepewa.
Alichokifanya baada ya kunywa maji Padri Silvanio ilikuwa ni kumpigia simu Sista Mariastela chumbani kwake wakaanza kuongea mambo mbalimbali kuhusiana na kilichotokea, wakipongezana na kusifiana kwa bahati kubwa waliyoipata! Sauti walizotumia zilikuwa ni za chini mno, kiasi kwamba hapakuwa na uwezekano wa mtu yeyote kusikia walikuwa wakiongea nini, walifanya hivyo kwa makusudi kwa sababu hawakutaka kabisa mtu apate picha ya kilichokuwa kikiendelea.
“We are back from hell!” (Tumerejea kutoka kuzimu!)
“Sure, it will take them forever to know the underground secret!” (Hakika, hawatafahamu milele siri iliyojificha chini ya ardhi!)
“Let’s enjoy our life!” (Hebu tufaidi maisha yetu!)
Ilikuwa siku ya furaha mno kwao, hawakumuonea huruma wala kumfikiria mwanasheria Crapton aliyekuwa amedhamiria kuurithi utajiri huo kwa dhuluma, baada ya mazungumzo yao, haukupita muda mrefu mno wakasinzia na kuamka asubuhi siku iliyofuata na kujiandaa kuelekea ofisini kwao ghorofa ya chini kutoka mahali walipolala ndani ya jengo hilo.
Maisha yao yakawa ni ya kazi tu, haikuwa rahisi hata kidogo kuamini walikuwa ni watawa, walichokiwaza ni kukuza kampuni kutoka pale ilipokuwa na kuipeleka kwenye hatua nyingine kubwa zaidi! Ndivyo ilivyotokea, wafanyakazi wote ndani ya kampuni hiyo walihamasika na kujikuta wameiga mwenendo na tabia ya Padri Silvanio na Sista Mariastela walivyofanya kazi karibu usiku na mchana, kampuni ikaendelea kukua.
Miaka miwili baadaye walinunua kampuni kubwa ya habari nchini Tanzania iliyoitwa Tanzania Media Corporation, ambayo ilimiliki vituo vya televisheni, redio na magazeti yaliyosomwa na watu wengi zaidi nchini Tanzania na Afrika ya Mashariki, walinunua kampuni hiyo si tu kwa kutaka faida bali walitaka kuongeza nguvu yao na ushawishi nchini Tanzania, bahati nzuri kulikuwa na uchaguzi mkuu mwaka huo, vyombo vyao vyote vya habari vilimuunga mkono mgombea wa chama tawala ambaye hatimaye aliibuka mshindi.
Kwa ushindi huo kampuni yao ilipewa heshima kubwa na wanasiasa, hicho ndicho walichokitaka Padri Silvanio na Sista Mariastela ili waweze kuwa na nguvu, jambo ambalo lingewahakikishia usalama wao na mali zao, hakika wakawa ni watu wasioguswa na mtu yeyote hata pale walipovunja sheria.
Kilichowashangaza watu wengi ni uamuzi wao mwaka mmoja baadaye wa kuamua kuuza kila kitu ghafla ili waondoke nchini Tanzania kuelekea mahali ambako hawakumwambia mtu yeyote, kampuni ya Kimarekani iliyoitwa Property America Inc. ndiyo iliyojitokeza kununua kampuni zote zilizomilikiwa na Padri Silvanio na Sista Mariastela kwa gharama ya dola bilioni nne za Kimarekani.
Mkataba ulitarajiwa kusainiwa siku mbili baada ya makubaliano hayo kwenye Hoteli ya Kilimanjaro, mbele ya wanasheria na maofisa mbalimbali wa Serikali ya Tanzania, watu walikuwa na huzuni lakini Padri Silvanio na Sista Mariastela walionekana kuwa na furaha mno na waliahidi kutoa asilimia thelathini ya fedha zote ambazo wangelipwa kusaidia jamii ya wasiojiweza nchini Tanzania, jambo ambalo liliwafurahisha watu wengi.
Saa sita na nusu tayari walishaketi kwenye meza, mikataba ikawekwa mezani, waandishi wa habari na kamera zao wakiwa tayari kupiga picha na kushuhudia utiaji saini mkataba huo, ukumbi ulikuwa umejaa watu wengi waliotaka kuwa sehemu ya historia hiyo.
***
Saa tano kamili asubuhi kwenye Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam, ndege aina ya Airbus ilitua kutokea Dubai, ndani yake alikuwemo Dennis Crapton, akirejea Tanzania baada ya miaka mitatu. Kitu cha kwanza alichokifanya akiwa nje ya uwanja ni kukodisha teksi akimwamuru dereva aendeshe kwa kasi kuelekea Kivukoni.
Hapo alipanda pantoni lililompeleka hadi kisiwani Bongoyo ambako alikodisha teksi nyingine iliyompeleka ofisini kwa Padri Silvanio na Sista Mariastela, lengo lake lilikuwa kukutana na watu hao, akaambiwa hawakuwepo ofisini wakati huo.
“Wako wapi?”
“Wamekwenda mjini kusaini mkataba, wameuza kila kitu na wanategemea kuondoka leo hapa nchini!”
“Kwenda wapi?”
“Hata sijui.”
“Wamekwenda mjini sehemu gani?”
“Kilimanjaro Hotel!”
“Asante.”
Akakodisha teksi nyingine iliyomrejesha tena Kivukoni na kupanda pantoni ambalo lilimrejesha mjini, akashuka na kuchukua teksi tena akimwamuru dereva aendeshe haraka kwenda Kilimanjaro Hotel, hakutaka kupoteza wakati, ilikuwa ni lazima akutane na watu hao kabla hawajaondoka nchini.

Je, nini kitaendelea? Kwa nini Dennis Crapton anawatafuta Padri Silvanio na Sista Mariastela? Fuatilia Jumatatu katika Gazeti la Championi.

Leave A Reply