The House of Favourite Newspapers

Madaha, Kwa Vee Money Ni Wivu Tu

0
Staa wa muziki wa Bongo Fleva, Baby Joseph Madaha.

MUZIKI wa Kizazi Kipya maarufu kama Bongo Fleva umepita katika njia nyingi sana hadi kufika hapa ulipo leo, ambako wanaoufanya wanatengeneza fedha nyingi tofauti na waasisi wake walivyofanya siku za nyuma.

Mashabiki, kulingana na umri wao, wamekuwa wakitofautiana, baadhi wakidai ‘ngoma’ za zamani zilikuwa ndizo zenyewe huku wengine wakiupa uzito mkubwa muziki wa sasa, hasa ule unaochanganywa na vionjo vya kutoka Afrika Magharibi, hususan Nigeria.

Msanii wa Bongo Fleva, Vanessa Mdee.

Na kadiri siku zinavyokwenda, unakuja na vijana wapya ambao nao wanakamata kijiti kwa muda, kwani wakati wao wa kuwapisha wengine utafika ilimradi Bongo Fleva itaendelea kuwepo kizazi hadi kizazi.

Nimekuwa mdau wa muziki huu kwa kiwango cha kuridhisha kidogo, kiasi kwamba angalau ninaweza kusema chochote, hata kama si kwa unyoofu wa rula. Ninapomtazama Baby Madaha, yule dada mwimbaji na muigizaji pia, namuona ni mmoja kati ya vijana waliojaribu kuweka bidii kwenye sanaa ili waweze kuendesha maisha kwa staili hiyo.

Nimem-fahamu tangu akiibukia katika Shindano la Bongo Star Search (BSS) mwaka ule wa 2007 maana ni mmoja kati ya wasanii waliojitokeza na kupata jina. Hakuwa mshindi, lakini ameweza kuwekeza na kubakia na ‘ujiko’ kuliko hata mshindi mwenyewe.

Ana nyimbo kadhaa zilizomtambulisha kama Summer Holiday, Nimezama, Nawaponda na Mahaba Niue. Amekaakaa kama rapa hivi ingawa anaimba vizuri. Kibao chake kikubwa zaidi ni Amore.

Lakini pia anafanya vizuri kwenye muvi na nimeshaziona kadhaa. Tazama filamu kama Misukosuko, Ray Of Hope, Tifu la Mwaka na Blessed By God. Ni halali yake kujiita msanii, tofauti na waigizaji wasanii waliojazana mjini.

Kuna kitu kimoja amekiongea siku chache zilizopita, ambacho kimenifanya nimgeukie na kuzungumza- naye kidogo kupitia safu hii. Katika kitu unachoweza kukitafsiri kama kuponda, Baby Madaha alisema mwimbaji mwenzake, Vanessa Mdee, ‘Vee Money’ siyo ‘mtamu’ kivile kimuziki na kwamba yeye siyo shabiki wake na zaidi, wadau wa muziki wanampa sifa asizostahili!

Kwamba haufurahii muziki wa Vanessa na kuwa yeye siyo shabiki wake, ni jambo la kawaida, kwa sababu kila mmoja ana mtu wake. Hata mimi nina mwanamuziki ninayemzimia, ninayemuelewa kuliko wengine na sioni dhambi kulisema hilo.

Lakini unapofikia na kusema ‘anabebwa’ linakuwa ni tatizo. Anabebwa na nani labda? Media? Kama ni vyombo vya habari ni vipi, hivi vya hapa nyumbani? Mbona anasikika na nje pia au nako anabebwa?

Vanessa anaweza akawa hafanyi muziki mzuri wa kumfurahisha Baby Madaha kama ule wanaofanya Lady Jaydee na Mwasiti anaowapenda, lakini kusikika kwa muziki katika media ni zaidi ya kazi nzuri.

Muziki ni biashara na biashara ni mipango. Unaweza ukawa na muziki usiopendeza, lakini ukatengeneza video yenye viwango na ubora.

Ninatambua uwezo wa Baby Madaha kimuziki, lakini pia najua kuwa msanii huyu siyo mzuri katika namna ya kujitengeneza ili aweze kupenya. Haonyeshi kuwa mtu wa mipango ya kuusogeza mbele muziki wake na anatumia muda mwingi kuamini katika ‘zali la mentali’.

Aina ya watu anao-hang nao siyo watu wanaoweza kuusogeza muziki wake mbele. Kuna wakati unapotaka kupiga hatua, iwe kurudi nyuma au kusonga mbele, kuna aina ya watu ni lazima uachane nao, hata kama ni ndugu.

Msanii kama Baby Madaha hawezi kumponda mtu kama Vanessa Mdee, kwamba sifa anazopewa ni ‘madaraka ya kulevya’, vinginevyo mtu anaweza kutafsiri kama ni wivu tu wa watoto wa kike.

NA OJUKU ABRAHAM, +255 719 786 355 | IJUMAA | ZA CHEMBE LAZIMA UKAE

Leave A Reply