The House of Favourite Newspapers

MADAI NDOA YA DOGO JANJA KUVUNJIKA, OFM YATINGA KWA UWOYA

DAR ES SALAAM: Baada ya tetesi nyingi kuvuma mitandaoni, zikidai kuwa ndoa ya msanii wa Bongo Fleva, Abdulaziz Chande ‘Dogo Janja’ na Irene Uwoya imevunjika na kwamba wawili hao hawaishi tena pamoja, Kikosi Kazi cha Kufichua Maovu (OFM) cha Global Publishers kimeibuka ‘kininja’ nyumbani kwa mrembo huyo maeneo ya Makongo Juu, jijini Dar na kubaini ukweli wa mambo.

ISHU ILIVYOANZA

Hivi karibuni, zilianza kusambaa picha na video za Uwoya zikimuonyesha yupo nchini Dubai akila raha na mwanaume mwingine, ambaye hata hivyo, hakuweza kujulikana kwa haraka ni nani, lakini baada ya muda Uwoya alimposti mwanaume huyo katika akaunti yake ya Instagram na kueleza kuwa si mwanaume wake kama ambavyo watu wamekuwa wakiongea bali ni rafiki tu.

MTOA UBUYU MWINGINE

Pamoja na Uwoya kukanusha madai hayo, mtoa ubuyu mwingine aliyeomba hifadhi ya jina lake alieleza kuwa, wawili hao wameshamwagana na kwamba Dogo Janja ameshaondoka katika nyumba aliyokuwa anaishi na Uwoya. “Nyie fuatilieni, angalia sasa hivi hata kwenye akaunti zao hawapostiani kama zamani, Uwoya yupo bize na mambo yake, Janja naye kivyake,” alisema mtoa ubuyu huyo.

OFM YATINGA KININJA

Baada ya kushibishwa madai hayo, mapema wiki hii, OFM iliamua kutinga ‘full nondo’ nyumbani kwa Uwoya ili kubaini ukweli. Kutokana na nyumba hiyo kuwa ya hadhi ya kistaa, OFM ililazimika kufanya utafiti wa namna ya kufika kwa kuepuka kuulizwa maswali mengi na mlinzi na pengine kuzuiliwa getini. Kabla ya kuzama ndani, makachero waliokuwa na vinasa sauti pamoja na kamera za picha mjongeo (video) na mnato walikita kambi nje ya nyumba hiyo kwa saa 11 tangu asubuhi mpaka jioni.

 

Katika kambi hiyo mambo mengi yalifanyika ikiwa ni pamoja na kuwahoji baadhi ya majirani na kufuatilia nyendo za nyumbani kwa mrembo huyo. “Mh! Kwa kweli sina hakika kama wameachana, ingawa nina muda kidogo sijawaona pamoja hapa nyumbani,” alisema mmoja wa majirani ambaye hakupenda kutajwa jina lake.

 

MWANDISHI AZUIWA GETINI

Baada ya kufanya mahojiano ya kutosha na kupeleleza mazingira mazima, mwandishi wa OFM alifika getini kwa lengo la kuingia nyumbani kwa Uwoya lakini mambo yalikuwa magumu.

Mlinzi: Sijaambiwa nikuruhusu.

MWANDISHI: Nenda kaniulizie ndani kwa wenyeji wangu.

Mlinzi:Umesema unamtafuta Uwoya? Nimekuambia hayupo sasa unataka nikakuulizie kwa nani?

Baada ya mwandishi kukwama katika ushawishi wa kumlainisha mlinzi aliamua kundoka na kwenda kuungana na timu ya uchunguzi kwa ajili ya kubadilisha mbinu. Baada ya saa 6 kupita mkuu wa kikosi cha OFM alipendekeza aende msichana mrembo ili amshawishi mlinzi aweze kuingia ndani, jambo ambalo lilifanywa.

OFM WAZAMA NDANI

Akiwa na uso mchangamfu msichana wa OFM aligonga geti na kufunguliwa na kijana mmoja.

OFM: Habari yako?

Kijana: Salama nikusaidie nini?

OFM: Nina shida na Irene Uwoya.

Kijana: Wewe ni nani yake?

OFM: Ni mdogo wake nimetokea Mikocheni nimepita hapa kuja kuwasalimia mara moja.

Kijana: Irene hayupo.

OFM: Kaka najua kama hayupo lakini wote nyumba nzima wameondoka?

Kijana: Basi yaishe, pandisha mpaka floo ya pili ndiyo anaishi huko.

OFM: Ahsante.

OFM alipanda hadi ghorofa ya pili alipoelekezwa na mlinzi. Alipofika huko alikuta viatu vingi mlangoni, baada ya kubisha hodi zaidi ya mara tatu, ilisikika sauti ya mama mtu mzima ikisema karibu mpaka ndani. Mwandishi alipokaribishwa akaomba atoke mara moja akawaingize rafiki zake.

“Samahani kuna rafiki zangu nimewaacha nje ngoja niwachukue mara moja mama narudi,” alisema mwandishi na kundoka huku akikubaliwa na mwenyeji. Mbinu hiyo ilisaidia kuwangiza OFM wengine wawili ambao walishirikiana katika kukamilisha uchunguzi wao.

 

SEBULE KAMA UWANJA WA TAIFA

OFM ilipozama ndani ilishuhuduia bonge la sebule linalonukia marashi si ya nchi hii. Sebule hiyo imesheheni makochi ya kisasa, ‘Flat’ skrini kubwa na ya kisasa.

‘FULL’ MAPICHA

Kabla ya kufanya mazungumzo, OFM alishuhudia picha kubwa moja ya Dogo Janja ambayo ilikuwa imebandikwa ukutani, na picha zingine tatu ndogo ambazo zilikuwa zimekaa juu ya meza; moja ilikuwa ni ya Uwoya, ya pili ilikuwa ni ya Dogo Janja ikafuatia picha ya mtoto wa Uwoya aliyezaa na marehemu mumewe Hamad Ndikumana, Krish.

Yule mama alimwambia OFM wetu wakae kwenye kiti ili akamuite mhusika ndani. Punde akatoka dada mmoja anayefahamika kwa jina la Zaimbaji ambaye Uwoya humtambulisha kama dada yake kwenye mitandao ya kijamii na mazungumzo yakawa hivi:

Zaimbaji: Karibu.

OFM: Ahsante, nilikuwa nina shida na Uwoya sijui nimemkuta. Mwandishi mmoja aliuliza.

Zaimbaji: Hapana, Irene (Uwoya) hayupo, kasafiri ila anatarajia kurudi siku si nyingi.

OFM: Ahaa sawa, hivi ameenda wapi?

Zaimbaji: Yupo Dubai

OFM: Na Dogo Janja je?

Zaimbaji: Naye pia hayupo, kasafiri.

OFM: Wamesafiri wote?

Zaimbaji: Ndiyo ila kila mtu kaenda sehemu yake, kwani wewe ni nani kwao naona una maswali mengi.

OFM: Mimi ni rafiki yao nilikuwa nina shida nao. Lakini kila nikiwapigia simu hawapokei, ndiyo nikaona nije hapa moja kwa moja.

Zaimbaji: Ok!

OFM: Lakini si bado wanaishi wote hapa? Au kila mmoja anaishi kivyake?

Zaimbaji: Mh! Wewe mwandishi nini, mbona una maswali hivyo?

OFM: Ndiyo mimi ni mwandishi wa habari nimetokea Global Publishers, hebu niambie sasa hivi ni kweli Uwoya na Janja wanaishi wote hapa?

Zaimbaji: Hahaha.

OFM: Mbona unacheka.

Zaimbaji: Nimefurahi; bado wanaishi wote, na hata wakirudi watakuwa wote hapa, niachie namba yako ya simu ili wakishafika nikupigie.

OFM: Sawa haina shida namba yangu ni 076689… (akamtajia namba kamili), basi wakirudi naomba ufanye hivyo, ngoja niwaache, nashukuru sana.

Zaimbaji: Haya karibu tena.

Hata hivyo; baada ya kukamilisha uchunguzi huo na kuelezwa kuwa ndoa hiyo ingali hai bado fununu za wadaku zilikataa ukweli huo na kudai kuwa wawili hao wameachana. “Mi nikuulize huko Dubai Uwoya anafuata nini? Anabishara kusema anakwenda kuchukua huko? “Mke wa mtu kwenye mahoteli makubwa ni sawa kweli, mimi nakuambia ndoa haipo na kama huamini subiri siku utakayoamini, lakini utakuwa umechelewa,” chanzo chetu kilisema kwa sharti la kutokutajwa jina.

HUYU HAPA DOGO JANJA

OFM ilipoona mambo yanakuwa mengi ilimtafuta Dogo Janja kwa lengo la kusikia msimamo wake, lakini alipopigiwa simu na kuelezwa kila kitu alisikiliza baadaye akakata simu. Uwoya kwa upande wake hakuweza kupatikana lakini kwenye mitandao ya kijamii ilionesha kwamba mrembo huyo bado yuko Dubai anakula bata na wasiojulikana.

Comments are closed.