The House of Favourite Newspapers

Serikali Yawasilisha Marekebisho Sheria ya TLS, Wabunge ni Marufuku

SERIKALI imewasilisha marekebisho ya Sheria ya Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) sura namba 307 ambapo sasa watumishi wa umma, madiwani, wabunge na viongozi wa vyama vya siasa hawataruhusiwa kugombewa ujumbe wa Baraza la TLS.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Katiba na Sheria bungeni juzi  Septemba 7 2018, mjumbe wa kamati hiyo Dk Damas Ndumbaro alisema marekebisho hayo yanalenga pia kuongeza vifungu vidogo na kuboresha mtiririko wake.
Alisema vifungu vinavyoongezwa katika muswada huo vinaweka sifa za mtu kuchaguliwa kuwa mjumbe wa baraza hilo ambapo mjumbe husika anatakiwa kuwa raia wa Tanzania, amethibitishwa kuwa na akili timamu.
Sifa nyingine zinazoongezwa ni kuwa hajatangazwa kuwa mufilisi na amethibitishwa na kamati ya uteuzi kuwa na weledi.
“Marekebisho yanayopendekezwa yanakusudia kutoruhusu mtumishi wa umma, diwani, mbunge ama kiongozi wa chama cha siasa kugombea ujumbe wa baraza hilo,”alisema.
Alisema pia muswada huo unapendekeza kuongeza kifungu kinachohusu kuzuia mjumbe wa baraza kujihusisha na shughuli za kisiasa na sheria.
Muswada huo umeainisha shughuli za kisiasa kuwa zinazokatazwa na sheria hiyo ni pamoja kugombea nafasi za kisiasa katika chama cha siasa, kupiga kampeni za kumuunga mkono au kumpiga mgombea yeyote chaguzi za kisiasa.
Shughuli nyingine ni kutoa hotuba za kampeni, kukusanya michango au kufanya harambee kwa ajili ya chama chochote cha siasa na kupanga au kusimamia maandamano ya kisiasa au mikutano au kuwa na nafasi ya madaraka katika vyama vya siasa.
“Inapendekezwa na ibara hii kuwa iwapo mjumbe atakiuka masharti atakuwa amefanya makosa makubwa ya kimaadili na ikitokea, mwanasheria mkuu wa Serikali anaweza kupeleka maombi katika kamati ya mawakili ili mhusika aondolewe kwenye orodha ya mawakili,”alisema Ndumbaro.
Pia muswada huo unapendekeza utungaji wa kanuni ufanywe na baraza kwa kushauriana Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kisha kanuni hizo zitatatikiwa kuchapishwa kwenye gazeti la Serikali.
Dk Ndumbaro amesema kamati hiyo imeridhia mapendekezo ya Serikali kwasababu yana lengo la kuimarisha misingi ya nidhamu, vigezo na mipaka ya kitaaluma kwa mawakili wa kujitegemea.

Comments are closed.