The House of Favourite Newspapers

Madaktari Wagundua Tatizo la Mbaraka Yusuf

Mshambuliaji wa Azam FC, Mbaraka Yusuf amegundulika kuwa hana tatizo kubwa sana kama ilivyoelezwa hapo awali. Madaktari wa Afrika Kusini, wamewaambia Azam FC kuwa mshambuliaji wao huyo chipukizi ameumia lakini si kama alivyoelezwa hapa nyumbani Tanzania.
Kutokana na hali hiyo, Mbaraka ataungana na wenzake mara baada ya sikukuu ya mwaka mpya na kuendelea na mazoezi. Baada ya kuumia akiwa anaitumikia Tanzania Bara katika michuano ya Chalenji, aliporejea Dar es Salaam, alifanyiwa vipimo na kuonekana ana maumivu makali ya goti kupitia mfupa mdogo unaojulikana kama meniscus na alitakiwa kufanyiwa upasuaji.
Lakini Azam FC iliamua kumpeleka Cape Town, Afrika Kusini kwa ajili ya uchunguzi zaidi lakini majibu yamekuwa tofauti na inaonekana hajaumia kama ilivyoelezwa baada ya vipimo alivyofanyiwa hapa Tanzania.
Msemaji wa Azam FC, Jaffar Iddi amethibitisha kuwa mchezaji huyo atajiunga na wenzake mara tu baada ya sikukuu ya mwaka mpya. “Tayari ameanza mazoezi ambayo yanasimamiwa na daktari wa timu ambaye amepokea maelekezo kutoka Afrika Kusini,” alisema.

Comments are closed.