KATIKA hatua ya kukomesha ajali za magari mkoani Pwani imeamua kuwapima kilevi madereva wote wanaopita mkoa huo.
Zoezi la kuwapima madereva hao limefanyika tangu jana asubuhi maeneo ya Mizani Kibaha- Maili Moja likiongozwa na Mratibu Msaidizi wa Polisi Mkoa wa Pwani (RTO) Salum Morimori.
Lengo la kuwapima madereva hao ulevi ni kukomesha au kupunguza ajali ambazo zimekuwa zikisababishwa na madereva hao kizembe.
“Unajua ajali nyingi zimekuwa zikisababishwa kizembe na baadhi ya madereva kwa kunywa pombe na baadhi yao kuvuta bangi kwa madai kuwa wanapata (starter) ‘mori’. Sasa nasema ole wao, ”alisema kamanda huyo.
Akiongea na waandishi, Morimori alisema zoezi la kuwapima madereva walevi litakuwa endelevu katika mkoa huo na hatawafumbia macho madereva wazembe, walevi na wanaoendesha magari kwa mwendo kasi.
Aidha aliwataka madereva wote wa magari madogo, malori, daladala, na mabasi yanayoenda mikoani na nje ya nchi kutokupita katika mkoa huo wakiwa wamelewa.
“Dereva yeyote yule akijiona amekunywa pombe au amevuta bangi namuomba sana kama anataka kusafiri kwa amani basi aahirishe safari yake na asikanyage katika mkoa wangu wa Pwani, “ alisisitiza kamanda huyo.
NA ISSA MNALLY/RICHARD BUKOS/GPL
SHUHUDIA MADEREVA WAKIPIMWA KILEVI