The House of Favourite Newspapers

MAFINDOFINDO CHANZO CHA MARADHI YA MOYO KWA WATOTO

MWANAMKE kabla ya kubeba ujauzito ni muhimu kujiandaa miezi sita kabla. Katika kipindi hicho anapaswa kula vyakula bora na kujiepusha na ulaji usiofaa.  

 

Mwanamke anapaswa kuwa makini pia katika kipindi cha wiki 12 za kwanza za ujauzito atakaobeba kipindi hicho ni muhimu kwani ndipo ambapo viungo vya mwili wa mtoto huanza kuumbwa ndani ya tumbo la mama yake. Viungo vya mtoto huanza kuumbwa tumboni mwa mama katika kipindi cha wiki 12 za kwanza za ujauzito.

 

Mama anapokuwa amejiandaa kubeba ujauzito miezi sita kabla, anakuwa anakula vyakula bora, anaachana na ulaji usiofaa, uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe na mambo mengine kama hayo, inakuwa imesaidia kumwepusha mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo mbalimbali.

 

Iwapo mama hajajiandaa katika kipindi cha miezi sita kabla huwa ni hatari kwa mtoto aliyembeba tumboni mwake kwani ataendelea na maisha yake ya kawaida mfano ulaji usiofaa, uvutaji sigara na unywaji pombe hivyo kumuathiri mtoto.

 

TATIZO LA MOYO KWA WATOTO

Kwa asilimia 10 tu ndiyo tunajua sababu ya mtoto kuzaliwa na tatizo hili la ugonjwa wa moyo na mara nyingi chanzo huwa ni matatizo anayoyapata mama katika kipindi cha miezi mitatu ya ujauzito. Unakuta huenda mama alipata homa kali wakati wa ujauzito, virusi vya rubella, shinikizo la damu, kisukari au alikuwa anakunywa dawa bila ushauri wa daktari. Lishe duni yaani mama asipopata virutubisho vya folic acid, uvutaji sigara, unywaji pombe na sababu nyinginezo ikiwemo kurithi ingawa si kwa asilimia kubwa, mtoto hupata matatizo ya moyo.

 

Ndiyo maana mjamzito anashauriwa kuhudhuria kliniki katika kipindi chote ili wataalamu wa afya wafuatilie afya ya mtoto aliyepo tumboni na ukuaji wake. Katika kipindi hicho cha awali mama hupewa chanjo mbalimbali ikiwemo dhidi ya ugonjwa wa rubella ambao unaweza kumsababishia mtoto kupata magonjwa ya moyo.

 

Magonjwa ya moyo kwa watoto yapo ya aina mbili ambayo ni yale ya kuzaliwa nayo na yasiyokuwa ya kuzaliwa nayo. Haya ya kuzaliwa nayo chanzo chake ni iwapo mama hatapatiwa baadhi ya chanjo ikiwemo ya rubella na kama ataendelea na ulaji usiofaa.

DALILI ZA UGONJWA WA MOYO

Watoto waliozaliwa na tatizo la moyo huwa wanaonesha dalili tofautitofauti ikiwemo kuzaliwa na uzito mdogo kuliko kawaida. Wengine wanabadilika rangi isiyokuwa ya kawaida na wengine wakinyonya ziwa la mama hata kidogo tu huchoka haraka na kutokwa jasho kwa wingi.

 

Mtoto akinyonya kidogo na kutokwa jasho jingi ni ishara kwamba ana tatizo la moyo, wamuwahishe hospitalini. Kuchoka haraka ni dalili yao kubwa na unaweza kukuta wengine hawakui vizuri kama watoto wa rika lao, kwa mfano ikiwa amezaliwa na kilo mbili baada ya wiki mbili unaweza kukuta ana kilo hizohizo au zikiongezeka ni kidogo mno.

 

Mtoto akiumwa kifua mara kwa mara wazazi na walezi hudhani kuwa ni tatizo la nimonia lakini kumbe ni ugonjwa wa moyo. Mzazi anapoona mtoto wake anahema harakaharaka au anapata homa ya mapafu mara kwa mara, hizo zote ni dalili za magonjwa ya moyo.

 

KUHUSU MAFINDOFINDO

Iwapo mtoto ataugua mafindofindo (tonsillitis) na asitibiwe inavyopaswa huwa kwenye hatari ya kupata magonjwa ya moyo katika ukuaji wake. Ipo dhana mtoto akiugua mafindofindo wazazi wanamtibu kienyeji nyumbani (pasipo ushauri wa daktari) – wanakwenda dukani na kununua dawa za kumtibu au wanampatia maji ya moto anywe, hiyo si sahihi.

 

Vipo vyanzo vya aina mbili ambavyo husababisha tezi kuvimba, chanzo kikubwa kikiwa ni virusi na kwa asilimia ndogo husababishwa na bakteria. Hatumaanishi kwamba tezi zote zikivimba lazima upate dawa, isipokuwa ipo tezi ambayo ikivimba lazima upewe dawa kutibu na hiyo aina ya tezi usipopata dawa ndipo unaishia kupata tatizo la moyo.

 

Magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo yanapaswa kugundulika mapema ili kuokoa maisha ya mtoto husika. Katika kundi hili kuna magonjwa yapatayo saba, haya yanapaswa kugundulika mapema ingawa yapo mengine si magonjwa ya kuzaliwa nayo ambayo yanapaswa nayo kugundulika mapema kabla mtoto hajafikisha mwaka mmoja.

TIBA

Mtoto akizaliwa na magonjwa ya moyo upasuaji hufanyika mara moja ili kumsaidia kutibu tatizo. Kwa kuwa watoto wengi huwa hawagunduliki mapema na matokeo yake asilimia 25 hufariki kabla ya kufikisha mwaka mmoja. Asilimia nyingine 25 wakibahatika kufikisha mwaka mmoja na nusu hufariki dunia na wakifikisha miaka miwili hadi mitatu asilimia 80 hadi 90 hufa iwapo wakicheleweshewa matibabu.

 

Watoto wengi huchelewa kugundulika mapema kwani hucheleweshwa kufikishwa hospitalini na wazazi au walezi wao kwa sababu, mara nyingi magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo dalili zake hufanana na magonjwa mengine ya kawaida kwa watoto kama malaria, nimonia na utapiamlo.

 

Kwa kuwa zile dalili zinafanana na magonjwa mengine ya watoto, wakati mwingine huchukua muda mrefu hadi mtu anayemuona mgonjwa ahisi kwamba mtoto husika anasumbuliwa na tatizo la moyo, wengine hufikishwa hospitali wakiwa katika hatua mbaya kiasi kwamba haiwezekani tena kuwafanyia upasuaji.

 

Kuna aina ya magonjwa ya moyo ambayo mtoto huzaliwa nayo hivyo anatakiwa afanyiwe upasuaji akiwa na mwezi mmoja, mitatu au mwaka mmoja, akizidi umri huo haiwezekani tena.

USHAURI

Uonapo dalili zozote tulizozitaja hapa kwa mtoto wako, muwahishe hospitali akapimwe ili apewe dawa sahihi.

Comments are closed.