The House of Favourite Newspapers

Mahakama ya Rufaa Yatupilia Mbali notisi ya Rufaa Kuendelea Kushikilia Mafuta ya Burundi

0
KAMPUNI mbili za kigeni, Numora Trading PTE Limited kutoka Singapore na Lamar Commodity Trading ya Dubai zimekwama mahakamani kuendelea kushikilia tani 20,685.61 za petroli yenye thamani ya Shillingi za Kitanzania 43bn/-, mali inayodaiwa kuwa ya kampuni ya Prestige Investment kutoka Burundi.
Katika uamuzi uliotolewa hivi karibuni, Mahakama ya Rufani imetupilia mbali notisi za rufaa zilizowasilishwa na kampuni hizo mbili dhidi ya uamuzi uliotolewa na Divisheni ya Biashara ya Mahakama Kuu kuhusu shehena hiyo ya mafuta yaliyokuwa yanasafirishwa kwenda katika Jamhuri ya Burundi.
Majaji Mary Levira, Zepharine Galeba na Mustapher Ismail waliamua kwamba notisi za rufaa zilizowasilishwa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu zinatokana na amri ndogo ambayo hatima yake haimalizi au kuamua kwa ukamilifu shauri lililopo mahakamani.
“Kwa hiyo, tunakubali ombi hilo na kufuta notisi ya rufaa kwa gharama,” Majaji hao walisema katika uamuzi wao wa hivi karibuni kuhusu Kampuni ya Numora Trading PTE Limited. Majaji hao pia walifikia uamuzi kama huo wa kuikataa notisi nyingine ya rufaa iliyowasilishwa na Lamar Commodity Trading katika kesi hiyo.
Aidha, Majaji hao walikataa ombi lililowasilishwa na Numora Trading PTE Limited, kutaka kuzuia utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu kuachia shehena hiyo ya mafuta kwa sababu maombi hayo yalikuwa yameegemea kwenye notisi ya rufaa ambayo imekataliwa.
Katika uamuzi wao, Majaji walibainisha kuwa Mawakili wote wanakubaliana kuwa shauri la msingi bado linaendelea mahakamani, hivyo haki hairuhusu rufaa kuwasilishwa katika shauri ambalo halijafikia uamuzi wa mwisho na uliotolewa na Mahakama Kuu.
“Tuna maoni kuwa mwisho ambao una athari ya kuruhusu rufaa chini ya kifungu cha 5 (2) (d) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa ni mwisho wa shauri na sio sehemu ya masuala yaliyomo ndani ya shauri husika,” Majaji hao walisema.
Mbele ya Mahakama Kuu, mwombaji alilalamikia mienendo ya kampuni za Lamar Commodity Trading DMCCC na Nomura Trading PTE Limited, zilizosababisha kuzuiliwa kwa shehena yao ya mafuta ya petroli waliyokuwa wameagizwa kutoka nje kwa lengo la kuyasafirisha kwenda Jamhuri ya Burundi.
Ilidaiwa kuwa shehena hiyo iliuzwa kwa kampuni ya Lake Oil Limited huku mwombaji akitimiza wajibu wake wa malipo chini ya hati ya dhamana ya malipo ambayo ilitolewa na Benki ya KCB Kenya Limited kwa ajili ya kampuni ya Nomura Trading PTE Limited.
Mahakama ilikuwa na maswali kadhaa wakati shehena hiyo inasemekana kuuzwa kwa kampuni ya Lake Oils Limited, inayodaiwa kuwa na madai kwenye mafuta hayo.
Kadhalika, Mahakama ilijiuliza kama kulikuwa na mpango wa kuchepusha shehena hiyo kwa kampuni ya Lake Oils Limited au ulikuwa ni udanganyifu kati ya Lamar Commodity Trading DMCCC na Nomura Trading PTE Limited na Lake Oils Limited kama ilivyobainishwa na wakili wa mwombaji.
Katika mawasilisho yake, wakili wa mwombaji, alidai kuwa mnamo Julai 6 au 7, 2023, Benki ya KCB Kenya Limited ilipokea pesa za dola za Kimarekani milioni 15 kwa shehena ya mwisho.
“Kama inavyoweza kubainika, iwapo Julai 7, 2023 hali ilikuwa hivyo na tarehe hiyo hiyo shehena hiyo ilidaiwa kuuzwa kwa (Lake Oils Limited), ukweli huo unaonyesha nini? Je, haipendekezi kwamba uuzaji huo unaonesha vitendo vya ulaghai ikiwa hilo litatokea kuwa kweli?” mahakama iliuliza.
Mahakama haikuweza kujibu maswali hayo katika uamuzi wake na kwenda kwa ndani kutoa maelezo yoyote kwa vile hayo ni masuala yanayoweza kuangaliwa katika shauri la msingi. Ilibainisha tu kuwa kutoka na hati za viapo na nyaraka zilizoambatanishwa kuwa shehena inayodaiwa kuuzwa iliuzwa kwa Lake Oils Limited.
Wakati wa kusikilizwa kwa shauri hilo, Kampuni ya Prestige iliwakilishwa na Wakili Seni Malimi, huku Mawakili Nuhu Mkumbukwa, Stephen Axwesso, Godwin Nyaisa na Gasper Nyika wakiwakilisha Numora Trading PTE Limited, Lamar Commodity Trading, KCB Bank Kenya Limited na Lake Oil Limited.
Wakili wa mwombaji aliwasilisha kwamba uamuzi wa Mahakama Kuu ambao wajibu maombi walikuwa wanataka kuupinga hauwezi kukatiwa rufaa.
Aliiambia mahakama kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 5 (2) (d) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa, uamuzi huo ulikuwa mdogo ndani ya shauri ambao haumalizi shauri katika ukamilifu wake baina ya wahusika.
Hata hivyo, upande wa majibu maombi ulidai kuwa uamuzi wa mahakama Kuu ulikuwa na athari ambayo inaamua shauri kwa ujumla na kwamba kilichobakia ni maombi yasiyo na maana ambayo hayakuwa na umuhimu mkubwa.
Mawakili wa wajibu maombi walibainisha kuwa kuachiliwa kwa mafuta hayo kunahusiha madai ambayo mwombaji ameainisha katika shauri la msingi ambapo Mahakama Kuu imeshaamua kuwa walikuwa wamekiuka mkataba wa kusambaza mafuta hayo.
Mwombaji alitaka kuzuia au kupunguza madhara makubwa zaidi ikizingatiwa kuwa alilipa fedhazinazohusiana na shehena ambayo, hata hivyo, haikutolewa, kama inavyotakiwa. Wajibu maombi walidai kuwa ni mwombaji mwenyewe ndiye wa kulaumiwa kwa kuchelewesha malipo yake.
Hata hivyo, baada ya kuangalia vielelezo vilivyoambatanishwa na hati ya kiapo, ukweli unaelekea kuiambia mahakama hadithi tofauti kama ilivyokuwa Lamar Commodity Trading, ambaye hakuweza kuruhusu meli kufikisha shehena kwa wakati licha ya kuwa na uhakika wa malipo.
Mahakama pia ilibainisha kuwa wahusika hawakuwa wageni katika biashara kiasi cha kuwa na kiwango hicho cha kutoaminiana. Mahakama haikuona kuwa ni sawa kwamba Lamar Commodity Trading na Nomura Trading PTE Limited zilipaswa kuzuia kuachiwa kwa shehena hiyo.
Leave A Reply