The House of Favourite Newspapers

Maisha halisi ya Kassim Kayira

0

kassim kayiraKutoka mkimbizi, babantilie, BBC hadi Azam TV

Aeleza uwezo wa kuzungumza lugha na makabila 30

HELADIUS Banzi, mmoja wa madereva mahiri ofisini kwetu, naanza kumuona akiishiwa na uvumilivu wa kuendelea kusubiri. Macho yake yanaashiria kukata tamaa, lakini hataki kuniambia kwa mdomo, anaruhusu vitendo vinipe ujumbe, hakutaka kuendelea kuwepo eneo hilo.

Tuko Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar, lengo ni moja tu. Kumpokea mtu ambaye macho yangu yalikuwa na hamu kubwa ya kumuona, muda aliouahidi kufika jijini Dar, sasa ulikuwa umetimia.

Wakati natafakari jinsi ya kumtuliza Banzi, ghafla naona umati wa watu ukikodolea macho eneo la kutokea abiria, kila aliyefika mahali hapo kwa lengo la kupokea wageni, anasogea kwa ukaribu zaidi.

Ghafla namuona mtu aliyenifanya kuwepo eneo hilo, akivuta begi kubwa, miwani ya jua ikiwa kichwani, haraka sana namfuata na kujitambulisha tena kwake, huyu si mwingine bali ni mtangazaji maarufu ulimwenguni, kupitia Idhaa ya Kiswahili ya BBC yenye makao yake makuu katika jiji la London nchini Uingereza, Kassim Kayira.

“Ooh, ni wewe? Yeah kweli naipata picha yako sasa,” anasema Kayira wakati tukisalimiana, huku akijaribu kunikumbuka zaidi kwani tumekuwa tukiwasiliana  kupitia mitandao ya kijamii, sasa tumeonana ana kwa ana.

“Kabisa, ni mimi Brighton, karibu sana nchini Tanzania, karibu sana Kayira,” namkaribisha, tayari kwa safari ya kuelekea ofisini kukamilisha kilichotufanya tukutane, mahojiano.

“Aah, kuna watu wengine walitakiwa pia waje kunipokea hapa, lakini sasa siwaoni, sijui tufanyeje sasa,” anasema huku akiangaza huku na kule kama anayejaribu kubahatisha kitu.

“Akina nani hao?,” namuuliza huku nikimkazia macho.

“Hawa watu wa Azam TV, kama nilivyokueleza, naanza rasmi kufanya nao kazi, sasa siwaoni unashauri nini?

“Nadhani tuondoke kwanza, eneo hili huku mawasiliano mengine yaendelee, nashauri tuelekee ofisini kwao, kuanzia hapo tutajua ratiba kamili ya mahojiano yenu,” haraka sana Banzi aliyekuwa kimya anaingilia mazungumzo yetu kwa ushauri ambao sote tunajikuta tukikubaliana nao.

“Lakini mahojiano yaanzie njiani, hatuna muda wa kupoteza, sijachoka na niko tayari kwa kazi,” anasema Kayira.

“Sawa, hakuna shida, basi twendeni,” nasema na kumuonesha ishara ya kutufuata.

“Siwezi kuchoka nimeshazoea sana mambo ya safari, si unajua unapokuwa mtangazaji wa kimataifa, kusafiri mara kwa mara inakuwa sehemu ya maisha,” anasema tena Kayira na kugeuka nyuma ambapo namuona akichukua simu yake ya mkononi na kuanza kupiga picha mazingira ya uwanja wa ndege, hapohapo anamkabidhi Banzi simu na kumuomba atupige kwa pamoja, anafanya hivyo.

Kufika hapo, mimi na Kayira tunaamua kukaa viti vya nyuma kwa lengo la kuanza mahojiano wakati tukielekea yaliko makao makuu ya Azam Tv, Tabata Relini, Ilala.

“Unawezaje kuzungumza lugha ya Kiswahili kwa ufasaha namna hii?,” naanza kumuuliza huku nikifunua kitabu changu cha kumbukumbu (diary) tayari kwa kudondosha wino, huku nikiweka kifaa cha kurekodia sauti mahali ambapo kila kitu kitaratibiwa.

“Ni kujifunza tu, napenda sana lugha, si Kiswahili tu, nazumgumza zaidi ya makabila na lugha 30 duniani, si mchezo eti,” anajibu Kayira kwa lafudhi ya Kiganda huku akimalizia kufunga mkanda wa gari kwenye siti yake.

“Zingine ni zipi?,” namuuliza kwa shauku kubwa.

“Ooh, nazungumza Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu, Kireno, Kiitaliano, Kichina, Kikorea, Kihispaniola, Kijapani, na Kiswahili kwa upande wa lugha. Kwa makabila najua Kirundi, Kihaya, Kinyankore, Kihutu, Kitusi, Kinyoro, Kinende na Kirinashi na sasa naendelea kujifunza lugha na makabila mengine zaidi,” anasema Kayira huku akiachia tabasamu na kumfanya dereva, Banzi ageuke kumtazama huku akiachia kicheko kinachoashiria kunogewa na mazungumzo yetu.

KUZALIWA KWAKE:

“Wewe ni raia wa wapi na umezaliwa lini?,” namuuliza.

“Mimi ni Mganda kwa upande wa baba na Mnyarwanda kwa upande wa mama, nilizaliwa Januari 27, 1974 huko Mbarara nchini Uganda, baba yangu anaitwa Sheikh Ibrahim Kayira na mama yangu anaitwa Hajat Amina ,” anasema Kayira na hapohapo simu yake inaita mfululizo.

“Ooh, samahani kidogo,” anasema kabla ya kupokea.

“Hakuna shida kaka,” namjibu kwa sauti ya upole kabisa huku nikimtazama usoni.

Baada ya kumalizana na simu yake, mazungumzo yanaendelea.

Je, nini kitafuata? Usikose kufuatilia wiki ijayo.

Leave A Reply