Maiti Iliyozikwa na Baadae Kukutwa Kitandani Nyumbani, Yazikwa Tena kwa Ulinzi Mkali wa Polisi
MBEYA: Maiti ya mtoto Haruna Kyando (9) ambayo ilikutwa nyumbani muda mfupi baada ya wananchi kutoka makaburini kumzika, imezikwa kwenye makaburi ya Isanga chini ya ulinzi wa askari wa Jeshi la Polisi nchini, huku waombolezaji wakiaga mwili huo kwa kufunuliwa jeneza eneo la kichwani makaburini hapo.
Hatua hiyo ilizua taharuki kubwa kiasi cha wananchi kutaka kufahamu ni kitu gani kilichozikwa ndani ya jeneza na ndipo Jeshi la Polisi lilipoingilia kati, kuzuia kufukuliwa kwa kaburi husika.
Lakini juzi baada ya kukamilishwa kwa taratibu husika, ikiwemo kupatikana kwa kibali kutoka mahakamani, saa nne na nusu asubuhi, Polisi Mkoa wa Mbeya walifika eneo la makaburi alipozikwa marehemu na kusimamia shughuli nzima ya kufukua kaburi hilo.
Nusu saa baadaye jeneza la mtoto huyo lilitolewa nje ya kaburi na ndipo Mwenyekiti wa Mtaa wa Igoma A, Fredy Mwaiswelo alipofunua jeneza na kukuta ndani kukiwa tupu, hali iliyoashiria mwili wa marehemu haukuwekwa ndani ya jeneza wakati wanakwenda kuzika.