The House of Favourite Newspapers

Maiti ya Mbongo kuzuiliwa India, baba bado ahaha!

0

Stori: Mwandishi Wetu, WIKIENDA
DAR ES SALAAM: Baada ya mtoto Abel Machanga aliyefia India akipata matibabu na maiti yake kuzuiliwa kutokana na deni la matibabu, baba mzazi, Revocatus Machanga bado anahaha kupata pesa za kulipa ili kuuleta mwili wa mwanaye Bongo.

Abel alikutwa na mauti Desemba 31, 2015 akiwa kwenye matibabu nchini humo, mbaya zaidi, maiti yake imezuiliwa kutolewa mochwari mpaka familia ilipe deni la shilingi milioni thelathini na tano.

Abel alianza kuugua Novemba 2014 akiwa denti wa Chuo cha Biashara Dar (CBE). Alivimba macho, yakatokeza nje, akapoteza uwezo wa kuona huku pia akipumua kwa shida.

Alitibiwa Hospitali ya Macho CCBRT, Dar ikashindikana, akapelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, hali ilizidi kuwa mbaya. Novemba 24, 2015, ndugu wakampeleka India.

Kwa mujibu wa mzee huyo, baada ya kufika India kwa fedha zilizochangwa na wasamaria wema, wakiwemo wasomaji wa Gazeti la Uwazi (habari ya ugonjwa wake ilichapishwa na gazeti hilo), alifanyiwa vipimo upya Hospitali ya Rufaa ya Columbia Asia.

“Alibainika kuwa na ugonjwa wa Amelobeblastoma na matatizo ya wadudu kwenye meno, pua, macho, kichwani kwenye ubongo. Inaendelea Uk. 4 Inatoka U. 3
“Alifanyiwa upasuaji wa kwanza, madaktari wakafanikiwa kuondoa asilia 60 ya uvimbe. Alipopata nafuu, alifanyiwa upasuaji wa pili, akaondolewa asilia 40 ya uvimbe na hali yake ikaendelea vizuri.

“Hata hivyo, mchana wa Desemba 31, 2015 mwanangu alifariki dunia baada ya shinikizo la damu kushuka kupita kiasi,” alisema mzee Machanga.

Mzee huyo aliendelea kusema, fedha walizochangiwa na wasamaria wema Tanzania hazikutosha kutokana na kubainika matatizo mengine ambayo yalisababisha kifo chake na kuacha deni la shilingi milioni 35 hospitalini hapo.

Mzee Machanga aliendelea kusema kwamba kutokana na deni hilo, hati za kusafiria za marehemu na ya kaka yake aliyekuwa akimuuguza kule, zinashikiliwa na uongozi wa hospitali hiyo huku pia wakikataa kuutoa mwili wa marehemu.

“Niliandika barua wizara ya afya kuomba msaada lakini nilijibiwa kuwa, kwa kuwa mwanangu hakusafirishwa kwa taratibu za serikali, ikiwemo kupata rufaa kutoka Muhimbili na kuidhinishwa na wizara, wasingeweza kunisaidia lolote.

“Nawaomba Watanzania kama mlivyoweza kunisaidia mara ya kwanza, mnisaidie pia kwa hali na mali ili maiti yake iletwe tumzike kwa heshima zote hapa nyumbani Tanzania,” anahitimisha baba wa marehemu, mkazi wa Ukonga- Mombasa, Dar.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipotafutwa kwa njia ya simu juzi, hakupatikana. Kwa aliyeguswa na habari hii, awasiliane na baba wa marehemu kwa simu namba 0713 275740, 0752 275740 na 0784 275740. Kutoa ni moyo! Mungu aipumzishe roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.

Leave A Reply