Maiti ya mwanamke yakutwa kwenye dimbwi

Gresia Chilindo enzi za uhai wake.

Na Gregory Nyankaira

Gresia Chilindo, 74, mkazi wa Kijiji cha Singu, Kata ya Kukirango, Butiama, mkoani Mara ameokotwa akiwa amefariki dunia ndani ya dimbwi la kunyweshea mifugo lililopo katika kijiji hicho.

Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo lilitokea Septemba 7, mwaka huu, walisema kwamba, awali bibi kizee huyo aliondoka nyumbani kwake Septemba 6 na kwenda mnadani Kiabakari kutafuta mahitaji ya kawaida akiwa na afya njema na jioni alionekana kwenye nyumba moja kijijini hapo akinywa gongo.

Walisema kwamba siku hiyo bibi huyo hakurejea nyumbani jambo lililomlazimu kijana wake , Korie Chilindo kuamua kumfuatilia ndipo alipokuta kundi kubwa la watu wakipiga mayowe pembezoni mwa dimbwi baada ya kukuta maiti ndani ya dimbwi hilo na alipoitazama alibaini kuwa ni mama yake.

Mwili wa Gresia Chilindo baada ya kuopolewa kutoka kwenye dimbwi.

Kifo cha mama huyo kimezua taharuki kubwa miongoni mwa wananchi pamoja na ndugu wa marehemu. Baadhi wanaamini kuwa aliuawa kisha kutupwa ndani ya maji katika dimbwi hilo ili kuficha ushahidi lakini wengine wakidai kuwa huenda alitumbukia kutokana na kulewa pombe baada ya kupotea njia ya kwenda kwake.

Dimbwi alilokutwa Gresia Chilindo.

Mganga wa Zahanati ya Mwanzaburiga aliyejitambulisha kwa jina moja la Musiranga, aliyeufanyia uchunguzi mwili huo alisema: “Marehemu hakuwa na majeraha ambayo yangesababisha kifo hicho.”Polisi wilayani Butiama wamethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kuwa, hakuna mtu aliyekamatwa au kuhusishwa na kwamba wanaendelea na uchunguzi.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!


Loading...

Toa comment