The House of Favourite Newspapers

Majaliwa: Serikali Itaendelea Kuthamini Mchango Wa Dini Katika Kutunza Amani

0

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kutambua na kuthamini mchango wa kamati za amani za viongozi wa dini zinazojumuisha dini zote na ambazo tangu kuanzishwa kwake, zimechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha amani nchini.

Amesema amani ambayo imekuwepo nchini tangu kupata uhuru imechangiwa kwa kiasi kikubwa na viongozi wa dini pamoja na Kamati za Amani za viongozi wa dini. “Upendo, utaifa na mshikamano ni mambo ya msingi kabisa katika kuimarisha amani, umoja na mshikamano.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Desemba 5, 2021) wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 100 ya Buddhism barani Afrika yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Mheshimiwa Majaliwa ametoa rai kwa viongozi, wafuasi na marafiki wa Buddha kwamba wanapoadhimisha miaka 100 ya Ubuddha barani Afrika, waendelee kuvumiliana na kustahimiliana hususan pale zinapotokea sintofahamu miongoni mwao.”

“Ninakupongeza sana wewe binafsi, Kiongozi wa Buddha Afrika ukiwa mjumbe wa kamati ya amani ya kitaifa na viongozi wengine wa dini kwa mchango mkubwa mnaoutoa kupitia kamati ya amani za kitaifa. Ninatambua kuwa katika kipindi cha takriban miaka 22 tangu kuanzishwa kwa kamati za amani, umekuwa miongoni mwa wadau wake muhimu.”

Sambamba na hilo, Waziri Mkuu amesifu taasisi za kidini za wabuddha ambazo zinatoa huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo kuwahudumia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu wasiopungua 100 katika kituo cha watoto yatima cha Chanika Children’s Shelter.

“Ninatambua kuwa kupitia taasisi yenu ya Kind Heart Africa Charitable Organization mmeendelea kutekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kuboresha utoaji wa huduma za kijamii nchini. Juhudi hizo zinajidhihirisha kupitia mradi wa Chanika Children’s Shelter (CCS) mnaoutekeleza kwa ubia na Human Welfare Trust (HWT).”

Leave A Reply