The House of Favourite Newspapers

MAJIBU YA UKIMWI YA DIAMOND GUMZO!

DAR ES SALAAM: Baada ya mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kuanika stika inyaoonesha amepima magonjwa yote, gumzo la aina yake limeibuka kwenye mitandao ya jamii huku kelele zaidi zikipigwa kwenye majibu hususan Ugonjwa wa Ukimwi.

 

Akiwa nchini Marekani katika ziara ya kimuziki hivi karibuni, Diamond aliweka ‘status’ kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram inayomuonesha mkononi amefunga stika maalum ya hospitali inayoashiria amefanyia vipimo vya mwili na ndipo mjadala mkali uliposhika kasi kama moto wa kifuu.

 

TUICHAMBUE KWANZA STATUS

Kwenye status hiyo ambayo hukaa muda mfupi na kuondoka, stika aliyoivaa mkononi ilionesha jina lake (Nasibu Abdul), tarehe aliyozaliwa (Oktoba 2, 1988) aliyofanya vipimo hivyo yaani Julai 22, mwaka huu huku akiambatanisha na ujumbe wa maandishi kwa lugha ya Kingereza.

Kwa tafsiri isiyo rasmi sana, ujumbe huo uliashiria kwamba; “ni vigumu kupima na kuhakikisha anarudi nyumbani bila maambukizi kwa kupima mwili mzima (full body checkup),” mwisho wa kunukuu.

BALAA LAANZIA HAPO

Mara baada ya kuandika ujumbe huo ulioonesha kwamba amechekiwa mwili mzima, wachangiaji mbalimbali waliochangia mtandaoni humo, walianza kujiongeza kwa kujadili suala zima la matokeo ya vipimo hivyo na zaidi kwao haikuwa katika majibu kama ya Homa ya Ini, Malaria au Kifua Kikuu bali wengi walijikita kwenye Ukimwi kwenye eneo hilo.Wapo walionesha wasiwasi na kupinga kuwa haiwezekani akawa salama lakini wapo pia ambao walisema inawezekana.

 

MREMBO ASHADADIA ISHU

Baada ya Diamond kuweka status hiyo, mrembo aliyejitaja kwa jina la Kei, aliinasa picha pamoja na ujumbe wake huo na kuiweka fasta kwenye akaunti yake ya Instagram huku akiiambatanishia maneno yake kama ifuatavyo:

“Kama Mond kapima ngoma.. basi Ukimwi haupo..ngoja na mimi nikapime kesho…”Maneno hayo yaliamsha uchangiaji wenye mgongano wa hoja kwa baadhi ya marafiki wa msichana huyo ambapo wengi walimshambulia kwa kujaribu kutilia shaka vipimo vya afya alivyofanya Diamond huko Marekani.

 

“Mshamba tu wewe, kupima kwake kunakuhusu nini au na wewe amekupitia?” “Mi napita tu wajamani.”“Mambo ni moto, hana ngoma mzee baba…tehe.”“Kwi, kwiii, kwiiiiiii.” Hizi zilikuwa ni baadhi ya fleva za wachangiaji katika posti hiyo huko kwingineko nako hakukua shwari.

MSURURU WA WAREMBO WATAJWA

Waliokuwa wanaonesha wasiwasi, walikwenda mbali zaidi kwa kuweka mezani warembo ambao wamewahi kuwapitia’ mkali huyo wa Bongo Fleva hususan wale mastaa na kuongeza na wale wasiojulikana.

 

“Jamani tuwe wakweli, we msururu wa warembo alionao Diamond kweli anaweza kuwa salama?” Alihoji mmoja wa wachangiaji mtandaoni. Mchangiaji mwingine alizidi kushusha data kwa kuanika msururu wa warembo wanaodaiwa kutembea na Diamond na kuanzia na Wema Sepetu (muigizaji), Jokate Mwegelo (modo na muigizaji), Penniel Mungilwa ‘Penny’ (mtangazaji), Irene Uwoya (muigizaji), Hamisa Mobeto (mwanamitindo), Lynn (modo) na Rehema Fabian (miss), orodha hii ibaki kuwa mali ya wachangiaji mitandaoni na siyo ya Amani.

 

Kuwekwa mezani kwa warembo hao na wengine wakidai hao ni baadhi tu ya watu maarufu na kwamba wapo wengine pia wasiokuwa mastaa, bado wengine waliiponda orodha hiyo kwa kusema haina mashiko kwani suala la Ukimwi linabaki kwenye hoja ya kupata mchubuko kati ya watu wawili wanaposhiriki tendo la ndoa.

DAKTARI ANENA

Ili kupata uelewa mpana wa jambo hilo lililozua gumzo mtandaoni, Ijumaa lilizungumza na daktari maarufu jijini Dar, Dk Chale ambaye alieleza kuwa, maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi husababishwa na mambo mbalimbali. Alisema ngono zembe huchangia, mtu kushea vitu vyenye ncha kali na mtu mwenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi kama sindano na wembe.

 

Mbali ya hilo, alisema upo uwezekano mdogo wa mtu kushiriki tendo la ndoa na mtu mwenye maambukizi na asipate maambukizi endapo hakutatokea mchubuko. “Lakini ni kwa asilimia chache sana mtu anaweza asipate mambukizi na ndiyo maana wataalamu mbalimbali wa masuala ya afya wanashauri kujikinga kwa kuvaa kondomu,” alisema dokta Chale.

MAJIBU YA DIAMOND YAKOJE?

Ijumaa lilimvutia waya juzi Diamond ili kutaka kujua anazungumziaje ishu hiyo na kama atakuwa tayari kuanika majibu ya vipimo vyake lakini simu yake ilikuwa haipatikani. Hata hivyo, mtu wa karibu na Diamond alieleza kuwa kwa wakati huo msanii huyo alikuwa safarini hivyo huenda ndiyo sababu ya kutompata kwa urahisi.

 

TUJIELIMISHE

Kama jamii suala la unyanyapaa ni la kupingwa na kila mtu, kwani haifai hata kidogo kunyoosheana vidole katika suala la Ukimwi kwani kufanya hivyo kunachangia kulikuza tatizo. Ifahamike pia kwamba mtu kuambukizwa Ukimwi hakutokani na wingi wa wapenzi alionao mtu bali kupuuza kutumia kinga katika kila tendo la ndoa, jambo ambalo kila mmoja anatakiwa kuwa na umakini nalo ili kulipiga vita gonjwa hilo.

STORI: MWANDISHI WETU, IJUMAA

Comments are closed.