Makachero Wa Nabi Wawamaliza Waarabu Fainali ya Kombe la Shirikisho
KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi ameshusha pumzi kuelekea katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger baada ya makachero wake kunasa mikanda ya mechi muhimu za wapinzani kabla ya mchezo huo.
Nabi ambaye amekuwa na msimu mzuri na Yanga kutokana na kufanikiwa kuingia fainali katika mashindano makubwa mawili tofauti, amezinasa video kuelekea katika mchezo wa kwanza wa hatua ya fainali unaotarajia kupigwa Jumapili hii ya Mei 28, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar kabla ya mchezo wa marudiano utakaopigwa Juni 3, mwaka huu.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo zinaeleza kocha huyo sasa amekuwa na uhakika mkubwa wa kuweza kuwamaliza wapinzani wake kutokana na kufanikiwa kunasa baadhi ya mikanda ya mechi muhimu za wapinzani wake ambazo zitamsaidia kuweza kupata matokeo katika mchezo wao ujao.
“Ni kweli kocha amefanikiwa kupata mikanda ya mechi muhimu za wapinzani kuelekea mchezo wa fainali kwa sababu alikuwa anataka kujua wanacheza kutumia mpango gani hasa wakiwa ugenini maana hata mchezo wa mwisho na Asec walikuwa tofauti sana.
“Lakini kwa sasa kila kitu kwa makachero walioagizwa wameweza kufanikisha hali iliyomfanya kocha kuwa na matumaini makubwa ya ubingwa kwa sababu tayari wameshafanyia kazi karibu mikanda yote,” alisema mtoa taarifa.
Championi Jumatano lilipomtafuta Nabi alisema kuwa: “Mechi itakuwa ya ushindani mkubwa nahitaji kuwafatilia wapinzani wetu jinsi wanavyocheza wanapokuwa ugenini na nyumbani, hii ni fainali itakuwa mechi ya ushindani mkubwa, tunatakiwa kuwafahamu wapinzani wetu vizuri.”
Stori na Ibrahim Mussa