The House of Favourite Newspapers

Makambo Mtu Mbayaaaa! Yanga Yafikisha Pointi 50

Straika Mkongomani, Heritier Makambo (katikati) akifanya yake.

HAKUNA namna yoyote ambayo timu yoyote ya Tanzania inaweza kuiondosha Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara mwaka huu wa 2018. Wenyewe wanasema tukutane mwakani.

Matokeo ya jana ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City yanamaanisha kwamba katika mechi 18 walizocheza msimu huu nyumbani na ugenini hawajapoteza mchezo,wakiwa wameshinda michezo 16 na kutoa sare mbili.

 

Kinachowapa kiburi zaidi Yanga, ni baada Azam kupoteza mchezo wake wa jana dhidi Mtibwa kwa kipigo cha mabao 2-0 ndani ya Uwanja wa Manungu. Hiyo inamaanisha kwamba Yanga ndiyo timu pekee ya Ligi Kuu, inayomaliza mwaka 2018 kesho bila kupoteza mchezo wowote. Mabao yaliyomaliza mchezo yalifungwa na straika Mkongomani, Heritier Makambo dakika ya 16 na 41 huku Idd Seleman akipachika dakika 23.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha pointi 50 huku Makambo akionyesha kuwa yeye ni mahiri kuliko Eliud Ambokile wa Mbeya City ambaye walikuwa wakichuana naye kwenye msimamo wa wafungaji. Eliud hakufunga jana na kubakiwa na mabao yake tisa, mwenzie Makambo akifikisha 11 na kupiga kifua akiwaonyesha mashabiki kwamba yeye ni tishio.

Mwaka 2018, unamalizika kesho Jumatatu na hakuna mechi nyingine ambazo zinaweza kuchezwa ndani ya muda huo kuitoa Yanga kileleni. Baadhi ya mashabiki mjini hapa jana walikuwa wakiimba ‘Happy new year’. Licha ya ukata waliokuwa nao ambao jana ulithibitika kwa mashabiki kutembeza vyombo maalumu vya kuchangishana uwanjani, lakini vilevile ndio waliotoa Sh.Milioni 9 zilizolipia usafiri wa ndege kufika Mbeya na kurudi.

Mbeya City walionekana kujiamini kwa kiasi kikubwa kipindi cha kwanza ingawa mabeki wao walionekana kufanya makosa ya wazi ambayo yalimkera kocha wao Nsanzurwimo Ramadhani. Kipindi cha pili katika dakika 20 za kwanza, wachezaji wa timu zote mbili walikuwa wakijiangusha hovyo huku mashabiki wa Mbeya City wakitaka Peter Mapunda aingizwe kuongeza kasi akaingizwa dakika 10 za mwisho kuchukua nafasi ya Eliud Ambokile aliyepata
maumivu makali baada ya kupigwa kiwiko na Japhary Mohammed.

 

Dakika hizo Mbeya City wakanyanyuliwa wachezaji wote wakapashe. Yanga wakamtoka Ibrahim Ajibu na kumuingiza Pius Buswita kulinda ushindi wao. Mchezo huo ulikuwa ni wa sita kwa Yanga kucheza na Mbeya City katika uwanja huo, huku Yanga ikiandika rekodi ya kushinda mechi tatu, sare mbili na kupoteza moja.

 

Baada ya mchezo huo Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera aliiambia Spoti Xtra kwamba aliwapa wachezaji wake shilingi laki moja na nusu kila mmoja kama ofa ya sikukuu baada ya kumfanyia kazi nzuri. “Hata kipigo cha Azam tumekifurahia kwa vile tunakwenda kukutana nao tukiwa na morali kubwa na tutawashinda,”alisema Zahera huku Nsanzurwimo akilaumu mabeki wake kwamba walitoa zawadi kwa Yanga.

STORI NA MUSA MATEJA

Comments are closed.