The House of Favourite Newspapers

Makonda aisisitiza GGML kuhakikisha CSR inabadilisha maisha ya wana-Geita

0

NA MWANDISHI WETU, ARUSHA

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ametoa wito kwa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kuhakikisha fedha zinazotolewa na kampuni hiyo kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii (CSR) zinagusa na kubadilisha maisha ya wananchi wa mkoa wa Geita na Tanzania kwa ujumla.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda (kushoto) na Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama na Mazingira wa GGML, Dk Kiva Mvungi (kulia) wakifurahia jambo katika banda la GGML wakati wa maonesho ya OSHA 2024 kwenye Viwanja vya General Tyres jijini Arusha. Katika Maonyesho ya OSHA 2023, Geita Gold Mining ilitambuliwa kama kampuni iliyofanya vizuri zaidi katika masuala ya afya na usalama kazini, na pia ilitunukiwa tuzo ya muonyeshaji bora kwa ujumla.

Mbali na kuipongeza GGML kwa kuja na tenolojia mbalimbali za uokoaji katika maonesho ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa kazi (OSHA) yanayoendelea kwenye viwanja vya General jijini Arusha, pia alieleza kuridhishwa na elimu inayotolewa kwa wananchi kuhusu masuala ya afya na usalama mahali pa kazi.

Makonda ambaye alitembelea banda la GGML katika maonesho hayo jana alisema mara nyingi maisha ya watu wa Geita hayafanani na utajiri uliopo katika mkoa huo.

“Mimi sioni aibu kuitwa tajiri,kwa sababu hilo ni jambo la

Kujivunia hivyo siwezi kujivunia umaskini ndio maana nataka ninyi Watanzania mliopo kwenye mgodi huu kuendelea kuwa chanzo cha mabadiliko ya watanzania wenzenu wanaozunguka mgodi huu,” alisema.

Aidha, Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama na Mazingira kutoka GGML, Dk Kiva Mvungi alimpatia maelezo Makonda kwamba mpango wa CSR wa mwaka huu ni mwendelezo wa mipango ya awali unaolenga kujumuisha maendeleo yaliyofikiwa na GGML hadi sasa katika maeneo ya mazingira, miundombinu, afya, elimu na biashara ndogondogo na za kati (SMEs) katika jamii ya mwenyeji wa Geita.

Dk. Kiva alitoa mfano kuwa mwaka jana GGML imesaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) na wenyeji wake Halmashauri ya Mji Geita, Wilaya ya Geita pamoja na Halmashauri za jirani za wilaya za Chato, Bukombe na Mbogwe kutekeleza Mpango wa Uwajibikaji wake kwa Jamii (CSR) kwa mwaka 2022/2023 wenye thamani ya Sh bilioni 19.

“Jumla ya Sh bilioni 9.8 zilitengwa kwa ajili ya Halmashauri ya Mji wa Geita ambapo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, bajeti ya Sh bilioni 8.6 ilitengwa.

“Uwepo wa GGML katika mkoa wa Geita umeonyesha matokeo chanya katika sekta ya elimu baada ya kampuni hiyo kujenga miundombinu zaidi ya 1800 ya shule za msingi na sekondari katika wilaya ya Geita yenye halmashauri mbili za Geita mji na ile ya wilaya ya Geita,” alisema.

Alisema miundombinu hiyo imetokana na utekelezaji wa mabadiliko ya sheria ya madini ya mwaka 2017 ambapo GGML imekuwa ikiandaa mpango wa huduma kwa jamii kwa kushirikiana na halmashauri husika huku kila mwaka hutenga kiasi cha Sh 9.2 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Mbali na miradi ya elimu, Dk. Kiva alisema GGML kupitia fedha za CSR walitenga fedha kwa ajili ya miradi ya mazingira ambapo kiasi cha Sh700 milioni zinatumika.

“Ipo pia miradi ya kimkakati ukiwemo ule wa ufugaji wa samaki, miradi kwa kinamama na vijana pamoja na wasiojiweza ambapo zaidi ya Sh1.5 bilioni zinatumika.

Alisema miradi hiyo inaongeza thamani katika sekta mbalimba za kiuchumi na kuwapatia wananchi maendeleo.

Leave A Reply