The House of Favourite Newspapers

Makonda, Ukawa wananchi Dar wanawategemea

0

Paul-MakondaMkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda.

Nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuiona leo.

Baada ya kusema hayo niseme kwamba leo nitakuwa natoa ushauri wa bure kwa viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Utaniuliza kwa nini nimechagua Dar. Zipo sababu nyingi baadhi ni kwamba Dar es Salaam ni mji mkubwa wa kibiashara Tanzania. Pili jiji hili lina wakazi wengi kuliko mji wowote katika nchi yetu.

Lakini tatu ni kwamba lina mchanganyiko wa viongozi, Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda ni kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mameya watatu ni wa kutoka Ukawa yaani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuna Naibu Meya kutoka Chama cha Wananchi (CUF).

Meya wa Jiji ni Issaya Mwita kutoka Chadema, Meya wa Manispaa ya Kinondoni ni Boniface Kuyeko wa Chadema na Naibu Meya wake ni Jumanne Amir wa CUF, Meya wa Manispaa ya Ilala ni Charles Kuyeko wa Chadema, Naibu wake ni Omary Kimbilamoto wa CUF.

Hakuna ubishi kwamba katika manispaa hizo madiwani wa Ukawa ni wengi kuliko wale wa chama tawala.
Ukifikiria sana utagundua kuwa ndiyo maana Rais Dk. John Pombe Magufuli aliamua kuhimiza kwamba iachiwe demokrasia itawale katika uchaguzi wa meya baada ya baadhi ya wanachama wa chama tawala kufanya mbinu mbalimbali za kukwamisha uchaguzi wa meya wa jiji.

Rais Magufuli aliona mbali, kiukweli hakuna kingine cha kumshauri mkuu wetu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda isipokuwa aamue kushirikiana katika serikali yake na mameya hao wa Chadema kwa sababu katiba inaruhusu.
Naamini wote wana lengo moja la kuletea maendeleo Mkoa wa Dar es Salaam ili wakazi wake waweze kujivunia matunda ya uhuru wa nchi yetu.
Katika uongozi wa kila sehemu kuna madaraja yake ya uongozi na hakuna ubishi kwamba katika mkoa kiserikali Makonda ndiye kinara.

Lakini pia hakuna ubishi kwamba katika mipango ya maendeleo kimanispaa, madiwani ndiyo wanaopitisha bajeti ya matumizi yote ya maendeleo katika eneo husika.
Kwa hali hiyo kila upande unategemeana katika kuleta maendeleo.
Kutokana na hayo wananchi hatutegemei kusikia kauli za mipasho dhidi ya vyama vya siasa vilivyotoa viongozi, yaani CCM, Chadema na CUF.

Makonda akitaka kufanikiwa ni lazima ashikamane na viongozi waliowekwa na wananchi bila kujali itikadi zao na wala asiwadhihaki.
Nilifurahishwa na kauli ya Isaya Mwita, Meya wa Jiji la Dar es Salaam ambaye ametangazia umma kwamba licha ya uanachama wake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), atafanya kazi bila kujali itikadi za vyama vya siasa.

Niwaambie viongozi wangu hawa kwamba wananchi wana matatizo mengi na wanahitaji kutatuliwa.
Nilifurahi kuona Makonda akimuagiza Kamishna Simon Sirro, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam akimtaka ashughulikie matatizo ya waendesha bodaboda.
Hiyo ni mifano tu lakini naamini viongozi wote mkishikamana mtaipeleka Dar kwenye neema, kila mmoja atambue kuwa wananchi wanawategemea.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Leave A Reply