The House of Favourite Newspapers

Makundi ya Panya Road Yaibukia Mkoani Katavi, Jeshi la Polisi Laingilia Kati na Kuwakamata 15

0
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, ACP Ali Makame Hamad

 

Baada ya kudhibitiwa kwa kiasi kikubwa jijini Dar es Salaam, makundi ya vijana wadogo wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu ikiwemo uporaji, ukabaji na uvunjaji wa nyumba maarufu kama Panya Road, wameibukia mkoani Katavi.

 

Kwa muwa wa wiki kadhaa sasa, mkoa wa Katavi umekumbwa na makundi ya vijana wadogo, baadhi yao wakiwa na umri wa chini ya miaka 18 ambao wamekuwa wakiwajeruhi raia na kuwapora mali zao nyakati za usiku.

 

Kutokana na kukithiri kwa matukio hayo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi kupitia misako na doria limefanikiwa kuwakamata vijana 15 na tayari wamefikishwa mahakamani huku baadhi yao wakihukumiwa kulipa faini ya shilingi elfu hamsini.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, ACP Ali Makame Hamad, akitoa ripoti kwa wanahabari kuhusu mafanikio ya jeshi hilo kwa kipindi cha mwezi Februari hadi Machi, ameyataja makundi hayo tishio kuwa yanajiita kwa majina ya Damu Chafu, Manyigu na Kaburi Wazi.

 

Aidha, ACP Makame amesema chanzo cha kuzuka kwa makundi hayo ni malezi mabovu ya wazazi kushindwa kuwadhibiti na kuwafundisha maadili mema.

 

Amewataka wazazi na walezi mkoani Katavi kuwasimamia watoto wao vizuri kwa kuwa umri wao ni wa kuwa shuleni na ametoa onyo kuwa jeshi litaendelea kuwachukulia hatua wazazi wa watoto watakaokamatwa ikiwemo kuwafikisha mahakamani.

 

Kadhalika, ameyataja mafanikio mengine yaliyopatikana kwa kipindi hicho ni kukamata watuhumiwa 14 wa makosa mbalimbali ya kukutwa na mali za wizi.

 

Pia Jeshi la Polisi mkoa wa Katavi limewafikisha mahakamani watu wawili Omary Lukele (56) na Denis Devis (44) wote wakazi wa Kigoma wakiwa na vipande sita vya meno ya Tembo ikiwemo kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa 10 baada ya kukamatwa na silaha 7 aina ya gobole.

Leave A Reply