The House of Favourite Newspapers

MAMA AMCHINJA MWANAYE LIVE NA KUMCHEMSHA SUPU UNYAMA ULIOJE?

NI unyama ulioje! Mtu kumuua mtoto wa kumzaa mwenyewe kisha kuchukua kisu na kumkatakata vipande vidogovidogo kisha nyama yake kuitia kwenye sufuria na kuichemsha supu. 

 

Achana na tukio hilo la mwanamke aitwaye Happines Shadrack mkazi wa Kijiji cha Buligi, Kata ya Senga, mkoani Geita, kumuua mwanaye wa mwaka mmoja kinyama; kuna watu wengine nane mkoani Ruvuma nao wamenaswa na mtoto wa mwaka moja na miezi tisa kwenye tambiko; Uwazi linakusimulia kwa kina matukio haya ya kusikitisha.

 

TUANZE NA MAMA KUUA MWANAYE

Uwazi lilifika eneo la tukio kulikofanyika mauaji hayo na kukuta huzuni imetanda miongoni mwa jamii huku kila mmoja akishidwa kuamini kilichotokea. Damu na vipande vya nyama za mtoto aliyeitwa Martha Yakobo zilikuwa zimetapakaa chumbani jambo lililowafanya watu wengi kushindwa kujizuia na kuangua kilio kama si kumuombolezea mtoto huyo aliyeuawa kinyama.

 

Kisa kinachotajwa na majirani kinadaiwa kuwa huenda Happines wakati akifanya tukio hilo alikuwa ameshikwa na ugonjwa wa akili ambao alitajwa kuugua siku za nyuma. Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Kamishina Msaidizi, ACP Dismas Kisusi amesema: “Hapana, bado mtuhumiwa tunamshikilia kwa uchunguzi zaidi, kwani mpaka tujiridhishe kama kweli ana tatizo la akili.”

 

MTOTO ALIVYOUAWA

Dada wa mtoto aliyeuawa aitwaye Doris Yakobo ambaye naye bado mdogo ambapo jina lake linahifadhiwa alisema: “Wakati mama yake akiingia chumbani alikokuwa amelazwa mdogo wake alimuona lakini hakuwa na mashaka yoyote.” Inaelezwa kuwa, mtoto huyo majira ya saa saba mchana alipelekwa kwenda kulala chumbani kwa bibi yake aitwaye Ruth Shadrack na kuwafanya watu wengine waendelee na shughuli zao.

 

“Baadaye nilimuona mama anaokota kuni, nikamuuliza anataka kupika nini? Akaniambia kuwa anachemsha maji. “Basi mimi nikaendelea kucheza nje, baadaye nikarudi na kukuta damu ndani na sufuria la nyama likiwa jikoni,” alisimulia Doris.

MWENYEKITI WA MTAA ANENA

Mwenyekiti wa Kitongoji cha CCM Buligi, aitwaye Manyoni F. Manyoni alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema ni la kutisha. “Eneo la tukio lilikuwa linatisha na kusikitisha, ilikuwa vigumu kuamini,” alisema Manyoni.

 

NYAMA ZAZIKWA

Baada ya kufanyika kwa uchunguzi wanakijiji walikusanyika na kuchukua vipande vya nyama za marehemu Martha na kwenda kuvizika na hivyo kuhitimisha safari ya maisha ya mwaka mmoja na miezi tisa hapa duniani ya mtoto huyo.

 

NANE WASHIKWA RUVUMA

Wakati Happiness akishikiliwa kwa mauaji ya wanaye watu, wengine nane wakiwa na mtoto mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi tisa wanaswa na Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma wakiwa kwenye tambiko juu ya Mlima Mgwijima uliopo Minanzini Wilaya ya Namtumbo.

 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, ACP Simon Maigwa, alilitaja tukio hilo kuwa lilitokea Juni 17, mwaka huu. Kamanda Maigwa aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Fredrick Ngalibhenaye (44), Oliva Kaduma (33), Beatus Lutenge (53), Samola Raphael (32) ambao wote ni wakazi wa Makambako, mkoani Njombe.

 

Aliwataja watuhumiwa wengine ni Rajab Yasini (38), Nasibu Issa (25), Omary Salumu (50) na Faraji Panjapi (41) ambaye ni mganga wa jadi pia ni wakazi wa Kijiji cha Minazini wilayani Namtumbo.

 

VIFAA WALIVYOKUTWA NAVYO

Alisema kuwa watuhumiwa hao walikutwa wakiwa na mbuzi mweusi, kuku mweusi, kuku mweupe, kigoda cheusi ,vitambaa vyeusi na vyeupe vikiwa na shanga pamoja na mikuki minne vitu ambayo vinadaiwa viliandaliwa kwa ajili ya kufanyia vitendo hivyo vinavyodaiwa ni vya kishirikina .

 

MTOTO WA NINI ENEO LA TAMBIKO?

Mara baada ya watuhumiwa hao kunaswa, Jeshi la Polisi lilimuuliza mama wa mtoto huyo ambaye alikamatwa eneo la tukio aitwaye Oliva kwa nini alikwenda kutambika akiwa na mtoto mdogo ambapo alijitetea kwa kusema: “Nilikuja kutambika kwa sababu nilioteshwa njozi kuwa nije huku kufanya tambiko katika chimbuko walikotokea wazazi wangu katika mlima huu ili niweze kutatua matatizo yangu.”

 

Hata hivyo, alishindwa kubainisha wazi ni aina gani ya matatizo ambayo alitaka kuyatatua kwa tambiko jambo ambalo liliwapa mashaka polisi kiasi cha kuhisi kuwa watu hao walikuwa na lengo baya kwa mtoto waliyekuwa naye. “Kumekuwa a matukio mengi sana ya watoto kupotea, wengine kuuawa na kuchunwa ngozi katika maeneo yanayozunguka mkoa wetu.

 

“Jeshi la Polisi tunatilia mashaka kufuatia watuhumiwa hao kuwa na mtoto mdogo kisha kwenda kufanya vitendo hivyo vya kishirikina jambo ambalo lingeweza kusababishia madhara kwa mtoto huyo kwa vitendo hivyo,” alisema Kamanda Maigwa.

 

MATUKIO YALAANIWA KILA KONA

Matukio ya kishirikina na hasa mauaji ya watoto yamekuwa yakilaaniwa kila kona ya nchi na kwamba jamii imeaswa kuachana nayo kwa sababu hayana faida na yanaharibu sifa njema ya taifa letu.

 

Hata hivyo, baada ya watu hao nane kunaswa wakiwa na mtoto huyo baadhi ya watu waliliomba Jeshi la Polisi lililo chini ya Inspekta Jenerali Simon Sirro, kufanya uchunguzi wa kina na kuwafikisha watuhumiwa hao kwenye vyombo vya sheria.

 

Wakati huohuo, wamesema uchunguzi wa kitabibu ufanyike ili mwanamke anayetajwa kumuua mwanaye na kumchemsha supu uthibitishe kama kweli ni mgonjwa wa akili au la ili naye achukuliwe hatua za kisheria. Mara kadhaa, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amekuwa akisisitiza kuwa suala la ulinzi wa watoto ni la jamii nzima.

Comments are closed.