Mama Diamond amkaribisha Wema

Image00024

Wema Sepetu ‘Madam’ akiwa na mama mzazi wa Diamond, Sanura Kassim ‘Sandra’.

Brighton Masalu NA IMELDA MTEMA
MAMBO yamekuwa mambo! Siku chache baada ya mzazi mwenza wa mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ kutimka Bongo na kuelekea kwake nchini Afrika Kusini ‘Sauz’, mama mzazi wa Diamond, Sanura Kassim ‘Sandra’ ameibuka na kusema hana kinyongo na mpenzi wa zamani wa mwanaye, Wema Sepetu ‘Madam’ na anamkaribisha nyumbani kwao muda wowote, Risasi Jumamosi lina ‘full’ stori.

Tangu Zari aondoke Bongo, imeelezwa kuwa, familia ya Diamond chini ya mama huyo mzaa chema, imempotezea ‘mazima’ Zari na endapo Wema ataamua kurudi nyumbani, atapokelewa kwa mikono miwili.

MWANAFAMILIA AVUJISHA UBUYU
Mmoja wa wanafamilia wa Diamond ambaye hakupenda jina lake lichorwe gazetini, mwishoni mwa wiki iliyopita, kwa zaidi ya dakika 34, alizungumza na mwanahabari wetu na kudai kutokana na ‘gepu’ lililoachwa na Zari, kuna uwezekano mkubwa Wema akarudisha majeshi kwa Diamond na mambo yakawa kama zamani kwani hana kipingamizi.

“Unajua Zari hawezi kurudi, mtu pekee ambaye tuna imani naye na tuliishi naye vizuri ni Wema, yaani hata kama ni kumshawishi, tutafanya hivyo ili arudi kwenye kiti chake kilichokaliwa na Zari kwa muda.

wemanadiamond (1)

Mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ akiwa na aliyekuwa mpenzi wake Wema Sepetu.

MAMA DIAMOND SASA
Baada ya kuzipata habari hizo, mwandishi wetu alimtafuta mama Diamond kwa njia ya simu, ambapo baada ya kuulizwa juu ya madai hayo, awali mama huyo ambaye hapo zamani alisifika kwa ustaarabu na upole, ‘alifyatuka’ kwa maneno makali na kumtaka mwanahabari wetu kutofuatilia maisha ya familia yake.

“Kwani, bila familia yangu huwezi kufanya kazi zako? Mbona hivyo lakini? Au na wewe uje kuishi huku basi kama unaona sisi tunafaidi,” alibwatuka mama Diamond.

AMKUBALI WEMA, AMKARIBISHA NYUMBANI
Baada ya mwandishi wetu kumbana mama huyo na kumtaka arudi kwenye hoja ya msingi ya kuzungumzia aliyekuwa mchumba wa mwanaye (Wema), bi mkubwa huyo alisema hana kinyongo naye na anamkaribisha nyumbani kwa Diamond, Madale-Tegeta, Dar (anapoishi pia mama huyo) muda wowote kuanzia sasa na yuko tayari kuona akiwa karibu na mwanaye, Diamond.

“Sijawahi kugombana na Wema, ni wao tu walishindwana kidogo katika mapenzi yao. Lakini mimi namkaribisha hata leo. Hapa ni kama kwake. Ni binti mwema na furaha yangu ni kumuona akiwa karibu na mwanangu hata kama ni maisha ya kawaida tu,” alisema mama Diamond na kukata simu kabla ya kuizima kabisa (mwandishi alimtafuta tena).

IMG_6274WEMA ANASEMAJE?
Awali jitihada za kumpata Wema ili aweze kuzungumza kama yupo tayari kurudisha moyo wake nyuma na kurejea kwenye himaya ya Diamond hazikuzaa matunda kufuatia mrembo huyo kuwa bize na kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na simu yake kutopokelewa.

Hata hivyo, muda mfupi kabla ya kwenda mitamboni, Wema alipatikana ambapo alitoa la moyoni juu ya ishu hiyo:
“Siwezi kurudia kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume kutoka familia ya Kiswahili.”

KUMBUKUMBU MUHIMU
Mara kadhaa, Wema alishawahi kuulizwa kupitia magazeti tofauti Pendwa ya Global Publishers (Ijumaa Wikienda, Uwazi, Ijumaa ‘Kubwa’, Amani, Risasi Jumatano, Risasi Jumamosi) kama anaweza kurudiana na Diamond, akadai hayupo tayari hata iweje!

Loading...

Toa comment