The House of Favourite Newspapers

MAMBO 16 MUHIMU YAMPASAYO MJAMZITO KUYAFAHAMU

KUNA mambo muhimu 16 ambayo mama mjamzito hupaswa kuyazingatia kwa afya yake wakati wote wa ujauzito wake wa miezi tisa. Leo tutaeleza kwa ufupi mambo hayo kwa faida ya wanawake wote.

1.Wakati wa ujauzito, unaweza kusikia uchovu mkubwa au usingizi. Mara nyingi uchovu huu upo katika miezi mitatu ya awali.

  1. Kama mjamzito, jitahidi kupumzika na kuweka miguu juu kila unapoweza na ulale na mito kati ya miguu yako na ulale mapema.
  2. Kizunguzungu wakati wa ujauzito ni jambo la kawaida na kinaweza kusababishwa na msukumo wa damu (presha) kushuka, hivyo ni vema kuwa makini na ikibidi muone daktari kikizidi.
  3. Kizunguzungu wakati wa ujauzito huweza kusababishwa na sukari katika damu kushuka, upungufu wa madini chuma mwilini, upungufu wa maji mwilini.
  4. Kusimama ghafla pia huweza kusababisha mama mjamzito akasikia kizunguzungu. Inashauriwa kama mjamzito, usimame taratibu.
  5. Mjamzito anaweza kupata kisukari kinachosababishwa na ujauzito. Hujitokeza katika miezi ya nne mpaka sita.
  6. Kwa akina mama wajawazito maji ni muhimu kuunda kondo ya nyuma na kuboresha mfuko wa uzazi ili mtoto apate virutubisho muhimu.
  7. Mstari mweusi upo mwilini mwa mama mjamzito kwenye tumbo katika hali ya kawaida kabla ya ujauzito lakini hauonekani sana akiwa na mimba, mstari huo huitwa Linea Nigra.
  8. Uvutaji sigara wakati wa ujauzito huweza kusababisha mtoto kuzaliwa kabla ya wakati wake (mtoto njiti) au kuzaliwa na uzito mdogo, usivute sigara ukiwa na ujauzito.
  9. Uvutaji sigara wakati na baada ya ujauzito pia huweza kusababisha mtoto kufariki ghafla. Sigara ina kemikali zaidi ya 4,000. Lakini pia unywaji wa pombe ukiwa na ujauzito ni hatari.
  10. Nini husababisha mishipa kutuna wakati wa ujauzito? Usiogope ni kawaida kwa sababu kadiri mtoto anavyokua, presha huongezeka katika mfuko wa uzazi na mishipa hutuna. Una uwezekano mkubwa zaidi wa mishipa ya damu kuvimba sana kama ni mjamzito na umebeba zaidi ya mtoto mmoja tumboni.
  11. Ni vyema kupumzika na kuweka miguu juu mara kwa mara wakati wa ujauzito ili kupunguza mishipa kuvimba sana.
  12. Je, wajua kuwa wakati wa ujauzito na hata baada ya kujifungua, akina mama huweza kupata mfadhaiko (postpartum depression)? Hili unapaswa kulijua.
  13. Ni muhimu kwa familia kuwa makini na kutomwacha mama mjamzito au mwenye mtoto mchanga ambaye ana huzuni au msongo wa mawazo peke yake nyumbani bila msaada wa kitaalam.
  14. Takriban asilimia 25 ya akina mama hutokwa na damu kidogo ukeni wakati wa ujauzito katika miezi mitatu ya mwanzo, ikizidi hapo muone daktari.
  15. Ukitokwa na damu nyingi na maumivu ya tumbo wakati wowote wa ujauzito, kamwone mtaalam mara moja!

USHAURI MUHIMU

Mambo hayo 16 ni muhimu kwa mjamzito au anayemhudumia mjamzito kuyafahamu na tatizo lolote kati ya haya likitokea haraka sana muone mtaalamu wa afya ili akuchunguze na kukupa dawa stahiki kama hapana budi.

Comments are closed.