The House of Favourite Newspapers

Mambo 9 kwa binti anayefaa kuwa hausigeli wako!

0

house girlKwa maisha ya sasa, ni familia chache sana ambazo hazina msichana wa kusaidia kazi za ndani ‘hausigeli’. Hili limewafanya wasichana hao wawe lulu hasa maeneo ya mjini.

Hata hivyo, wapo ambao wamekuwa wakiwanyanyasa sana wasichana hao licha ya msaada mkubwa wanaoutoa kwa jamii. Wapo wanaowatukana, kuwalipa mshahara kidogo au wakati mwingine kutowalipa kabisa, jambo ambalo siyo zuri hata kidogo.

Hivi mtu ambaye anakulelea watoto wako, anakusaidia kupika, kufua, kuosha vyombo, kusafisha nyumba na kazi nyingine za ndani unaanzaje kumfanyia mambo ya ajabu kama hayo? Mimi nadhani ni wakati wa kubadilika kwa wale wanaowanyanyasa mahausigeli wao.

Baada ya kusema hayo, sasa nigeukie kwenye kiini cha mada hii. Nazungumzia mambo 9 kwa msichana anayefaa kuwa hausigeli wako.

Ujue anakotoka

Hata kama una shida vipi, hakikisha binti unayeletewa unajua anatoka wapi na ikiwezekana ufanye mawasiliano na ndugu zake, waridhie wewe kuishi naye.

Hii ya kuokotaokota inaweza kukuletea shida baadaye kwani huenda msichana huyo katoroka kwao. Shida zaidi itakuwa pale akipata matatizo, akiumwa au hata akifa. Unadhani utaanzia wapi?

Mchapakazi

Wapo mabinti wengine wanatafuta kazi za ndani lakini si wachapakazi. Ukijichanganya ukachukua binti ambaye amepitia kwenye usistaduu, maisha yakamchenga, akaamua kutafuta kazi na wewe ukamchukua kama hausigeli wako, utajuta.

Ajue kuelekezwa na kufokewa

Wakati mwingine binti wa kazi anaweza kufanya makosa na ukamuelekeza au kumfokea kama unavyomfokea mwanao.

Unayemchukua ajue kuwa kuna wakati utalazimika kumuelekeza kwa ukali pale atakapokuwa amekwenda kinyume na asiwe mtu wa kuchukulia kwamba anafokewa kwa kuwa hapendwi.

Asiwe na tamaa

Binti unayemchukua hakikisha hana tamaa za kupenda mambo makubwa. Aridhike na kipato anachopata, maisha anayoishi na asiwe mtu wa kushawishika kirahisi.

Akuchukulie kama mzazi

Unapomchukua msichana kutoka kwenye familia nyingine ili aje kukusaidia kazi za ndani, akuchukulie wewe kama mzazi wako na wewe umchukulie kama mwanao.

Umri wake

Wapo ambao wanakosea kwa kuchukua mabinti wenye umri mdogo na kujikuta wanaingia kwenye mikono ya sheria. Hausigeli hatakiwi kuwa mtoto, umri unaojulikana ni kuanzia miaka 18 na kuendelea.

Hii itakufanya uwe salama lakini pia kwa umri huo atakuwa ni msichana mwenye uelewa ambaye hawezi kufanya mambo ya kitoto.

Msikivu

Sifa nyingine ya hausigeli ni usikivu. Awe ni binti ambaye akielekezwa anaelewa haraka na anafuata yale ambayo unamwambia. Ajue majukumu yake, atambue ni yapi anayotakiwa kuyafanya ili amfanye ‘bosi’ wake afurahi na ajue amepata mtu sahihi.

IJUE Afya yake

Wapo waliochukua wafanyakazi wa ndani ambao baada ya siku waligundua wana matatizo ya kiafya. Hii ni hatari, unapomchukua binti wa watu, ni vyema ukajua kama ana tatizo lolote.

Kwa mfano, huenda ana mashetani, ana ugonjwa wa kuanguka, pumu, presha au matatizo mengine. Ukijua hivyo itakuwa ni rahisi sana kukabiliana na hali hiyo pale itakapojitokeza.

Upendo na uvumilivu

Msichana wa kazi lazima awe na upendo hasa kwa kuwa, nyumbani watakuja ndugu, jamaa na marafiki wanaostahili kukirimiwa Ipasavyo. Yeye anatakiwa kuwa mkarimu.

Pia familia nyingine zina watoto watundu sana, ni vyema akawa mtu wa kuvumilia vurugu za watoto na kujua njia sahihi ya kuishi nao. Asiwe mwepesi wa kupiga.

Leave A Reply