The House of Favourite Newspapers

Mambo Makubwa 16 Aliyofanya Rais JPM Yakaitisa Nchi – Video

LICHA ya kutimiza miaka minne madarakani, kasi, weledi na ufanisi katika utendaji wa Rais Dk John Magufuli ‘JPM’ umedhihirisha mafanikio ya uongozi wake na kuwaacha solemba waliofikiri ari yake ni sawa na nguvu ya soda.

Kama ilivyokuwa kwenye matoleo mawili ya Gazeti la Uwazi na Risasi Mchanganyiko, leo tunaendelea na sehemu ya tatu na ya mwisho ya makala haya.

 

10: KODI

Katika kuleta mapinduzi ya kikodi, Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kuongeza ukusanyaji mapato, kutoka shilingi trilioni 9.9 wakati wa Awamu ya Nne hadi shilingi trilioni 14 kwa mwaka.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yenye jukumu la kukadiria, kukusanya na kuhasibu mapato ya Serikali, ni miongoni mwa taasisi za umma ambazo zimefanikiwa kutekeleza malengo ya JPM kwa vitendo katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuleta maendeleo.

 

Hilo linadhihirishwa na ukweli kuwa Serikali katika kipindi cha miaka mitatu, imefanikiwa kuongeza makusanyo ya mapato kutoka wastani wa Sh bilioni 850 kwa mwezi, mwaka 2015 hadi wastani wa Sh trilioni 1.3 kwa mwezi kwa sasa huku TRA ikiendelea kuongeza ukusanyaji wa mapato.

Mwaka 2015/16 makusanyo yalikuwa Sh trilioni 12.5, mwaka 2016/17 yaliongezeka hadi kufikia Sh trilioni 14.4 na mwaka 2017/18 yaliongezeka hadi Sh trilioni 15.5. Mapato yote yaliyokusanywa kwa miaka mitatu mfululizo ni Sh trilioni 42.4.

 

Tangu TRA ilipoanza kufanya kazi Julai Mosi, 1996, mapema mwezi huu imevunja rekodi kwa kukusanya Sh trilioni 1.76 kwa Septemba, 2019.

Makusanyo haya ni sawa na ufanisi wa asilimia 97.2 ya lengo la TRA kukusanya Sh trilioni 1.81 iliyojiwekea mamlaka hiyo. Yakilinganishwa na Septemba 2018, makusanyo hayo yameongezeka kwa asilimia 29.18, hivyo kuzidi ufanisi wa miezi yote ya robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha.

 

Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Edwin Mhede alisema makusanyo haya ni kiashiria wananchi wameelewa, wamekubali na kuitikia wito wa Serikali kuchangia maendeleo ya Taifa.

Ongezeko hili la ukusanyaji mapato ni hatua kubwa nchini ambalo kwa kiwango kikubwa limechangiwa na kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi na umma kumwelewa Rais, hivyo kujitoa kwa dhati kumuunga mkono.

 

11: USIMAMIZI WA RASILIMALI

Usimamizi thabiti wa rasilimali za Taifa letu ni miongoni mwa mambo ambayo Rais Magufuli amefanikiwa kwa kuwa hata yeye binafsi husema Tanzania si nchi maskini.

Kutokana na hali hiyo, amefanikiwa kushinikiza marekebisho mapya ya Sheria ya Kodi ya Madini na kuiamuru kampuni ya kuchimba madini Barrick kuafiki marekebisho hayo ambayo pamoja na mambo mengine yameifutilia mbali Acacia na kuundwa kampuni nyingine ya Twiga Minning kwa ubia wa Serikali na Barrick.

 

Itakumbukwa hayo yote yalikuja baada ya Rais Magufuli kuunda tume za mabingwa na wanasheria waliobobea katika mambo ya madini, ambayo ilichunguza makontena 77 makinikia ambayo yaligundulika kuwa na kiasi kikubwa cha dhahabu, shaba, zinki, cobalt, manganizi na fedha.

 

12: MIGOGORO YA ARDHI

Migogoro ya ardhi ni mojawapo ya mambo ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kuitokomeza. Migogoro hiyo ilikuwa imeshamiri katika Mikoa ya Morogoro na Manyara, ilhali baadhi ya vijiji ambavyo vilikuwa vimepakana na mapori tengefu, hifadhi za taifa nako kukiwaka moto.

Septemba mwaka huu, Waziri mkuu, Kassim Majaliwa alitangaza kuwa Serikali imefuta mapori tengefu 12 ambayo sasa yataneemesha vijiji zaidi ya 900.

 

Aidha, uteuzi wa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi uliofanywa na Rais Magufuli, ulidhihirisha kuwa migogoro hii imepata muarobaini baada ya waziri huyo kutekeleza bila kuchoka maelekezo ya Rais kuhusu utatuzi wa migogoro hiyo.

 

Utatuzi huo umehusisha pia kupima ardhi na kuirasimisha na kuigeuza kuwa mitaji iliyoandikishwa na kuwawezesha wamiliki wake kuitumia ardhi yao kama dhamana ya kupata mikopo kutoka katika taasisi mbalimbali za fedha.

Mfano katika mwaka wa fedha wa 2016/17 Wizara iliandaa jumla ya hatimiliki za ardhi 400,000 na kutoa hatimiliki za kimila 57,000 hadi kufikia Mei 15, mwaka jana, Wizara imeshatoa hatimiliki za ardhi 33,979 na iliandaa uratibu wa hatimiliki za kimila 35,002.

 

13: NIDHAMU

Suala la nidhamu serikalini, sasa limepata mwarobaini kwani Rais Magufuli amefanikiwa kulirejesha ipasavyo. Watumishi wengi walikuwa wakifanya kazi kwa mazoea na kukiuka maadili ya kazi kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa pamoja na mambo mengine.

Ni dhahidi kuwa Rais Magufuli ameutafuna mfupa wa rushwa uliomlazimisha muasisi wa taifa hili, Hayati Mwalimu Julius Nyerere kuutungia kitabu kilichojulikana kama Uongozi na Hatima ya Tanzania, kinachozungumzia kwa ukali madhara ya rushwa na uongozi wa taifa letu akionesha kwa uchungu jinsi rushwa ilivyokuwa inautafuna uongozi na uchumi wetu.

 

Aidha, katika kurudisha nidhamu serikalini, pia alifanikiwa kutokomeza watumishi hewa ambao ulikuwa ni mfumo uliokuwa tayari umeota mizizi.

Hatua hiyo ya kuwabaini watumishi hewa waliokuwa wakiisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya fedha kila mwezi, nayo ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya kujivunia Serikali ya Awamu ya Tano. Zaidi ya watumishi 10,000 walikuwa wakilipwa mishahara na kupata mikopo kwenye taasisi mbalimbali za fedha hali iliyosababisha Serikali kupata hasara ya mamilioni ya fedha.

14: SAFARI ZA NJE

Itakumbukwa kuwa alipoingia Ikulu, Rais Magufuli alipiga marufuku safari holela za nje ya nchi zilizokuwa zikiigharimu nchi mabilioni ya fedha na kutoa masharti magumu kwa kiongozi wa umma anayetaka kusafiri nje ya nchi.

Magufuli alisema kazi wanazokwenda kufanya maofisa wa Serikali, zifanywe na mabalozi walioko huko hatua ambayo nayo iliwafurahisha wengi kutokana na ukweli kwamba safari hizo zilikuwa mzigo kwa Serikali.

 

Katika hotuba yake wakati akilizindua Bunge Novemba 20, 2015, Rais Magufuli alisema anafuta safari zote holela za nje kwa sababu zimekuwa zikiligharimu taifa mabilioni ya fedha ambayo yangeweza kusaidia shughuli za maendeleo kama kujenga barabara za lami za urefu wa kilomita 400, kuchimba visima vya maji safi na salama na kujenga zahanati au kununua dawa ili kuondoa kero wanayopata wananchi waendapo kwenye hospitali za umma.

Katika kutoa mfano, hadi sasa Rais Magufuli alisema amekataa mialiko zaidi ya 60 katika nchi za Ulaya, huku akisafiri ndani ya bara la Afrika pekee na ziara nyingi akizifanya ndani ya nchi kutatua kero za wananchi.

 

15: KUHAMIA DODOMA

Licha ya kuwa ni ndoto iliyodumu zaidi ya miaka 40 tangu enzi za uongozi wa Mwalimu Nyerere, Rais Magufuli amefanikiwa kuitimiza baada ya kuhamishia Serikali mkoani Dodoma ambapo zaidi ya watumishi 5, 136 wanatarajiwa kuhamia Dodoma mpaka mwishoni mwa mwaka huu. Hata hivyo, tayari Rais Magufuli ameshathibitisha kuhamia mkoani humo.

 

16: DAWA ZA KULEVYA

Matumizi ya dawa za kulevya ni tatizo lingine sugu lililokuwa linalitafuna taifa, kutokana na kukithiri kwa mapapa waliokuwa wanaogopwa kuguswa kwa kuwa waliikita mizizi katika biashara hiyo haramu.

Hata hivyo, Rais Magufuli alifanikiwa kuanzisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ambayo hadi sasa imefanikiwa kudhibiti tatizo hilo kwa kiasi kikubwa.

Kwa simulizi kwa njia ya sauti na picha, tembelea GlobalTV kwenye YouTube.

Makala: GABRIEL MUSHI, DAR

 

Comments are closed.