The House of Favourite Newspapers

Mambo Manne (4) Yanayoua Biashara Mpya

JARIDA la Bloomberg la Marekani limeeleza kuwa takribani biashara nane kati ya kumi ambazo huanzishwa, zinakufa baada ya muda wa miezi 18 (Mwaka mmoja na nusu). Takwimu hizi zinamaanisha kuwa katika kila watu kumi ambao wanaanzisha biashara leo, watu wanane kati yao biashara zao hazitakuwepo baada ya miezi 18.

 

Hii inaonyesha kuwa kuna umuhimu wa kujipanga na kujiandaa kama unapanga kuanzisha biashara ili usiwe mmoja wa wale ambao biashara zao hazitafanikiwa.Ili kujiepusha kuwa kati ya watu ambao biashara zao zinafaeli na hazifiki mbali, ni muhimu kujifunza sababu ambazo huwafanya watu wengi waishie njiani na washindwe kufanikiwa.

 

Mambo yanayofanya biashara zisifanikiwe

Moja ya mambo yanayofanya biashara zife ni kukosekana kwa utatifi kabla ya kuanzishwa kwake. Watu wengi huanzisha biashara bila kujipa muda wa kutosha kuchunguza aina ya biashara wanayotaka kufanya na kujua kama ni biashara ama la. Kosa mojawapo katika hatua hii ambalo wengi sana huwa wanalifanya ni kuangalia faida tu inayoweza kupatikana na kusahau kuwa kuna mambo mengine mengi sana yanapaswa kuzingatiwa.

 

Moja ya kitu ambacho unatakiwa kukifanyia utafiti ni mwendelezo wa biashara unayotaka kuifanya. Kuna watu wengi wanaparamia biashara za msimu na kuinginza pesa nyingi bila kujua kuwa wakati wanaingia kumbe ndio msimu wa mafanikio wa biashara hiyo ulikuwa ndio unaishia.

Ni kama vile kuanza kuagiza miamvuli makontena 100 wakati kumbe kipindi cha mvua ndio kinaishia. Si unakumbuka watu walivyovyamia mayai ya kwale? Leo yako wapi. Ni muhimu kuangalia asili ya biashara na kujua itadumu muda gani.

 

Pia ni muhimu sana kufanya utafiti wa upatikanaji wa bidhaa hasa kama unafanya biashara ambayo inahitaji malighafi. Kuna mtu niliwahi kukutana naye ambaye baada ya kusikia biashara fulani inalipa, akaenda akanunua mashine nyingi sana kwa pesa kubwa, lakini baada ya muda akakosa kabisa kupata malighafi na akasitisha uzalishaji hadi leo. Na wewe jiulize, hivi bidhaa hizi ninazoanza kuuza/ kuzalisha nina uhakika wa kuzipata kila nitakapohitaji.

 

Haya ni baadhi ya mambo ya kuangalia hata kabla haujaangalia kiwango cha mtaji ambacho unahitaji. Usiparamie biashara bila kufanya utafiti na kama unaona hauwezi kufanya utafiti mwenyewe unaweza kutafuta watu ambao wanaweza kukusaidia kiutalaamu zaidi.

Jambo lingine linalofanya biashara zikwame ni kutojiamini katika bidhaa unazouza/ huduma unayotoa. Changamoto mojawapo wanayopata watu wanaoanzisha biashara ni kuamini kuwa wanatakiwa waonewe huruma na watu watumie bidhaa zao kama njia ya kuwasapoti.

 

Hili ni kosa kubwa sana, unapoingiza sokoni bidhaa ama huduma yoyote ile, unatakiwa uingie kwa kujiamini na uonyeshe ubora na thamani ya kile unachokifanya bila woga. Watu wengi wameingia kwenye biashara na kwa sababu ya kutokujiamini wamejiwekea thamani ndogo sana kuliko hata ile ambayo wanayo (undervaluing) matokeo yake wamejikuta wanabakia chini na watu wanawachukulia kama watu ambao hawana thamani na wanashindwa hata kuongeza bei ya bidhaa zao wanazotoa.

 

Unapoamua kuwa mfanyabiashara kumbuka kuwa watu wanataka kuona kujiamini kwako katika biashara unayofanya, na kumbuka kuwa wakiona mfanyabiashara yoyote hajiamini basi na wao pia wataacha kuamini kwa kiwango kikubwa bidhaa ua huduma unayotoa. Je,unajiamini?

 

Kitu kingine kinachoua biashara nyingi ni wafanyabiashara kushindwa kujua wateja wao. Moja ya kitu ambacho kinaweza kukupotezea muda na fedha katika kukuza biashara yako ni pale unapojaribu kuwauzia watu ambao sio sahihi. Kumbuka kutangaza biashara yako kwa bidii na kwa gharama kubwa haitakupeleka unakotaka. Ni lazima uhakikishe kuwa unauza biashara yako kwa watu sahihi.

 

Hebu jiulize,umeshawahi kuona tangazo lolote la soda lenye wazee? Matangazo yao yote wamejaza vijana, kwa nini? Wazee wengi wako makini na vyakula hasa vyenye sukari na kampuni za soda wanajua kabisa hawa sio wateja wao wa kudumu. Wateja wao wengi ni vijana na ili kuwapata vijana wengi inawalazimu kutumia vijana zaidi kufanya matangazo yao.

 

Leo, jiulize hivi biashara yangu hii nawalenga watu wa namna gani? Inawezekana ukawalenga watu kutokana na umri wao, kutokana na jinsia zao au hata kutokana na kiwango chao cha kipato. Kitu muhimu sana kwenye kukuza biashara yako ni kuhakikisha kuwa lile kundi ambalo unalilenga unalifikia mara kwa mara bila kuchoka.

Usipoteze nguvu kubwa katika kujaribu kuwafikiwa watu ambao sio kundi la wateja wako. Kumbuka kuwa mikakati yako yote inatakiwa ilenge kuwafikia kundi la watu ambao ndio hasa wateja wako.

 

Pia kutumia pesa nyingi unapoanza biashara ni tatizo. Mtu anapotaka kutumia pesa nyingi sana hasa katika kujenga taswira badala ya kutumia pesa nyingi katika shughuli za uzalishaji, kuna shida. Unakuta mtu anaanza biashara tu na anataka kuwa na ofisi kubwa, ananunua samani za bei ghali kwa ajili ya ofisi, komputa za gharama kubwa sana.

 

Kumbuka unapoanza biashara yako, matumizi makubwa ya pesa yako yanatakiwa yaende zaidi katika vitu ambavyo vina uhusiano wa moja kwa moja na uzalishaji wa bidhaa au huduma. Ingawa mwonekano wa nje ni muhimu sana, hautakuwa na maana kama unajenga mwonekano mzuri ila kwenye uhalisia wa biashara haufanyi vizuri.

 

Kila unapotaka kutumia pesa wakati biashara yako ndio imeanza, ni lazima ujiulize-Je, matumizi ya pesa hii yanachangia vipi kuongeza uzalishaji au faida ya biashara ninayoifanya? Ukiona kama kila unachokifanya hakina uhusiano wa moja kwa moja na kuongeza uzalishaji ama faida kwenye biashara yako, hasa pale biashara inapokuwa imeanza, unatakiwa ujue kuwa maamuzi hayo yanaweza kuwa chanzo cha kuua biashara yako.

 

Je, unafikiri kuna sababu yoyote kati ya hizi zimechangia biashara yako kutofanya vizuri? Unaweza kunitumia ujumbe mfupi kupitia namba zangu kwa ushauri zaidi.

 

Joel Arthur Nanauka

YouTube: Joel Nanauka

Facebook: Joel Nanauka Page

Instagram: joel_Nanauka

[email protected]

0655-720 197.

Comments are closed.