The House of Favourite Newspapers

Mambo matatu kwa wenye wapenzi wachunaji!

0

Junge Frau zieht einem Mann Geld aus der Tasche.Dollar

Huko mtaani ambapo imekuwa ni kitu cha kawaida kumsikia msichana akitamba mbele za wasichana wenzake kwa kusema; ‘Mimi nina pedeshee wangu bwana, kila ninachotaka ananipa, anajua asiponipa namtosa tu, yaani namchuna kama sina akili nzuri.’

Si hivyo tu, wapo wanaume pia ambao ni kero kwa wapenzi wao, yaani wamegeuka wanaume kama mabinti kwa tabia zao za kutegemea kupewa kila kitu na wapenzi wao hata kama wanao uwezo wa kuvipata vitu hivyo kama watajishughulisha.

Unaweza kumsikia mwanaume akisema; ‘Aaah! Yule demu kazimika ile mbaya na mapigo yangu, kila ninachotaka ananipa, anajua akinizingua namtosa, hadi mshahara wake akipata ananigawia.’

Ninachotaka kusema leo ni kwamba, mapenzi ya kweli hayana uhusiano wowote na pesa, ukiona mpenzi wako anaweka pesa mbele na ukishindwa kumpatilizia anachokitaka anakasirika, jua penzi lake lina walakini, hakupendi bali anataka kukutumia kisha kukuacha.

Katika mapenzi hatukatai suala la kusaidiana, mpenzi wako akiwa na shida fulani akaomba umsaidie, kama unao uwezo msaidie na kama huna mueleze kwamba sina kisha muangalie jinsi gani mnaweza kusaidiana katika kutatua tatizo linalomkabili.
Itakuwa siyo busara kama utakuwa na tatizo lakini ukaona kwamba ukimweleza mpenzi wako ataona kwamba unamchuna. Wapenzi wanaopendana kwa dhati hawachunani bali wanasaidiana, na hili ni kwa pande zote mbili.

Kinachokera ni kutoishiwa na matatizo na wakati mwingine unakuta kuchuna kwingine ni kwa mambo ya starehe. Kwa mtu mwenye mapenzi ya kweli na wewe unadhania atakuchukuliaje? Ni wazi ataona huna malengo naye bali unataka kumtumia tu. Na akigundua hivyo ni rahisi sana kuamua kuachana na wewe.

Kimsingi ukiwa na mpenzi mwenye tabia ya kutaka kukuomba pesa kila wakati tena katika matumizi mengine ambayo siyo ya msingi, mbinu zifuatazo ni muhimu kuzifuata:

Kwanza; kama huna pesa wakati mpenzi wako anakuomba, mueleze wazi kuwa huna na kamwe usijaribu kutoa ahadi ambazo huenda ukashindwa kuzitimiza.

Pili; jambo la muhimu ambalo wanaume wengi wanalisahau ni kutokuwafundisha wapenzi wao wajibu wa kutoa. Utakuta kila kitu ananunua yeye, hata nauli ya basi analipa, wakati mpenzi wake ana kazi yake.

Ifike wakati kwa makusudi, mwanaume ampe majukumu ya kufanya mpenzi wake, hiyo itamsaidia mwanamke kujua namna pesa zinavyokuwa hazitoshi na akaweza kubana matumizi.

Tatu; kuna wanaume wengine tangu wanatongoza wanakuwa ni wafujaji wakubwa wa pesa kwa kutoa ofa na zawadi kibao. Hii inaweza kumjengea imani mpenzi wako kuwa wewe unazo.

Unachotakiwa mapema ni kudhibiti matumizi yako hata kama pesa zinakuwepo. Ifahamike kuwa kutoa hakushibishi uhitaji, kadiri unavyotoa ndivyo unavyoongeza mahitaji.

Mwisho naomba niseme kwamba, mapenzi ni kusaidiana. Jenga tabia ya kumsaidia mwenzako ili siku na wewe ukiwa na tatizo akusaidie.

Kitu unachotakiwa kukiepuka ni kuwa tegemezi hadi unakuwa kero. Kumbuka kumpiga mizinga mpenzi wako kila mara kunapunguza mapenzi hivyo epukana na tabia hiyo.

Leave A Reply