The House of Favourite Newspapers

Matatizo yanayomfanya mwanamke asipate ujauzito haraka (Infertility)

0

205061Kwa kawaida mwanamke anatakiwa apate ujauzito ndani ya mwaka mmoja baada tu ya kuolewa au kuanza mahusiano na yule ambaye tayari ana mtoto.

Tunategemea baada ya miaka miwili hadi mitatu baada ya kupata mtoto apate mwingine labda kama hajaamua yeye pamoja na mumewe. Ujauzito unapatikana baada ya kufanya tendo la ndoa kwa ukamilifu, yaani katika kipindi ambacho mwanamke anaweza kupata ujauzito wengine wanaita siku za hatari lakini kitaalam tunaita siku za ‘Ovulations’.

Suala hili pia linaangalia kwa upande wa pili wa mwanaume ambaye pia tunategemea ana uwezo huo wa kumpa mwanamke mimba kwa kuwa na mbegu zenye ubora na awe na nguvu za kutosha za kufanya tendo ili mwenzi wake apate ujauzito.

Kitendo cha kukaa muda mrefu bila ya kupata mtoto huku mkiwa mnamtafuta huitwa ugumba kwa hiyo unahitaji uchunguzi na tiba.

CHANZO CHA MATATIZO
Mwanamke kutopata ujauzito husababishwa na matatizo mengi kwa upande wake au mumewe.

Kwa upande wa mwanaume, vyanzo vinaweza kuwa kukosa nguvu kabisa au kupungukiwa nguvu za kiume tatizo liitwalo, ‘Erectile Dysfunction,’ tayari tumelizungumzia katika makala zilizopita.

Mwanaume anaweza kutoa manii mepesi sana kiasi kwamba baada tu ya kumaliza tendo mwanamke akisimama zinamwagika au zinatoka.

Dalili nyingine ni pale manii zinapopimwa hospitali na kuonekana zipo chache sana au hazina nguvu. Matatizo haya pia tayari tumeshayaeleza hapo nyuma.

Kwa upande wa mwanamke, vyanzo vinaweza kuwa matatizo katika mfumo wa homoni au vichocheo mbalimbali vya uzalishaji na upevushaji mayai na mzunguko. Mwanamke mwenye tatizo hili hupoteza siku zake za hedhi, mzunguko wa hedhi huvurugika na asijue ratiba yake ya mzunguko.

Pia hupoteza hamu na raha ya tendo, maumivu wakati wa tendo, hapati ute wa uzazi. Matatizo mengine ni kuziba kwa mirija ya uzazi, uwepo wa uvimbe katika mfuko wa uzazi, kupata damu ya hedhi kwa muda mfupi sana yaani moja au mbili au zaidi ya siku saba.

Pia kuumwa tumbo chini ya kitovu mara kwa mara, kutokwa sana na uchafu ukeni ambao wakati mwingine huambatana na harufu mbaya na muwasho pamoja na maumivu wakati wa haja ndogo.

Matatizo ya kutokwa na uchafu ukeni na muwasho havihusiani na ugonjwa wa yutiai ‘UTI’ kama wengi walivyozoea.

Matatizo mengine yanayomfanya mwanamke asipate ujauzito anapohitaji ni kutokufahamu siku za kupata mimba. Ili kufahamu siku za kupata mimba lazima ufahamu kwanza mzunguko wako uko vipi, mada hii tutakuja kuiongelea katika makala zijazo.

Vile vile mwanamke ajue siku zake za ‘Ovulation’ au siku za ute wa uzazi. Ute wa uzazi upo wa aina tatu, kuna mwepesi, mwepesi wa kuvutika na mzito.

Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply