The House of Favourite Newspapers

Mambo ya kufanya na yasiyotakiwa kwa mjamzito

KUWA mjamzito ni kitu cha furaha sana kwa wengina wengine huona kuwa ni mafanikio. Huongeza upendo na furaha. Kwa wachache huwa ni kama ajali, na hupatwa na huzuni. Tofauti hizi hutokana na mipango ya wanawake hao, hali zao za kimaisha na maandalizi yao.

Baada ya kupata ujauzito, kazi kubwa iliyopo mbele ni kulea vizuri ujauzito huo hadi kujifungua mtoto. Unaleaje vizuri ujauzito wako? Mambo gani huhatarisha afya yako na mtoto aliyepo tumboni?

MAMBO YA KUFANYA

Mwanamama mjamzito pamoja na mwanaume wake ni lazima wahakikishe afya njema ya mama na mtoto aliyepo tumboni kipindi chote cha ujauzito. Hii ni kwa siku nzima na kwa siku zote za ujauzito. Wahakikishe mazingira mazuri kwa mama mjamzito na mtindo mzuri wa maisha ili awe na afya njema.

Mama mjamzito afanye mambo yafuatayo: Kuanza kliniki na kuhudhuria kila mwezi bila kukosa, kupata elimu na ushauri wa mambo yanayotokea wakati wa ujauzito, mjamzito ajuwe dalili zote za hatari wakati wa ujauzito, tahadhari za kuchukua na mahali pa kwenda kupata msaada.

Mjamzito pia anatakiwa kuwa na bajeti ya malezi ya ujauzito na dharura yoyote inayoweza kujitokeza, kula chakula bora na kwa mtindo mzuri, kunywa maji ya kutosha, kula matunda mengi na kula sana mboga za majani, kufanya mazoezi ya kutosha na ashughulishe mwili na ajipumzishe kiasi cha kutosha kwa kulala angalau saa 8 usiku na saa 4 mchana pia.

Lakini pia mjamzito anatakiwa kujiburudisha na kujifurahisha kiasi cha kutosha kila siku na kuwa msafi mara zote. Hakikisha mazingira yote, vyombo vyote, nguo zote na mwili wote ni safi.

Mjamzito anatakiwa kujikinga na magonjwa yote – Ya kuambukizwa na yasiyo ya kuambukizwa, atumie dawa zote vizuri kama alivyoelekezwa na daktari.

Mjamzito hakikisha usalama mara zote. Kuwa makini zaidi na kemikali zote – dawa, vipodozi, vyakula vya kutoka kiwandani, dawa za kuua wadudu, rangi za kupaka nyumba nk. Pata ushauri kutoka kwa wataalam wa afya. Mara zote uliza kama hazitakudhuru au kumdhuru mtoto aliyepo tumboni.

Mama mjamzito pia anatakiwa kufanya uchunguzi wa mara kwa mara wa afya na kupata matibabu mazuri na kwa wakati. Pia ajuwe siku anazotarajia kujifungua na kisha ajiandae vizuri, angalau mwezi mmoja kabla. Kwa mjamzito, fika mapema hospitali ambayo umepangiwa kujifungulia

MAMBO YA KUEPUKA NA KUACHA KABISA

Kwa mjamzito, kuna mambo ya kuyaepuka au kuacha kabisa kama ulikuwa unayafanya.

Epuka/ acha kabisa kuvuta sigara, kunywa pombe na kutumia madawa ya kulevya. Acha kabisa matumizi mabaya ya dawa, dawa zisizoruhusiwa kwa wajawazito na vipodozi visivyo salama, acha kuvaa nguo za kubana na viatu vyenye visigino virefu.

Mjamzito unashauriwa usifanye kazi ngumu, usiwe na msongo wa mawazo. Waza vizuri bila kuwa na simanzi, epuka kukasirika mara kwa mara, hakikisha unakuwa na furaha na amani mara kwa mara, epuka jua kali, vumbi, na kukaa karibu na wanyama wafugwao nyumbani na mabanda yao.

Mjamzito pia epuka vyakula visivyopikwa na kuiva vizuri kwani vinaweza kukusababishia magonjwa, epuka kula sana kula kiasi sahihi na jishughulishe vya kutosha, epuka ugomvi na ajali.

USHAURI MUHIMU

Mjamzito usiwe msiri kwa wataalam wa afya. Toa taarifa na maelezo ya kutosha ili usaidiwe vizuri hasa kama kuna tatizo unaloliona lisilo la kawaida. Epuka kujifungulia nyumbani au sehemu pasipo na wataalam. Jitahidi siku zikikaribia kuwa karibu na hospitali uliyopangiwa kujifungulia, pia kuwa na uhakika wa usafiri wa kukuwahisha muda wowote ukihisi dalili.

Ukizingatia haya tuliyoyataja leo na mengineyo, utaishi vizuri na utajifungua salama mtoto mzuri akiwa na afya njema. Kwa ushauri zaidi unaweza kuwasiliana nasi kwa namba ya simu hiyo hapo juu ili uwe salama zaidi siku zote

Comments are closed.