The House of Favourite Newspapers

MAN UTD YAMTAKA STAA WA SPURS

KOCHA wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer ameamua atarusha kete yake kumnasa staa wa Tottenham Hotspur, Christian Eriksen wakati wa kipindi cha dirisha dogo la usajili mwezi Januari mwakani.

 

Manchester United ilijaribu kumsajili mwezi Julai mwaka huu lakini mpango huo ulikwama. Eriksen mwenye umri wa miaka 27 ameweka wazi anataka kuondoka Tottenham. Staa huyo wa timu ya taifa ya Denmark aligomea hata ofa ya klabu hiyo ya kuongeza mkataba. Eriksen ameweka wazi anataka changamoto mpya lakini ameshuhudia dili za kumsajili zikikwama,

Real Madrid na Barcelona ni klabu nyingine ambazo zilikuwa zinataka kumchukua kiungo huyo mshambuliaji. Solskjaer sasa anataka kurudi kumsajili Eriksen kutokana na kikosi chake kupwaya kwenye safu ya kiungo.

 

Kocha huyo alikuwa anamtegemea sana Jesse Lingard lakini ameshindwa kuonyesha cheche zake msimu huu kwani hajafunga bao wala kutoa asisti. Manchester United imefunga mabao matatu tu katika mechi tatu zilizopita ndio maana Solskjaer anaamini Eriksen ataweza kuongeza makali ya timu yake.

 

Klabu hiyo iliandaa kitita cha pauni milioni 70 ili kumnasa Eriksen lakini dili hilo lilikwama. Tottenham bila shaka itakuwa tayari kumuuza Eriksen mwezi Januari ili asiondoke bure mwishoni mwa msimu huu.

LONDON, England

Comments are closed.