The House of Favourite Newspapers

Manji afanya kufuru ya bilioni nne

0

MANJI.jpg Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji.

Wandishi Wetu, Dar es Salaam
WAKATI Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likiwa katika harakati za kuhakikisha mchezo wa soka unapiga hatua hapa nchini kwa kuwa na mashindano mengi yatakayowapatia fursa wachezaji wengi kuonyesha viwango vyao, Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, anatarajia kuliunga mkono shirikisho hilo ili liweze kufanikisha mikakati yake hiyo.

Inadaiwa kuwa, Manji hivi sasa yupo katika harakati kabambe za kutaka kuandaa mashindano makubwa kwa nchi za Afrika Mashariki ambayo yatakuwa yakishirikisha klabu mbalimbali kutoka katika mataifa hayo ambayo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.

muroMkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Yanga, Jery Muro.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga zimedai kuwa lengo kubwa la Manji kuanzisha michuano hiyo ni kuhakikisha mchezo wa soka unapiga hatua katika mataifa hayo ambayo yanaonekana kuachwa nyuma na mataifa mengine ya Afrika Magharibi, Kaskazini na Kusini.
“Lakini pia ni kuhakikisha wachezaji waliosajiliwa na klabu hizo, wanatumika ipasavyo kwa kucheza mechi nyingi zitakazowafanya kuwa sawa.
“Hivi sasa kiongozi wetu huyo, yupo katika harakati za kutafuta fedha ambapo anahitaji kama bilioni nne ili michuano hiyo iweze kuanza kutimua vumbi mara moja.
“Hata hivyo, kama mambo yatakuwa sawa, kila nchi itakuwa ikitoa timu tano kwenye ligi yake ya nyumbani kwa ajili ya kushiriki michuano hiyo ambayo kimtazamo itakuwa ni mikubwa zaidi kuwahi kutokea katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.
“Jinsi itakavyokuwa ikifanyika ni tofauti kabisa na ile ya Kombe la Kagame ambayo huandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ambapo kila nchi hutoa timu moja au mbili na mashindano kufanyika sehemu moja,” kilisema chanzo hicho cha habari na kuongeza:
“Michuano hii itakuwa ikifanyika kama ile ya Mabingwa Ulaya ambapo timu hucheza nyumbani na ugenini na mwisho wa siku fainali kupigwa katika nchi moja ambayo itachaguliwa, tumuombe Mungu aweze kumjalia afya njema ili atimize lengo lake hilo ambalo litakuwa na faida kubwa katika ukanda wetu huu.”
Alipotafutwa Manji ili aweze kuzungumzia suala hilo hakuweza kupatikana lakini jitihada zaidi zilifanyika na kumpata Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Yanga, Jery Muro.
Alipoulizwa kuhusiana na suala hilo hakuonekana kushtuka sana lakini mwisho alishindwa kukubali wala kukataa kuwepo kwa mpango huo.
“Nani kakwambia habari hizo?” Alihoji Muro kisha akaendelea kusema: “ Kwa sasa siwezi kusema chochote juu ya suala hilo kuwepo au kutokuwepo ila ninachoweza kusema ni kwamba tusubiri tuone.”
Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit, yeye alisema: “Mimi siyo msemaji wa klabu, msemaji ni Jerry Muro, kwa hiyo kila kitu anakizungumzia yeye, nikiwa na kitu nitamwambia yeye ndiyo azungumze na vyombo vya habari.”

Leave A Reply