Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umepewa tuzo kama ishara ya kuthamini mchango wake katika mapambano ya VVU na UKIMWI.
Tuzo hiyo ilitolewa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) na kukabidhiwa na mgeni rasmi ambaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, wakati wa maadhimisho ya siku ya UKiMWI duniani yaliyofanyika jijini Mbeya.
NSSF imekuwa ikitekeleza Sera ya UKIMWI mahala pa kazi na imekuwa ikisimamia miongozo yote inayohusu VVU na UKIMWI
Pia, Mfuko ulishiriki katika maonesho na maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani ili kuendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa Taifa kuendelea kujikinga na masuala ya VVU na UKIMWI.
Mkurugenzi Mkuu Bw. Masha J. Mshomba katika salamu zake kwa wafanyakazi wa Mfuko katika siku ya UKIMWI duniani alisema “Nasisitiza kuwa, ni wajibu wa kila mfanyakazi kuchukua hatua katika kudhibiti VVU na UKIMWI ili kuokoa nguvu kazi ya Mfuko na Taifa”.
Aidha, Mshomba alifafanua zaidi na kusema kwamba NSSF inayo sera inayohusu masuala ya VVU na UKIMWI ambayo inasisitiza kujilinda, kujikinga, kumlinda mfanyakazi aliyeathirika, kuzuia unyanyapaa na kumsaidia mfanyakazi aliyeathirika.
Kauli Mbiu ya mwaka huu ilikuwa “Zingatia Usawa, Tokomeza Ukimwi, Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko”.