The House of Favourite Newspapers

Mapazia ya chumbani -13

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

“Ila unahitaji uvumilivu wa hali ya juu!”

“Nipo tayari kwa vyovyote!” alisema mama Dick kwa kujiamini.

Wakakubaliana watengeneze kila njia ya kumdhalilisha mama Kirumba.

“Nipo tayari leoleo kumtafuta kijana mwenye umbo kama la shemeji, wewe jipange kwa upande wa meseji, sawa!”

ENDELEA NAYO MWENYEWE..

Muda ulizidi kusonga. Siku nzima mama Muro aliitumia kumtafuta kijana anayefanana na shemeji yake, mzee Mashali.

“Lakini pesa ipo mama?” alisema kijana mmoja aliyekutana na mama Muro.

“Tatizo wala siyo pesa, tutakupa!”

“Ni sehemu gani kwani?” aliendelea kudadisi kijana yule mwenye umbo kama la mzee Mashali.

“Kwangu si unapajua?”

“Napajua sana!”

“Kwa mama Dick je?”

“Mama Dick wa pale jirani yako?”

“Ndiyo huyohuyo!”

“Napajua.”

“Sasa kama unapajua kote huko, biashara imeisha kwani ni mazingira hayohayo.”

Mama Muro alikaa kwa muda mrefu kidogo na yule kijana huku akimpanga mtego utakavyokuwa.

“Kwa hiyo kwa mtego wote huo, nitengeeni elfu ishirini tu.”

“Elfu ishirini?”

“Ndiyo, wee kuvamia nyumba ya mtu usikuusiku, wakiniitia mwizi je?”

“Sikiliza kijana, elfu ishirini kubwa sana, kama ni kumi tutakupa na tutaanza kukupa tano kisha ukimaliza mchezo mzima tunakumalizia tano.”

Kijana yule alijifikiria mara mbilimbili kisha akajiangalia na maisha yake yalivyo ya kuunga mitaani.

“Sawa nimekubali.”

“Hayo ndiyo mambo sasa!”

“Kwa hiyo?”

 “Chukua hii elfu tano, ikifika saa mbili kamili usiku utanikuta kibarazani kwangu sawa!”

“Haina shida.”

Waliagana kisha mama Muro akarudi moja kwa moja hadi kwa mama Dick na kumpa mchapo mzima.

“Usinipe furaha kiasi hicho!”

“Kweli nakwambia na hapa ikifika saa mbili tu yupo maeneo ya kwangu.”

“Sasa tupange, akishakuja tunafanye?”

“Kabla hajaja tu hiyo saa mbili usiku, unachotakiwa ni kuhakikisha unapata simu ya shemeji na hii itakuwa rahisi sana kama tutatumia namba yake kuchati na mama Kirumba.”

“Mhhh!!”

“Unachoguna nini sasa!”

“Najifikiria jinsi ya kuipata hiyo simu ya mume wangu?”

“Mama Dick, kama uliweza kupata na kusoma meseji kwenye simu yake, unashindwa nini leo?”

“Sawa tutaangalia basi shoga!”

“Siyo utaangalia tu, nakutegemea na nipo hapa kwa ajili ya kumnyoosha huyo mdandia waume za watu.”

Mama Muro na mama Dick walikubaliana kisha kila mmoja akaelekea nyumbani kwake.

* * *

Jua lilikuwa limempiga sana mzee Mashali. Kutwa nzima aliambulia shilingi laki moja tena ni ile aliyokuwa amepewa na mama Kirumba kama sehemu ya hela yake baada ya kumuuzia mapazia.

“Bora gereji, jua limenichoma sijaona kitu. Je mama Kirumba asingeniungisha?” alijisemea mzee Mashali kwa sauti ya kilevi baada ya kufika nje mlangoni kwake na fuko la mapazia.

“Pole mume wangu!” mama Dick alimkaribisha kwa kubeba lile fuko la mapazia na kuongoza hadi sebuleni.

“Mbona umechoka sana kulikoni?”

“Wee acha tu!”

“kuna tatizo?”

“Hii biashara inahitaji moyo sana, nimepigwa sana na jua.”

“Lakini si umeuzauza?”

“Niuze wapi?, nimefanikiwa kuuza kwa mtu mmoja tu kati ya hamsini waliyoyaangalia.”

“Usijali mume wangu, safari ndiyo kwanza imeanza, kuwa mvumilivu mpaka utakapozooleka sana,” alisema mama Dick kwa kumpa moyo huku akili yake yote akiilekeza kwenye simu ya mumewe. Ujio wake tena akiwa katika hali ya kulewa ulimpa furaha kubwa moyoni.

“Nikuandalie maji ya kuoga?” aliuzia mama Dick kimtego.

“Hapana, hata chakula sili.”

“Kwa nini mume wangu?”

“Nimekula huko nilikotoka, nilipitia kwa mama ntilie,” alisema mzee Mashali huku akipepesuka na kuelekea chumbani. Hakuwa mzee Mashali wa kawaida, pombe zilimzidia nguvu na kujikuta akijibwaga kitandani.

Furaha ya mama Dick ilikuwa haielezeki. Aliona kama miujiza kurudi kwa mumewe akiwa amelewa. Aliingia chumbani na kuzima taa kisha akamfuata mzee Mashali na kuanza kuingiza taratibu kwenye mifuko yake ya suruali na kutoka na simu.

Akafunga mlango kwa funguo na kuelekea kwa mama Muro kukamilisha mtego.

Leave A Reply