The House of Favourite Newspapers

‘MAPEPO’ YA ROSE MUHANDO YAMUIBUA MBASHA

Emmanuel Mbasha

VIDEO iliyosambaa mitandaoni ikimwonyesha muimbaji maarufu wa Injili, Rose Muhando, akiwa anaombewa baada ya kupagawa na mapepo imeshtua watu wengi.   

Video hiyo inayomwonyesha Muhando akiwa amedhoofu na amejaa makovu kama ameungua moto, ilisambaa kwa kasi jana kwenye mitandao mbalimbali, jambo ambalo limeibua nadhari ya watu wengi kutaka kujua kilichompata mtu huyo maarufu.   

Miongoni mwa waliojitokeza kuzungumzia jambo hilo ni mwimbaji wa nyimbo za Injili, Emmanuel Mbasa, ambaye, kupitia ukurasa wake wa Instagram ameandika yafuatayo:

“Nikiwa kama baba wa kiroho na mlezi mkuu wa waimbaji wote wa nyimbo za Injili Tanzania, napenda kuweka wazi kuwa nimehuzunishwa sana na hii video ya maombezi ya muimbaji mwenzetu Rose Muhando.

“Kwa unyenyekevu kabisa naweza kusema kuwa, maombi ni muhimu sana kwa watu wote, ila namna ya kuombea ikiwa mbaya inaweza kuharibu umuhimu wote wa maombi na kusababisha maombi yadharaulike au yamdharaulishe aliyeombewa.

“Katika nia yangu ya ndani nimefurahishwa sana na kitendo cha Rose kuombewa, ila kero yangu kubwa imekuwa kwenye njia iliyotumika kumuombea. Rose Muhando ni star, na katika medani za muziki wa Injili ni mtu anayetazamwa na watu wengi sana kama rolemodel wao, hivyo nadhani ilikuwa ni bora zaidi kuwa waangalifu katika kumuombea ili kulinda brand yake.

 

“Biblia inasema, mwenye heshima apewe heshima, hivyo kwangu mimi sidhani kama mchungaji aliyemuombea Rose amempatia heshima anayostahili, maana binafsi sikuona haja ya kuwasha camera na kuanza kumuombea hadharani vile.

 

“Hali hii inaweza kumtangaza sana muombeaji lakini kwa upande wa muombeaji inaweza kuzidisha tatizo na kusababisha adharaulike zaidi kwenye jamii inayomtazama. Watumishi wa Mungu wanahitaji kuwa na hekima pamoja na kifua cha kutunza siri, na siyo kufanya mambo kwa mihemko huku mkitazama maslahi yenu.

 

“Mimi nadhani ingekuwa bora sana endapo mchungaji angemuombea ofisini, na kama maombi yangeleta majibu naamini video ya shuhuda ambayo Rose Muhando angeongea wakati akiwa na akili zake timamu ndiyo ingefaa kusambaa na kuendelea kumjengea heshima yeye pamoja na mtumishi aliyemhudumia.

 

“Kumbuka yule akida (mkuu wa vikosi cha askari wa Kirumi) alipohitaji maombi kwa Yesu, Biblia inasema Yesu alifunga safari kwenda nyumbani kwake ili kumuombea. Unadhani ni kwa nini hakumwambia alete askari wake mgonjwa amuombee hadharani kama akina Batromayo?

 

“Hii ilikuwa ni hekima ya kulinda heshima ya muombewaji. Maana huwezi kumuombea rais kama unavyoombea ombaomba au mpiga debe!

 

“Kwa kweli nimeamua kuwa muwazi na kuziweka huzuni zangu hadharani ili waombeaji mjirekebishe. Siyo kila maombi yafanyike wakati caméra ziko on, kuna mengine ya kuzima camera na kuomba kwa staha ili kuendeleza uhai na kipawa,” alisema Mbasha.

 

Hata hivyo, hali ya msanii huyo kwa sasa anaendelea vizuri, ambapo kwa sasa yupo kwenye ziara nchini Kenya ambako ndiko alikokuwa akiombewa kama video inavyoonyesha. Baada ya kuombewa na mapepo kulipuka kwa sasa anaendelea vizuri na baada ya kumaliza ziara Kenya, ataenda Uganda na atamalizia Zambia.

MAJINI Yamtesa Rose Mhando!, Asimulia Mazito Akiombewa

Comments are closed.