The House of Favourite Newspapers

MAPISHI YA LEO! WALI WA KUKAANGA NA MAYAI

MAHITAJI

-Wali uliopikwa vikombe vitano.

-Mayai matano.

-Manjano robo kijiko cha chai

-Mafuta vijiko viwili vya chakula.

-Kitunguu maji kimoja kilichokatwakatwa.

-Hoho nyekundu zilizokatwakatwa nusu kikombe.

-Njegere zilizoganda na kuacha zikayeyuka nusu kikombe.

-Chumvi kiasi.

-Sukari robo kijiko cha chai.

-Pilipili manga robo kijiko cha chai.

-Vitunguu vya majani viwili vilivyokatwakatwa

 

KUTAYARISHA NA KUPIKA

Chukua wali ambao umeshapika uchambue vizuri kisha utie katika sahani au sinia pana, acha upoe kabisa.

Vunja mayai matatu katika bakuli moja, kisha vunja mayai mengine mawili pamoja na maji vijiko viwili vya chakula, tia manjano kisha ziweke pembeni bakuli zako zote mbili.

Baada ya hapo weka kikaangio au sufuria yako jikoni, weka moto wa kiasi kisha tia mafuta ya kula vijiko viwili vya chakula, yakipata moto weka mayai matatu uliyoyavunja, bila viungo yavurugevuruge, epua weka pembeni.

 

Weka tena chombo jikoni katika moto mkali, tia mafuta kijiko kimoja cha chakula. Yakipata moto weka vitunguu na hoho kisha kaanga kwa dakika mbili.Tia wali wako kisha geuzageuza vizuri ili wali upate moto vizuri.

Mimina mayai mabichi uliyoyakoroga na viungo juu ya wali wako kisha kaanga kwa dakika moja hadi mayai yaenee vizuri katika wali.

 

Chukua njegere, weka kisha koroga bila kuachia kwa muda wa dakika moja, nyunyizia chumvi, (na sukari ukipenda) na pilipili manga juu ya wali wako kisha koroga vizuri kuchanganya.

Ukiona wali mkavu sana nyunyizia maji ya uvuguvugu kidogo au supu.

Baada ya hapo acha uive vizuri kisha weka mezani tayari kwa kula.

Gladness Mallya +255 654 880707

Comments are closed.