The House of Favourite Newspapers

Marekani Yaidhinisha Dawa ya Dharura Kwa Wagonjwa wa Corona

0

MAREKANI leo Mei 2, 2020 imeidhinisha majaribio ya dawa ya dharura itakayotumika kwa wenye virusi vya corona, wakati majimbo zaidi nchini humo yakilegeza masharti ya kutotoka nje licha ya vifo vitokanavyo na virusi hivyo kuzidi kuongezeka.

 

Kuidhinishwa kwa dawa hiyo ni hatua ya hivi karibuni ya juhudi za dunia kupata tiba kamili na chanjo ya virusi vya corona vilivyowaacha nusu ya watu duniani wakibakia nyumbani, kuutikisa uchumi wa dunia na kuwaambukiza watu zaidi ya milioni 3.3 ulimwenguni.

 

Dawa hiyo inayojulikana kama Remdesivir, iliyotengenezwa kupambana na ugonjwa wa ebola iliidhinishwa baada ya majaribio kadhaa kuonesha imewasaidia wagonjwa mahututi wa COVID 19 kupata nafuu.

Marekani ina wagonjwa milioni 1.1 wa virusi vya corona na kurekodi vifo 65,000 hali inayomfanya rais Donald Trump kuwa mbioni kubadili hali wakati taifa hilo lililo na uchumi mkubwa duniani likirekodi idadi kubwa ya watu waliokosa ajira kutokana na janga la virusi hivyo.

 

Ruhusa ya kutumika kwa dawa hiyo kwa sasa imetolewa kwa watu ambao wamelazwa hospitalini tu kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

 

Jaribio la hivi karibuni la kitabibu linaonyesha kuwa dawa hiyo inaweza kuwasaidia watu mahututi wanaoumwa corona, na inaaminiwa kuwa inaweza kuwasaidia kupona haraka.

Wataalamu wa dawa wametoa onyo kuhusu dawa hizo -ambazo zilitengenezwa ili kutibu Ebola, na zilitengenezwa na kampuni ya Gilead pharmaceutical iliyopo mjini California -kwamba visionekane kuwa ni jambo la ajabu sana kwa dawa hiyo kuanza kutumika kwa ajili ya kutibu virusi vya corona.

 

Katika kikao na Rais wa Marekani Donald Trump katika ofisi za Oval, Mkurugenzi Mkuu wa Gilead Daniel O’Day alisema Mamlaka ya Dawa (FDA) ndiyo hatua muhimu ya kwanza.

 

Kampuni hiyo itachangia chupa za dawa hiyo milioni 1.5 , alisema.

Kamishina wa FDA, Stephen Hahn alisema kwenye mkutano huo: “Hii itakuwa tiba ya kwanza ya Covid-19 kupitishwa , tumefurahi sana kuwa sehemu ya uwezeshaji huo.”

 

Mamlaka ya dharura ya FDA si sawa na ile ambayo inatoa idhini rasmi ambayo inahitaji uangalizi wa hali ya juu zaidi.

 

Katika jaribio la kitabibu, taasisi ya taifa ya mzio na magonjwa yanayoambukiza nchini Marekani (NIAID) imebaini kuwa remdesivir inapunguza muda wa dalili za ugonjwa huo kutoka siku 15 mpaka siku 11.

 

Jaribio la dawa hilo lilifanyika kwa watu 1,063 katika hospitali mbalimbali duniani, – zikiwemo Marekani, Ufaransa, Italia,Uingereza, China na Korea kusini. Baadhi ya wagonjwa walipewa dawa hiyo na wengine walipewa tiba ya ‘placebo’.

 

Dkt Anthony Fauci ambaye anaiongoza NIAID, alisema kuwa remdesivir imeonyesha wazi umuhimu wake, kikubwa ni kuharakisha muda wa mtu kupona.

 

Hata hivyo remdesivir inaweza kusaidia katika uponyaji – na kuzuia watu kutibiwa kwenye chumba cha dharura – majaribio ya dawa hiyo haijaonyesha wazi kuwa inaweza kuzuia watu kufa kutokana na virusi vya corona.

 

Wakati maswali mengi yakiwa hayana majibu bado kuhusu muongozo wa tiba hiyo, Gilead alishauri kuwa wagonjwa watumie dozi ya siku kwa wale ambao wanatumia mashine ya kupumulia na siku tano kwa wagonjwa ambao hawatumii mashine

Leave A Reply