The House of Favourite Newspapers

Marioo Aibua Vita Mpya Mondi, Harmo

0

BWA’MDOGO anayefanya poa kwa sasa kwenye anga la Bongo Fleva, Omari Mwanga ‘Marioo’, ametajwa kuwaingiza kwenye vita mpya, mastaa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Rajab Abdul ‘Harmonize’, IJUMAA WIKIENDA limedokezwa.

Chanzo makini kimepenyeza ubuyu kuwa, Marioo, kijana anayetajwa kuwa ‘moto’ kwa mwaka huu wa 2020, anawaingiza Diamond au Mondi na Harmonize au Harmo kwenye vita ya kumgombea kwani wote wanatajwa kuiwania saini yake.

“Mondi anamtaka huyu dogo sababu ameona uwezo wake. Anataka amsajili kwenye lebo yake ya Wasafi Classic Baby (WCB), lakini pia kule kwa Harmo nako wanamhitaji ili kuendelea kuiimarisha lebo yake ya Konde Music World Wide,” kilisema chanzo hicho.

VITA YATANDA MITANDAONI

Wakati chanzo kikiwa kimelitonya Gazeti la IJUMAA WIKIENDA kuhusu ishu hiyo, huko mitandaoni nako kukachafuka ghafla kufuatia mashabiki wa Mondi kuchuana na wale wa Harmo baada ya picha za Mondi akiwa na Marioo kusambaa.

PICHA ZENYEWE…

Picha hizo zilizosambaa ziliwaonesha Mondi akiwa na Marioo walipokutana jijini Lagos nchini Nigeria kwenye Tuzo za Sound City ambapo wawili hao walikuwa miongoni mwa wasanii waliokuwa wakiziwania tuzo hizo.

MASHABIKI WAJIONGEZA

Picha hizo mbalimbali ziliwaonesha wawili hapo kuwa na ukaribu mkubwa kushibisha hoja za kwamba, huenda bwa’mdogo huyo yupo kwenye harakati za kusainiwa na lebo hiyo kubwa nchini.

“Deal done, mliokuwa mnasema ataenda ku-side (kuwa upande) kwa Harmo imekula kwenu, Harmo ana nini cha kushindana na Mondi?” Alihoji mdau mmoja mtandaoni.

TIMU HARMO YACHARUKA

Kufuatia kauli hiyo, mashabiki wanaomuunga mkono Harmo waliibuka kama nyuki mitandaoni na kuanza kujibu mashambulizi. Mashabiki hao walifikia hatua ya kutukanana huku kila mmoja akionesha ni jinsi gani upande wake ni bora kuliko mwingine.

Mashabiki wa Harmo walisema, msanii wao ana akili kubwa na ndiyo maana hata hao Wasafi wanahaha kutafuta mtu wa kuziba pengo la Harmo ambaye aliachana na Wasafi mwishoni mwa mwaka jana.

“Hili ni pigo la pili, upande wa pili huko wanangaika kupata mbadala wa Harmo maana tangu aondoke, pengo lake halijazibwa,” alichangia shabiki wa Harmo.

Wengine walikwenda mbele zaidi kwa kusema Marioo ni mali yao kwa kuwa ana ukaribu na kituo kimoja cha redio ambacho kina utofauti na Mondi.

“Walie tu, Harmo atamsaini tu kiurahisi si unajua yupo upande huu wa redio ambayo haimsapoti Mondi?” Alichangia mdau huyo wa Harmo huku akisindikiza ujumbe huo na picha za Harmo akiwa na Marioo kushibisha hoja yake.

MARIOO ATEGUA UTATA

Baada ya vita hiyo mpya kukolea mitandaoni, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA liliingia mzigoni na kutaka kujua ukweli wa mambo.

Kubwa zaidi IJUMAA WIKIENDA lilimvutia waya mhusika mkuu, Marioo ili kujua kama ana msimamo gani kuhusu usajili uliozua mtafaruku.

Ajabu sasa, Marioo alisema hana mpango wowote wa kusainiwa na lebo yoyote na kama haitoshi, akazungumzia ukaribu wake na Mondi ambao ndiyo unaonekana kuchagiza maneno mengi mitandaoni. Alisema ni tabia yake ya kuwa karibu na wasanii waliomtangulia kama Mondi kwenye gemu kwani hujifunza mambo mengi.

“Hizo tetesi nimezisikia sana, lakini napenda kuwaambia mashabiki wangu kuwa wazipuuze, mimi kuonekana kuwa na ukaribu na Mondi haimaanishi ndiyo ninasainiwa Wasafi, bali ni tabia yangu ya kuwa karibu na wasanii walionitangulia kwenye gemu. “Jamaa (Mondi) ni miongoni mwa wasanii wenye mengi ambayo ninaweza kujifunza kutoka kwao,” alisema Marioo.

VITA ILIANZA KITAMBO

Hii si mara ya kwanza kwa mashabiki kuwaingiza Mondi na Harmo kwenye vita yao (japo wenyewe hawaweki wazi), awali, walizua tafrani wakati Harmo anaondoka Wasafi.

Hiyo ni baada ya Harmo kuzungumza kwamba Mondi alimzuia kutumia nyimbo zote alizofanya akiwa Wasafi hadi atakapolipa shilingi milioni 500 za kuvunja mkataba. Chuki ilikuwa kubwa kwa mashabiki ambapo walianza kutoa ushahidi wao kuonesha kwamba wawili hao picha haziivi japo wenyewe hawakudhihirisha hadharani kama wana tatizo au hawaelewani.

MARIOO NI NANI?

Marioo ni miongoni mwa wasanii wanaofanya poa kwa sasa kunako gemu la Bongo Fleva na tayari ameshaanza kuvuka mipaka kwani mapema mwaka huu alitajwa na waandaaji wa Tuzo za Sound City kuwa miongoni mwa wasanii wanaokuja kwa kasi barani Afrika. Miongoni mwa ngoma zake zilizomuweka kwenye ramani na kukubalika vilivyo ni Inatosha na sasa anasumbua na Aya.

Baadhi ya mashabiki mitandaoni wamempa tahadhari dogo huyo wakisema awe makini, asilewe sifa kwani anaweza kupotea. Wengine wamedai kuwa ndiye mbadala sahihi wa Harmo kama atasajiliwa Wasafi na atafika mbali hususan katika nyanja za kimataifa.

 

Leave A Reply