Marioo: Kungekuwa na Tuzo Ningejaza Kabati!

“Tikisatikisa, mbona nikaa nataka kufa…

Mbona nikaa sijielewi…

Nipe kubwa nipe na ndogo..

Changamka usiwe gogo..

Zikipanda nakuwa gogo…

Sikawii kuzua zogo..

Inavyo knockdown…

Inanikata ah ah..

Usinimwage mwage bwana gambe’’.

NI sehemu ya mistari mikali iliyo ndani ya mkwaju mpya wa Tikisa wa dogo ambaye kwa sasa anaweka alama kwenye ramani ya Bongo Fleva.

Tangu anaanza na Ngoma ya Dar Pagumu, Aya, Inatosha, Unanikosha, Raha, Nyatunyatu, Anyanyinya na Unanionea, aisee hajawahi kulegea.

Jina halisi ni Omari Mwanga almaarufu Marioo ‘Toto Bad’.

Ameutawala muziki vizuri. Amepita kwenye mikono ya mtu mzima, Sweetbert Charles wengi wanamfahamu kama Producer Abbah Process.

Abbah amekuwa nyuma ya mafanikio na kazi kali za Marioo ambazo zinakimbiza balaa sokoni.

Baada ya kuachia mikwaju yote mikali, Marioo amekuja kuwashangaza mashabiki wake baada ya kuachia ladha ya tofauti na alivyozoeleka.

Mkwaju mpya ambao anatamba nao ni Tikisa ambao aliuachia rasmi Julai 17, mwaka huu na unafanya poa kwenye Mtandao wa YouTube. Tayari ngoma hiyo imetazamwa zaidi ya mara laki tatu ndani ya siku tano.

IJUMAA SHOWBIZ imekusogeza karibu na Marioo na amefunguka mengi ikiwemo kazi zake na lebo yake ya Bad Nation. Ungana naye;

IJUMAA SHOWBIZ: Kwa nini umeamua kubadili ladha ya muziki wako tofauti na ulivyozoeleka?

MARIOO: Tangu nimeanza kutoa nyimbo zimekuwa ni za kutulia, watu walikuwa wanataka nitoe ngoma kama Tikisa. Mara nyingi nimekuwa nikifanya vitu vyangu kwa hatua, hivyo huu ni wakati sahihi wa kutoa ladha kama ilivyo kwenye Tikisa.

IJUMAA SHOWBIZ: Je, mapokeo yake yakoje?

MARIOO: Mapokeo yake ni mazuri, komenti nyingi za mashabiki zinasema hivyo. Huwa napenda sana kusikiliza mashabiki wangu na Tikisa imepokelewa kwa shangwe maana napata simu nyingi ndani ya Dar na mikoani.

IJUMAA SHOWBIZ: Kipindi cha Corona hukuweza kupafomu, je, kwa sasa umejipanga vipi na shoo?

MARIOO: Nimejipanga vizuri na shoo yangu ya kwanza itakuwa mwisho wa mwezi huu mkoani Kigoma, nitakuwa na King Kiba. Nitafanya shoo nzuri, watu wa Kigoma wata-enjoy maana napendwa sana Kigoma.

IJUMAA SHOWBIZ: Je, ni dau la bei gani ambalo limekufanya kupafomu shoo hiyo?

MARIOO: Dau limekuwa kubwa kidogo na nilikuwa na shoo nyingine, ikabidi niivunje kwanza.

IJUMAA SHOWBIZ: Unadhani shoo hiyo na King Kiba itakupa mafanikio gani kwenye muziki wako maana Kiba ni mwanamuziki mkubwa?

MARIOO: Shoo ile itanipa vitu vikubwa kwa sababu mimi ni mwanamuziki mzuri na niko na mwanamuziki mkubwa ambaye ni mkongwe kwenye gemu hivyo itakuwa na faida kubwa.

IJUMAA SHOWBIZ: Je, mipango ya kufanya kazi ya pamoja na Kiba ikoje?

MARIOO: Niseme asante kwa kuwa karibu na kaka yangu Kiba. Ameonesha kukubali kile ninachokifanya, niwaahidi mashabiki kuwa lolote linaweza kutokea kwa sababu tuko kuendeleza muziki mzuri.

IJUMAA SHOWBIZ: vipi kuhusu kutoboa kimataifa?

MARIOO: Mipango ipo ila tatizo ni Corona ilisimamisha vitu vingi maana kuna nchi nyingi bado janga hili lipo. Dunia nzima ikitulia nakuja kuliamsha maana tayari nimeshafanya ngoma na msanii wa Ghana, Nigeria, Zimbabwe na Namibia hivyo kazi zinakuja.

IJUMAA SHOWBIZ: Kwa upande wako unazungumziaje suala la tuzo hapa Bongo?

MARIOO: Ni jambo zuri maana tuzo zinaleta chachu ya kufanya kazi. Mimi kama zingekuwepo tuzo kwa upande wangu kabati lingejaa maana nyimbo zangu nyingi zilikuwa zina-hit na ningechukua tuzo nyingi. Suala la kukosekana kwa tuzo linaninyong’onyesha.

IJUMAA SHOWBIZ: Mipango yako mingine ikoje?

MARIOO: Ni mwendelezo wa kufanya vitu vingine vikubwa na hata album yangu ya kwanza inatoka mwakani.

IJUMAA SHOWBIZ: Unamzungumziaje Diamond Platnumz?

MARIOO: Ninamshukuru sana kwa jinsi alivyonifundisha njia za kuwa mwanamuziki bora. Hata nilipokwenda naye Nigeria nilihisi kabisa nakwenda kuchukua tuzo, japo nimekosa ila hata nilivyokuwa narudi mashabiki wangu walinipokea kwa furaha.

IJUMAA SHOWBIZ: Unamzungumziaje Zuchu kama msanii ambaye kwa sasa yupo kileleni?

MARIOO: Zuchu ni rafiki yangu sana tu, hata niliposikiliza ngoma yake ya kwanza niliua ana kitu ndani yake. Nimpongeze Zuchu yuko mikono salama. Si yeye tu hata Ibrah, Jay Melody, Whozu na wengine wote wanafanya vizuri.

IJUMAA SHOWBIZ: Je, mapokezi yake kwa mashabiki umeyaonaje?

MARIOO: Mapokezi yake ni mazuri kwa sababu ana kipaji.

IJUMAA SHOWBIZ: Je, kwa promo anazofanyiwa Zuchu kama wasemavyo watu ni sawa kwa msanii?

MARIOO: Promo ni muhimu kwa msanii ikiwemo muziki mzuri na video kali. Si dhambi kwa msanii kufanyiwa promo hivyo kwa Zuchu amestahili hivyo kutokana na kipaji chake.

IJUMAA SHOWBIZ: Muziki umekufungulia mafanikio gani?

MARIOO: Nina yadi (sehemu ya kuuza magari) ambayo nimekodisha na kuna vijana wangu ambao nimewatafuta wanafanya kazi. Pia kwa sasa nina lebo yangu ya Bad Nation.

IJUMAA SHOWBIZ: Je, hiyo lebo yako imeshaanza kusimamia kazi za wasanii?

MARIOO: Tayari kuna watu ambao wameanza kunifuata japo bado sijaitambulisha rasmi, lakini imeanzia kwenye kazi zangu. Najipanga ili iwe ni lebo ambayo ina misingi mizuri, mizizi mizuri hata ninaposema namsaidia msanii, basi niwe namsaidia kwelikweli.

IJUMAA SHOWBIZ: Umekuwa ni msanii ambaye una mafanikio mazuri kwenye kazi zako, je, nini siri ya mafanikio?

MARIOO: Mimi naamini kwenye kufanya kazi, heshima kwa kila mtu kwa sababu iko siku nitarudi kama raia wa kawaida. Kuishi sawa na kila mtu pia nina menejimenti inayonisimamia.

IJUMAA SHOWBIZ: Nafasi ya Abbah iko vipi kwenye kazi zako?

MARIOO: Abbah ni mlezi wangu yupo katika kila ninachofanya. Nimetoka naye mbali kabla ya kuwa Marioo.

IJUMAA SHOWBIZ: Nyimbo zako ni kali na zinafaa kuwekwa kwenye mjumuiko mmoja, je, umewaza kuandaa album?

MARIOO: Kwa upande wangu kutoa album au EP ni kitu kizuri maana ndiyo hatua ya msanii kwa hiyo ipo kwenye mawazo yangu na timu kwa jumla.

IJUMAA SHOWBIZ: Gemu ni gumu, je, mikakati yako ikoje?

MARIOO: Mikakati ni mikubwa maana lengo letu kubwa ni kuitangaza Tanzania na kumuomba Mungu na kufanya kazi kwa bidii.

MAKALA: HAPPYNESS MASUNGA NA KHADIJA BAKARI, BONGO

Toa comment