The House of Favourite Newspapers

Mbelgiji Aja na Mikakati Mikali ya Kusuka Kikosi

0

KATIKA kuhakikisha anakuwa na kikosi imara cha kubeba makombe, Kocha Mkuu wa Yanga, Mbelgiji, Luc Eymael amewaambia mabosi wake kuwa katika usajili wake wa msimu ujao anahitaji wachezaji wenye ubora watakaoingia moja kwa moja katika kikosi chake cha kwanza.

 

Tayari timu hiyo imeshamalizana na baadhi ya wachezaji kimyakimya katika kuelekea dirisha la usajili msimu ujao unaotarajiwa kufunguliwa Agosti 2, mwaka huu.

 

Kati ya wachezaji wanaotajwa kuwepo kwenye mipango ya kusajiliwa Yanga ni Eric Rutanga (Rayon Sports), Heritier Makambo (Horoya AC), Tuisila Kisanda (AS Vita), Hassan Kessy (Nkana Rangers), Awesu Awesu (Kagera Sugar) na Ibrahim Ame ‘Varane’ (Coastal Union).

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, wadhamini wa Yanga ambao ni GSM tayari wamekamilisha usajili wa wachezaji wote aliowapendekeza kocha wao watakaoanza kutua nchini kuanzia Agosti 2, mwaka huu tayari kujiunga na wenzao.

 

Mtoa taarifa huyo alisema wachezaji hao watawahi kuripoti tayari kwa kuanza kambi ambayo hawataivunja baada ya ligi msimu huu kumalizika kwa lengo la kuanza ‘pre-seasson’ pamoja na wachezaji wenzao ili waiwahi ligi msimu ujao.

 

Aliongeza kuwa lengo la kutovunja kambi ni wachezaji kupata nafasi ya kukaa pamoja na kuzoeana kwa haraka baada ya kukibomoa nusu ya kikosi cha kwanza cha msimu ujao huenda kikabakiwa na nyota watatu hao wengine wote wapya.

 

“Ijumaa iliyopita Kamati ya Usajili ya Yanga ilikutana na kupitia kwa makini ripoti ya kocha aliyoitoa kwa viongozi, kikubwa iliangalia mapendekezo ya wachezaji ambao amewapendekeza tutakaowasajili kwa ya msimu ujao ambao kwetu muhimu.

 

“Katika ripoti hiyo aliyoitoa ametaka usajili wa wachezaji saba wapya ambao wataingia moja kwa moja katika kikosi chake cha kwanza baada ya kuona upungufu wa timu yake katika msimu huu, zipo baadhi ya nafasi ambazo zipo wazi lazima ziboreshwe.

 

“Kati ya hiyo ni safu ya ushambuliaji ambayo imetufanya tukose ubingwa wa ligi na Kombe la FA, hivyo kati ya mapendekezo hayo ya kocha aliyoyatoa kwa asilimia mia moja wachezaji wote tumekamilisha mazungumzo nayo na kilichobakia ni wao kuja kusaini na kuanzia Agosti 2, mwaka huu wachezaji hao wataanza kutua nchini.

 

“Mara baada ya kusaini, moja kwa moja wataingia kambini kwa ajili ya kuanza maandalizi ya msimu ujao, lengo la kuanza mapema kambi ni kuhakikisha wanazoeana kwa haraka kutokana na nusu ya kikosi cha kwanza cha msimu huu kupanguliwa na kusukwa kipya, lengo ni kuchukua makombe yote yatakayokuwepo mbele yetu,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Mkurugenzi Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said, hivi karibuni aliliambia Championi kuwa: “Kwa asilimia mia moja tumeshamalizana na wachezaji wote tunaowahitaji na kikubwa tumesuka kikosi imara cha kuchukua makombe katika msimu ujao.

 

“Niwatoe hofu Wanayanga wote kuwa msimu ujao utakuwa wetu, lazima tuchukue ubingwa wa ligi na kama hatujauchukua, basi lawama zote zije kwetu GSM, kwani msimu huu tumeingia katikati ya msimu huu.”

Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Leave A Reply